HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

November 06, 2021

Serikali yarudisha Mfumo wa TeRMIS, kuanza kazi Disemba Mosi

 


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) Mhe. Ummy Mwalimu (katikati) akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi ndogo za Wizara hiyo leo Jijini Dar es Salaam.

 

Hussein Ndubikile, Dar es Salaam 

 

Serikali kupitia Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imeridhia kurudisha Mfumo wa Ukusanyaji Ushuru wa Maegesho kwa njia ya Kielektroniki (TeRMIS) huku ikibainisha kuwa utaanza kutumika tena kuanzia Disemba Mosi, mwaka huu katika maeneo yote ambayo mfumo huo umefika.

Akizungumza na wanahabari leo Jijini Dar es Salaam, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Ummy Mwalimu amesema kuwa hadi sasa TARURA kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI tayari wamezifanyia kazi changamoto zilizojitokeza katika matumizi ya mfumo wa kielektroniki wa ukusanyaji ushuru wa maegesho ambapo ilikuwa changamoto kwa watumiaji.

“Ukusanyaji wa Ushuru wa Maegesho ya magari kwa kutumia mfumo wa TerMIS utapunguza mianya ya upotevu wa mapato ya Serikali na kuwezesha fedha hizo kuingia moja kwa moja Serikalini. 

Kutokana na umuhimu wake ninarejesja matumizi ya Mfumo huu kuanzia tarehe 1 Desemba 2021”. Amesema Waziri Ummy.

Amebainisha kuwa  miongoni mwa changamoto ambazo wamezifanyia kazi ni pamoja na wateja kutopatiwa taarifa za kudaiwa ushuru wa maegesho kwa wakati, kiwango kikubwa cha gharama za maegesho, Muda wa kulipa ambapo hapo awali mtumiaji wa maegesho alitakiwa kulipa ushuru ndani ya siku 7 tangu alipotumia maegesho na endapo atashindwa kulipa ndani ya muda huo alipaswa kulipa mara mbili ya ushuru aliokuwa anadaiwa. Na endapo atazidisha siku 14 pia alitakiwa Ushuru wa Maegesho pamoja na faini ya shilingi 30,000.

“Mtumiaji wa maegesho sasa atatakiwa kulipa ushuru ndani ya siku 14 badala ya siku 7 tangu alipotumia maegesho na endapo atashindwa kulipa ndani ya muda huo atatakiwa kulipa Ushuru wa Maegesho pamoja na faini ya shilingi 10,000 badala ya shilingi 30,000 zilizokuwa zikitozwa awali. Hivyo adhabu wa shilingi 30,000/- nimeifuta”. Amesema

“Kero kubwa ilikuwa gharama ya maegesho kuwa kubwa, kanuni zimeboreshwa, kwa mfano kwenye Jiji la Dar es Salaam watumiaji watatozwa  kiasi cha Shilingi 500/- kwa saa na kiasi cha Shilingi 2,500/- kwa siku, tofauti na zamani Shilingi 500 /- kwa saa na Shilingi 4,500/- kwa siku”, ameeleza Waziri Ummy.

 Ameitaka TARURA kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi hasa kwa Mikoa ilioanza kutumia mfumo huo ikiwemo Mkoa wa Dar es Salaam, Mwanza, Singida, Iringa na Dodoma ili kuwepo na uelewa wa kutosha kabla ya kuanza tena kwa matumizi ya mfumo huo.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Mhandisi Victor Seff amesema TARURA wanahusika zaidi kwenye maeneo ya hifadhi za barabara zilizo chini yao,hivyo nje ya hapo hawahusiki na usimamizi wa ukusanya wa ushuru.

“Mfano kwa hapa Dar, kwenye Kituo cha Mabasi Mbezi Luis, nje ya Hifadhi za Barabara TARURA haihusiki na ukusanyaji ushuru. Hata Mlimani City sisi hatuhusiki kabisa katika ukusanyaji ushuru”, amesema Mhandisi Seff.

Pia amesema kuhusu suala la kutotoa risiti watalifuatilia kwa ukaribu ili kuhakikisha risiti zinatolewa kwa watumiaji wa maegesho pale watakapolipa ada.



No comments:

Post a Comment

Pages