HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 28, 2022

Wajane wa Mrisho kuweka kambi kwenye kiwanja

 Na Selemani Msuya

 

WAJANE wa Marehemu Mzee Amir Mrisho, Aseline na Amina Mrisho wamesema ili haki yao ya kumiliki kiwanja namba 108 Port Access isipotee wataweka kambi katika kiwanja hicho kuanzia leo.

Uamuzi wa wajane hao kuweka kambi katika kiwanja hicho walichoachiwa na mume wao, umekuja baada ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mwanzo Kariakoo, wilayani Ilala mkoani Dar es Salaam, Julieth Dama kutupilia mbali ombi lao ambalo waliomba mahakama hiyo iweke zuio la umilikishwaji wa kiwanja namba 108 kwa mmiliki mpya Kampuni ya Nahla.

Wakizungumza na waandishi wa habari baada ya hukumu hiyo wajane hao Aseline na Amina walisema sakata hilo la eneo lao kuuzwa kinyemela limechukua muda mrefu, hivyo wameamua kupambana kwa kila njia ili haki ipatikane.

“Sisi kuanzia sasa tunahamishia vitanda vyetu pale kwenye kiwanja chetu, hatuko tayari kukubali kunyang’anywa kiwanja chetu, ambacho tumeachiwa na mume wetu na watoto wetu 21,” alisema.

Wajane hao walisisitiza kumomboa Rais Samia, Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Anjelina Mabula kuwasaidia kwa kuwa wanaona mahakama zimeshindwa.

“Kinachoonekana kuna mchezo mchafu unafanyika kwenye mahakama zetu, tunaamini Rais Samia na wasaidizi wake wanaweza kutusaidia sisi wajane. Mbaya zaidi hili suala wakati wa uongozi wa Rais John Magufuli lilikuwa kimya baada ya kufa tu limeibuka kwa kasi ya ajabu kuna kitu, sisi hatutakubali, afadhali tufie kwenye kiwanja chetu,” alisema.

Walisema kinachoonekana ni dhahiri kuwa kuna mipango nyuma ya pazia hivyo wanaamini iwapo kutakuwa na uchunguzi wa vyombo vingine ukweli utajulikana.

Wajane hao walisema eneo hilo maarufu kwa Vetenari Mapambano limeajiri vijana zaidi ya miatano ambao wanalipa kodi Serikalini hivyo kuwaondoa kihuni ni jambo ambalo halikubaliki.

Pamoja na wajane hao wanufaika wengine ni watoto wa marehemu Mzee Mrisho ambao ni Omari, Naima, Mariam, Rachel,Rehema, Mrisho, Juma, Zahara, Zainabu, Sharifa, Saidi, Karim, Rajab, Abdul, Hadija, Sauda, Hussein, Ibrahim, Iddi, Riziki  na Sofia.

No comments:

Post a Comment

Pages