HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

October 30, 2021

Waziri Mkuu Awataka Mawaziri Kutotumia Wasaidizi Binafsi Katika Ofisi za Umma


Na Jasmine Shamwepu, Dodoma


 Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa amewataka manaibu na mawaziri wa wizara zote nchini kuacha matumizi ya wasaidizi binafsi kwa ajili ya kuwafanyia kazi katika ofisi za umma.

Akifungua mafunzo ya viongozi hao yaliyoandaliwa na Taasisi ya Uongozi leo jijini Dodoma, Mhe. Majaliwa amesema matumizi ya walinzi na wanahabari binafsi katika ofisi za umma kunasababisha kuvuja kwa siri za Serikali.

“Upo utaratibu wa kufuata endapo itabainika mnahitajika kupatiwa wasaidizi hao zingatieni utaratibu huo na si vinginevyo,” ametanabahisha Waziri Mkuu.

Sambamba na hayo, Mhe. Majaliwa amewataka viongozi hao wa umma kuwa kusimamia amani na utulivu, utawala bora, kuepuka uzembe na ubadhirifu, kusimamia nidhamu na uwajibikaji, pamoja na kutumia lugha ya staha.

Mengine aliyoyasisitiza ni kuunga mkono kampeni na maelekezo ya viongozi wakuu wa kitaifa sambamba na kuzingatia itifaki na mawasiliano.

“wakati wa ziara katika Mikoa hakikisheni Wakuu wa Mikoa husika wanapata taarifa kwa wakati na ni vema kutembelea Ofisi hizo pamoja na za Chama kwa ajili ya kupata maelezo muhimu,” amesisitiza Mhe. Majaliwa.

Kadhalika amewaagiza Mawaziri na Naibu Waziri wasimamie taasisi na idara zilizopo chini ya wizara zao ili zizingatie vigezo vyote vya utawala bora pamoja na kukomesha vitendo vya rushwa ambavyo ndio adui mkubwa wa utawala bora.

“Ninyi ni nyenzo muhimu katika utendaji wa Serikali, hivyo wazembe, wezi na wabadhirifu waliopo chini ya mamlaka zenu lazima wote wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za Serikali. Kila kiongozi lazima awe makini muda wote.”

Amesema lengo la mafunzo hayo ni kupanua uelewa wa Mawaziri na Naibu Mawaziri kuhusu masuala mbalimbali ya uongozi ikiwa ni pamoja na kuelewa majukumu, madaraka na mipaka ya nafasi zao, kuongoza watu, kufanya maamuzi ya kimkakati na kuboresha sifa binafsi za kiuongozi.

Naye Waziri, Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed O. Mchengerwa amesema kuwa wanaishukuru serikali kwa kuona umuhimu wa mafunzo hayo yenye lengo la kuwakumbusha viongozi hao katika majukumu.

Pia, Waziri Mchengerwa ameziagiza wizara, idara na taasisi zote za Serikali zihakikishe zinatenga bajeti kwa ajili ya kuwapeleka watumishi viongozi kushiriki katika mafunzo yanayoandaliwa  na kutolewa na Taasisi ya Uongozi.

No comments:

Post a Comment

Pages