HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

March 06, 2022

Mpwapwa kutoa elimu kilimo bora cha mtama


Mkulima wa zao la mtama Ernest Sebastian kutoka kijiji cha Mtamba wilayani Mpwapwa akizungumza na waandishi wa habari namna kilimo hicho kilivyomnufaisha, pembeni ni mke wake Frida wakiwa kwenye shamba lao.

Mkulima wa zao la mtama kupitia Mradi wa Kilimo Himilivu cha Mtama (CSA), Ernest Sebastian kutoka kijiji cha Mtamba wilayani Mpwapwa akipalilia mtama katika shamba lake.

Ofisa Mawasiliano wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) Desta Laizer akizungumza na Ofisa mwenzake William Laswai.

Ofisa Mradi wa Kilimo Himilivu cha Mtama (CSA), kutoka Shirika la Farm Afrika, Adeline Ayoub akimuelezea Ofisa Ufuatiliaji Msaidizi kutoka Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), William Laswai namna ambavyo mradi unatekelezwa.

Ofisa Program Mwandamizi kutoka Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), Steyne Roggers akionesha mti malisho ambao unasaidia kurutubisha ardhi na malisho ya mifugo.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma, Mwanahamis Ally akizungumza na waandishi wa habari waliomtembelea ofisini kwake hivi karibuni kujua namna Mradi wa Kilimo Himilivu cha Mtama (CSA) unavyotekelezwa.

 

Na Mwandishi Wetu, Dodoma
 

KATIKA kuunga mkono Mradi wa Kilimo Himilivu cha Mtama (CSA), unaotekelezwa na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani(WFP) na Shirika la Farm Afrika, Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa imesema itatumia maofisa kilimo wake kutoa mafunzo kwa wakulima kuhusu umuhimu wa kulima kitalaam

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa Mwanahamis Ally wakati akizungumza na waandishi wa habari ambao walitembelea wilaya hiyo kuona namna mradi huo unavyotekelezwa.

Ally amesema katika kipindi cha miaka mitatu ya mradi wa CSA halmashauri imeweza kuongeza mapato kupitia kodi ya mazao ikiwemo zao la mtama, hivyo hawana budi kuwekeza katika kilimo hicho hasa kwa kutumia maofisa ugani kutoa elimu.

Amesema wananchi wamekuwa na mwitikio mkubwa kwenye kilimo hicho, hivyo jukumu lao kama viongozi ni kuhamasisha wakulima wengine kujiunga na kutekeleza mradi huo.

“Tunafarijika kuwa na WFP pamoja na Farm Afrika katika halmashauri kilimo cha mtama kimekuwa maarufu sana hapa kwetu lakini kimeleta tija kwa wananchi kwani kimeboresha kipato, kimesaidia kuongeza pato la halmashauri, ukienda kwenye jamii sasa hivi wanazungumzia mashirika hayo kwa namna gani wamenyanyua vipato kupitia zao la mtama.

Wote tunamkomboa mwananchi wa Mpwapwa, wote tunachangia kwenye pato la halmashauri ya Mpwapwa. Niseme tu hili zao la mtama limekuwa mkombozi mkubwa katika jamii yetu na wananchi wamekuwa mashuhuda wa manufaa ambayo yanapatikana kupitia kilimo cha mtama,” amesema.

Mkurugenzi huyo amesema halmashauri kupitia idara ya kilimo wanaendelea kuwapa uatalaamu wakulima kuhusu kilimo na uhifadhi mazao pamoja na kuwatafutia masoko.

Aidha, amesema ili kuongeza hamasa na tija kwa wakulima wa zao la mtama wanatarajia  kuandaa taarifa ambayo itaonesha kiasi cha fedha kinachotokana na zao hilo kwa kila msimu.

 

Naye Ofisa Kilimo wa Wilaya ya Mpwapwa Edson Kileo amesema mradi wa CSA unaotekelezwa katika vijiji 51 na kata 22 umeweza kunufaisha wakulima 5,558 kuanzia mwaka 2018.

Kileo amesema katika msimu uliopita wakulima wa Mpwapwa waliuza zaidi ya yani 13 kwa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) na Mfanyabiashara Ally Juma.

Ofisa Mradi wa CSA wilayani hapo kutoka Farm Afrika Adelina Ayubu amesema kilimo hicho kimewakomba wakulima wengi hali ambayo inachangia uhitaji kuongezeka.

Ayoub amesema pamoja na kuongeza uzalishaji mradi huo umesaidia wakulima kupata lishe bora lishe kwa kulima bustani za mbogamboga nyumbani pamoja na kutoa elimu ya utunzaji mazingira kwa kutumia miti malisho.

“Kingine ambacho tunakifanya kupitia mradi huu ni tunawaunganisha wakulima na masoko, benki pamoja wadau wengine wa kilimo,” amesema.

 

No comments:

Post a Comment

Pages