HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

November 17, 2021

Madiwani Kasulu washuhudia uvamizi eneo la hifadhi ya wanyamapori

Madiwani wakitembelea eneo lenye uvamizi kwenye hifadhi ya Makere.

Baadhi ya watuhumiwa wa ujangili waliokamatwa katika eneo hilo.
Meneja wa Kitalu cha Uwindaji cha Makere na eneo la wazi Uvinza, Shadrack Kagoma akionesha watu walivyovamia eneo la hifadhi na kulima mpunga.

 

Mwandishi Wetu, Kasulu

BARAZA la Madiwani wa Halmashauri ya Kasulu, Mkoa wa Kigoma na viongozi wa halmashauri hiyo wametembelea eneo la hifadhi ya Makere na ardhi oevu ambalo wafugaji na wakulima limelivamia.

Eneo la ikolojia Moyowasi-Malagarasi ni muhimu Kwa maslahi ya Uhifadhi kwa kuwa kuna wanyama ambao hawapatikani sehemu nyingine ulimwenguni.

Katika eneo hili linalopakana na Ziwa Tanganyika pia kuna ndege aina ya Korongo Nyangumi ambao hawapatikani sehemu nyingine duniani na kuna makundi makubwa ya Zohe Statunga na Pofu.

Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Elia Kagoma akiwa na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Joseph Rwiza wakizungumza baada ya kutembelea eneo hilo jana wameeleza kusikitishwa na uvamizi unaoendelea.

Kagoma alitaka hatua za haraka kuchukuliwa na mamlaka husika kwa kuweka mipaka eneo hilo ili kuitenga hifadhi na eneo la vijiji katika kukabiliana na wavamizi wote.

"Lazima kuwepo alama maalum kuzunguka eneo hili ambalo ni kitalu cha uwindaji ili kuhakikisha uvamizi unakomeshwa,” alisema.

Kwa upande wake Rwiza alitaka kuwepo na ushirikiano wa kupambana na majangili katika eneo hilo ambalo ni muhimu kwa maslahi ya taifa.

Akizungumza na viongozi hao wa halmashauri, Meneja wa  Kitalu cha Uwindaji cha Makere na eneo la wazi Uvinza, Shadrack Kagoma amesema eneo hilo kwa sasa kuna ujangili kutokana na uvamizi wa watu.

"Tuna wageni wa kimataifa wa uwindaji katika eneo hili lakini shida wakifika wanakuta kitalu chetu kimevamiwa na mifugo, wakati mwingine wanalima kabisa,” amesema.

Amesema wavamizi wakiwepo kutoka nchi jirani wanaingia na mifugo eneo la hifadhi na kulima.

No comments:

Post a Comment

Pages