HABARI MSETO (HEADER)


 


Breaking

January 18, 2022

ZINGATIENI MTAKAYOFUNDISWA NA KUITUNZA MIUNDOMBINU YA SHULE - DED MULEBA

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba Ndg. Elias Kayandabila amefanya ziara katika shule za Sekondari ya Kaigara, Anna Tibaijuka,  Kasharunga na Shule ya Sekondari ya Kasharunga Mpya (Kiteme) kukagua mwitikio wa wanafunzi wa kidato cha kwanza kuripoti shuleni huku akiwasihi wanafunzi hao kuzingatia watayofundishwa na walimu wao.

Akizungumza na wanafunzi hao alipozitembelea shule hizo Ndg. Kayandabila amewasihi wanafunzi hao kutunza miundombinu ya madarasa huku akiwaeleza kuwa wamepata nafasi ya kusomea katika mazingira yaliyo bora hivyo anatarajia watafanya vizuri na hatimaye kuwa na ufaulu mziri.

"Nafurahi kusikia mnafahamu madarasa yamejengwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Fadhila pekee ambayo tunaweza kumlipa mama ni kufanya vizuri kwenye masomo yenu kwahiyo niwaombe sasa muweke nguvu kwenye masomo", amesema na kuwasisitiza wanafunzi Ndg. Kayandabila.

Aidha, akiwa shule mpya ya Kasharunga amewasihi wazazi na jamii kuisaidia Serikali kuwabaini watoto ambao wamefaulu lakini watoto au wazazi wao wamelazimisha kwenda  kuolewa ili Serikali iweze kuchukua hatua dhidi yao na kuwarudisha shule watoto hao kwani malengo ya Serikali ni watoto wote waliofaulu waendelee na masomo.

Naye Kaimu Afisa Elimu Sekondari wa wilaya ya Muleba. Ndg. Masatu Chisumo amewasihi wanafunzi kutunza vyumba vya madarasa na kuwataka walimu kuanza ratiba za vipindi.

Mkuu wa Shule ya Anna Tibaijuka mwalimu Paulo Mligo ametoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutoa fedha za ujenzi wa vyumba vya madarasa mapya vya kisasa ambavyo vimesaidia kupunguza  uhaba na kuahidi kwamba watavitunza vyumba hivyo vya madarasa ili viweze kuwasaidia na wanafunzi wengine kwa miaka ijayo.

Naye mwanafunzi wa kidato cha kwanza shule ya Sekondari Anna Tibaijuka kwa niaba ya wanafunzi wenzake ametoa shukrani na pongezi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa ujenzi wa vyumba vya madarasa vya kisasa na kuahidi kuwa atasoma kwa bidii ili kuweza kufikia ndoto zake.

Mmoja wa wazazi Ndg. Gosbert Gervas wa kijiji cha Kiteme, Kata ya Kasharunga alipofika shuleni kuleta mtoto ameonesha furaha yake na kumshukuru sana Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuona uhitaji na umuhimu wa kupunguza adha ya michango ya vyumba vya madarasa hususani kipindi cha mwisho wa mwaka na kuamua kuleta fedha katika kila wilaya ili vyumba vya madarasa vijengwe.

Ameeleza kuwa watoto wa kijiji cha Kiteme, Kata ya Kasharunga walikuwa wakitembea umbali mrefu kutoka kijiji hapo kwenda shule ya sekondari Kasharunga. Hali ambayo ilipelekea wazazi kuwapangia vyumba vya kuishi karibu na shule matokeo yake baadhi ya watoto walibeba mimba na hata kuharibikiwa kwa kukosa uangalizi wa karibu wa wazazi. Sasa wamejengewa shule mpya ya Kasharunga (Kiteme) ambayo itawapunguzia watoto kutembea umbali mrefu na hata kuwa na uangalizi wa karibu wa wazazi.

Wazazi wa wanafunzi waliofika shuleni kuleta watoto wameeleza kuwa kupitia fedha iliyotolewa kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa ambavyo pia vimewekewa viti na meza hali hii imewaondolea adha ya kuchangia michango mbalimbali shuleni na kuwaondolea watoto usumbufu wa kwenda na viti na meza.

Shule ya Sekondari Anna Tibaijuka leo tarehe 17/1/2022 imepokea jumla ya wanafunzi 51 ambapo idadi ya wanafunzi wanaotakiwa kuripoti shuleni ni wanafunzi 243 na shule ya Sekondari Kasharunga wameripoti wanafunzi 75 idadi ya wanafunzi wanaotakiwa kuripoti shuleni ni wanafunzi 269.

No comments:

Post a Comment

Pages