HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

November 09, 2021

Tanzania kupata joto kali

Meneja wa Kituo Kikuu cha Utabiri, Samwel Mbuya.


Na Mwandishi Wetu


MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa taarifa juu ya ongezeko la joto katika maeneo mengi hapa nchini.


Hayo yamesema Dar es Salaam leo Novemba 08,2021 na Meneja wa Kituo Kikuu cha Utabiri, Samwel Mbuya alipozungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.


Mbuya amesema ongezeko hili la joto linatokana na kusogea kwa jua la utosi sambamba na upungufu wa mvua katika maeneo mengi ya nchi yetu kama ilivyotabiriwa awali. 


Amefafanua kwamba hapa nchini, vipindi vya jua la utosi hufikia kilele mwishoni mwa Novemba wakati jua la utosi likielekea kusini (Tropiki ya Kaprikoni) na hali hiyo hujirudia tena Februari wakati jua la utosi likielekea kaskazini (Tropiki ya Kansa). 


“Jua la utosi huambatana na hali ya Joto kali kwa sababu uso wa dunia katika eneo tajwa huwa karibu zaidi na jua kuliko maeneo mengine. 


“Vilevile, hali ya joto kali hujitokeza zaidi kunapokuwa na upungufu wa mvua kama ilivyo katika kipindi hiki cha vuli na msimu mrefu,” amesema Meneja Mbuya.


Amesema kipindi hiki viwango vya joto vilivyoripotiwa katika maeneo mbalimbali ni vikubwa ambapo Mkoa wa Kilimanjaro uliripoti kiwango cha juu cha joto kilichofikia nyuzi joto 36.4 sawa na ongezeko la nyuzi joto 4.6 ukilinganisha na wastani wa muda mrefu kwa Novemba. 


“Kiwango cha juu cha joto kwa Mkoa wa Dar es Salaam, kimefikia nyuzi joto 33.8 sawa na ongezeko la nyuzi joto 2.2 wakati katika Mkoa wa Ruvuma limeripotiwa joto la nyuzi joto 34.4 sawa na ongezeko la nyuzi joto 4.3. 


“Hali kama hii imejitokeza pia katika mikoa yote nchini ambapo kiwango cha joto kimekuwa kikubwa kuliko wastani wa muda mrefu,” amebainisha Mbuya. 


Kwa mujibu wa meneja huyo wa TMA, vipindi vya joto kali vinatarajiwa kuendelea kujitokeza Novemba, 2021 na kupungua kidogo ifikapo Disemba, 2021 ambapo mtawanyiko wa mvua unatarajiwa kuongezeka sambamba na mionzi ya jua la utosi kuwa imeondoka katika maeneo ya nchi yetu. 


“Hivyo basi Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania inaendelea kutoa wito kwa wananchi kufuatilia taarifa za mwenendo wa hali ya hewa zinazotolewa na kutafuta, kupata na kutumia ushauri wa wataalamu wa kisekta ili kujiepusha na athari zinazoweza kusababishwa na hali mbaya ya hewa ikiwemo joto kali,” anasema Mbuya.

No comments:

Post a Comment

Pages