Leo Septemba 15 ni siku ya Demokrasia Duniani. Siku hii huaadhimishwa na mataifa mbalimbali, tarehe kama ya leo tangu ilipotangazwa na Umoja wa Mataifa mwaka 2007.
Hii ni siku adhimu na muhimu kwa watu na mataifa yote ambayo demokrasia imekuwa sehemu ya maisha na utamaduni wao. Kwa watu na mataifa ambayo demokrasia bado ni ndoto, kama hili la kwetu, hii ni siku ya kufanya tafakuri .
Hivi sasa dunia imekazia suala la demokrasia kupitia mikataba kadhaa ambayo ina nguvu ya kisheria lakini bado kuna nchi zinawanyima raia wake haki hiyo ambayo inastahiki kuwepo.
Demokrasia ina matawi yake kadhaa yakiwemo; Haki za Binaadamu, Uhuru wa Maoni, Uhuru wa Kujikusanya na Kujiunga (Kujumuika), Uhuru wa Kupiga Kura na Kuchagua na kadhalika ambapo kwa baadhi ya nchi mambo hayo yamewekwa kwenye katiba ikiwemo nchi za Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
ACT Wazalendo inapenda kutoa kauli ya wazi kuwa nchini Tanzania kwa sasa "demokrasia ipo kizuizini." Tunasema hivyo kwa sababu Serikali imetamka wazi kusitisha michakato ya kidemorasia kwa kisingizio cha kujenga uchumi.
CCM inaamini kuwa kwa kukusanya kodi na tozo za manyanyaso ili kujenga vituo va afya, mashule, barabara, miradi ya maji na kadhalika, wataweza kuwanyamazisha wananchi na hivyo kuwatawala milele Watanzania. Ni bahati mbaya kuwa uongozi wa serikali ya CCM kwa makusudi unajisahaulisha uhusiano usiokinzana baina ya demokrasia na ujenzi wa uchumi endelevu.
Watanzania wa miaka zaidi ya 100 iliyopita walithamini sana Uhuru wao kuliko vitu walivyopewa na Wajerumani kama mashule, barabara na hata Reli ya Kati.
Waliamini kuwa watu wakiwa huru wanaweza kupata vitu hivyo wao wenyewe na kwa kuthamini utu wao. Mbegu iliyopandwa na wazee wetu miaka hiyo ambayo ilisambaa mikoa yote bado inachemsha damu zetu. Ndio ilichemsha damu za Waasisi wa Taifa letu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Sheikh Abeid Karume kwani walipigania Uhuru licha ya kuwa Mkoloni Mwingereza alijenga reli, mabarabara, bandari, madaraja, nk.
Uhuru wa watu kujieleza, kujiunga, kukosoa Serikali na Uhuru wa kujiamulia mambo yao wenyewe ulikuwa ni muhimu zaidi kuliko vitu. Mbegu hii pia ndio inaendelea kuchemsha damu ya Watanzania wanaoitakia mema nchi hii kuendeleza harakati za kudai uhuru wa Watu na kutetea Demokrasia yetu.
Bahati nzuri Tanzania tunayo mifano iliyo dhahiri ya hivi karibuni. Mfano kwa upande wa Zanzibar, hakuna Mzanzibari hata mmoja ambaye alinusurika na uhasama, chuki na ugomvi wa kisiasa uliokuwa umetamalaki katika visiwa hivyo, ambao wakati mwengine uliteteresha hata usalama wa nchi na hivyo kuvuruga mipango endelevu ya kiuchumi kutokana na kuvunja tawi moja tu la demokrasia la Uhuru wa Kupiga Kura na Kuchagua katika miaka ya 2001- 2020.
Madhira ya Uchaguzi wa serikali za Mitaa mwaka 2019 na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 uliandika historia mpya nchini mwetu juu ya kile kilichoelezwa awali kuwa ni demokrasia kuwekwa kizuizini.
Kwa muktadha huo ni dhahiri serikali ya CCM kusitisha michakato ya kidemorasia kwa kisingizio cha kujenga uchumi ni jambo ambalo halikubaliki, na ACT Wazalendo tunasema wazi hili halikubaliki na tutalipinga kwa nguvu zote.
Sote tunakumbuka wakati wa mjadala wa Katiba Mpya namna Watanzania tulivyoshikamana kwa pamoja tukapaza sauti zetu kwa umoja wetu na kilio kilisikika dunia nzima. Sauti ilianza kupazwa na wananchi kwa umoja wao, zikafuata jumuiya za kiraia, viongozi wa dini, na wanasiasa wa vyama vyote, sote tukiwa na kauli moja kuhusu mustakbali wa nchi yetu. Hii ilitokana na mbegu ya umoja tuliyoijenga kupitia tawi ya demokrasia la “uhuru wa kutoa maoni”.
Demokrasia ni kichocheo na hamasa kubwa ya uwajibikaji wa pamoja, jambo linaloashiria mwelekeo mwema kwa nchi yoyote. Wananchi hupata matumaini ya kunyanyua hali zao za maisha, wawekezaji wa ndani na nje humiminika na jumuiya ya kimatifa nayo huungana na nchi yenye demokrasia ya kweli kwa kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo.
Laiti serikali ya CCM ingeliliona hilo, kasi ya maendeleo ingelikuwa kubwa na Tanzania ingelifika mbali kuliko ilivyo sasa. Ni bahati mbaya kuwa miongoni mwa viongozi wa CCM kuna ambao hawapendi kuona Watanzania tunaungana kupaza sauti kwa sababu umoja wa Watanzania unaathiri maslahi yao binafsi na maslahi ya wanaowatumikia.
Viongozi hawa wanadhani ukiwapa watu vitu umemaliza kiu yao. La hasha. Demokrasia ni Maendeleo na Maendeleo ni Uhuru wa kidemokrasia wa Watu. ACT Wazalendo ni muumini mkubwa wa Uhuru wa kidemokrasia wa watu (fundamental democratic freedoms).
Kwa muktadha huo hakuna mtu yeyote katika hali isiyo ya dharura mno, mwenye mamlaka ya kuzuia watu kukutana, watu kujiunga na vyama, watu kutoa maoni yao kwa uhuru, watu kupiga kura na sauti za walio wengi kuheshimiwa. Kwa bahati mbaya sana chini ya utawala wa CCM jambo hilo limeanza kutekelezwa na awamu ya tano na linaendelezwa na awamu ya sita bila kuzuiliwa na hivyo kuitumbukiza nchi "katika giza la demokrasia"
Pamoja na kuwa tunajali wenzetu ambao demokrasia zao zimekabwa na kunyongwa na nchi nyengine, lakini wajibu wetu ACT Wazalendo ni kupigania demokrasia isimame kwa miguu yake miwili humu ndani ya nchi yetu.
ACT Wazalendo tunaomba wadau wote wa demokrasia vikiwemo vyama vya siasa, vyombo vya habari, taasisi za haki za binaadamu, taasisi za kijamii tuungane kwa pamoja tuitoe demokrasia yetu GIZANI na KIZUIZINI na kusimamisha ndani ya mipaka ya Tanzania
Sauti zetu, nguvu zetu na ushirikiano wetu kustawisha Tanzania inayoheshimu na kulinda demokrasia ni muhimu mno katika kujenga Tanzania yenye uchumi imara kwa maana uchumi na demokrasia ni watoto pacha.
MUNGU IBARIKI TANZANIA
Salim A. Bimani
Katibu wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma
ACT Wazalendo
15 Septemba, 2021.
No comments:
Post a Comment