HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 24, 2022

Serikali yasisitiza sekta ya madini kipaumbele ukuzaji uchumi


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akihutubia wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa nne wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini uliofanyika katika Ukumbi wa Mwalimu Nyerere.


Na Hussein Ndubikile, Dar es Salaam.

Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan imesema kuwa,Sekta ya Madini ni miongoni za sekta muhimu na ya kipaumbele katika kukuza uchumi wa nchi.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango ameyeyasema hayo jijini Dar es Salaam  wakati akifungua Mkutano wa Nne wa Kimataifa wa Uwekezaji Katika Sekta ya Madini unaofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini humo.

Dkt.Mpango ambaye alikuwa mgeni rasmi alimwakilisha Rais wa Samia katika mkutano huo muhimu ambao unawakutanisha kwa pamoja wadau mbalimbali wa sekta hiyo kutoka ndani na nje ya nchi.

Makamu wa Rais awali ametumia nafasi hiyo kuwapongeza waandaaji wa mkutano huo wakiongoza na Waziri wa Madini, Dkt.Doto Biteko kwa maandalizi ambayo yameonesha ufanisi mkubwa.

"Mheshimiwa Rais alitamani kujumuika nanyi katika mkutano huu muhimu ambao kutokana na majukumu mengine ya Kitaifa aliyonayo, amenituma nimuwakilishe. Amenituma niwaeleze kuwa, niwaeleze kuwa, Sekta ya Madini ni miongoni za sekta muhimu na ya kipaumbele katika Serikali yake ya Awamu ya Sita, hivyo Mheshimiwa Rais anafuatilia kwa karibu zaidi mijadala, mapendekezo na maazimio yanayohusu sekta hii,"amefafanua Makamu wa Rais Dkt.Mpango.

Pia Mheshimiwa Rais Samia kupitia taarifa aliyoiwasilisha Makamu wa Rais Dkt. Mpango amesema kuwa, Serikali ipo tayari kushirikiana kwa karibu na wawekezaji wa sekta ya madini kutoka ndani na nje ya nchi katika sekta ya madini.

"Mkutano huu ni muhimu, kwani unatupatia fursa ya kupokea maoni na michango yenu kutokana na uzoefu mlionayo katika Sekta ya Madini na hivyo kutuwezesha sisi kama Serikali kuboresha mazingira ya kufanya biashara na kuchochea uwekezaji,"amesema Dkt.Mpango.

Amesema, pia mkutano huo unatoa nafasi ya kipekee ya kuujulisha ulimwengu kuhusu fursa mbalimbali za uwekezaji za madini zilizopo katika sekta ya madini hapa nchini.

"Hivyo kauli mbiu ya mwaka huu inayosema, Mazingira Wezeshi kwenye Uwekezaji katika Sekta ya Madini. Ninaamini inahakisi vema nia ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuvutia wawekezaji nchini.

"Serikali inafahamu kuwa, ili tuweze kufanikiwa katika sekta hii, tunahitaji mazingira wezeshi na ushirikiano wa makundi mbalimbali ya wadau wanaojihusisha na uchimbaji na biashara ya madini hapa nchini, kwa sababu hiyo, mkutano huu umewaleta kwa pamoja wadau mbalimbali wa sekta ya madini na wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.

"Ninaamini mchanganyiko huu wa wadau utachochea mjadala wenye afya ambao utatoa mapendekezo ya kuboresha mazingira ya uwekezaji katika sekta hii bila kuathiri maslahi ya nchi yetu.

"Ni azma ya Serikali kuona kuwa nchi yetu inanufaika na madini yake na wawekezaji nao wanapata manufaa kwa kuwekeza mitaji yao, na ujuzi hapa nchini, hivyo mwaka 2017 Serikali iliamua kufanya maboresho ya Sheria yetu ya Madini ili kuongeza mchango wa sekta hii katika pato la Taifa na sekta nyingine.

"Maeneo yaliyozingatiwa katika maboresho ni pamoja na kuimarisha ushiriki wa nchi, na wananchi katika mnyororo wa uchumi wa madini, na kuhakikisha kwamba uongezaji wa thamani ya madini unafanyika zaidi hapa nchini, maboresho hayo yote yameleta mapinduzi makubwa katika sekta ya madini. Kwa kuzingaia haya, mpango wetu wa maendeleo wa miaka mitano umeongezea lengo la mchango wa sekta ya madini katika pato la Taifa hadi kufikia asilimia 10 ifikapo mwaka 2025/26 ikilinganishwa na kiwango cha asilimia 6.7 mwaka 2020/21.

"Kwa upande wa thamani ya mauzo nje ya nchi kutokana na madini, lengo ni kuyaongeza kutoka dola za Marekani Bilioni 3.4 mwaka 2020 hadi dola za Marekani bilioni 5.5 ifikapo mwaka 2025/26.

"Hatuna budi kuhakikisha tunashirikiana ili kuhakikisha kwamba, malengo haya yanafikiwa ili sekta hii iweze kuchangia zaidi jitihada za Taifa katika kupunguza umaskini nchini,"amefafanua kwa kina Makamu wa Rais.

FEMATA

Kwa upande wake, Rais wa Shirikisho la Vyama Vya Wachimba Madini Tanzania (FEMATA), John Bina amesema kuwa, kuna maboresho makubwa ambayo yamefanywa na Serikali katika Sekta ya Madini ingawa wanaamini baadhi ya changamoto zilizipo kwa sasa zikipatiwa ufumbuzi uzalishaji utaongezeka zaidi.

"Mheshimiwa Makamu wa Rais, kwetu changamoto ya umeme imekuwa kikwazo katika migodi mbalimbali, hivyo, tanaiomba Serikali kuingilia kati kwa kulipatia ufumbuzi tatizo, ili uzalishaji uendelee kwa ufanisi,"amesema Bw.Bina.

"Umeme umekuwa ni tatizo na hata umeme ukirudi unakuwa hautoshelezi, trasfoma zinakuwa chini. Pia tunaiomba Serikali na wadau wengine kukaa kwa pamoja ili kujadili namna ya kunusuru soko la Tanzanite...linaweza kudondoka kutokana na urasimu tu," Alisema. 

No comments:

Post a Comment

Pages