HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

March 06, 2022

Wakulima wa mtama wafundwa uzalishaji mbegu bora

 

Ofisa Ugani wa Kata ya Idifu, wilayani Chamwino, mkoa wa Dodoma Fredrick Mwalongo akijadiliana jambo na Mkulima wa mbegu bora za mtama, Joyce Ng’ambi baada ya waandishi wa habari kutembelea shamba hilo.

 

Shamba la Mkulima Joyce Ng’ambi ambalo ni maalum kwa mbegu bora ya mtama.

 

Ofisa Mradi wa Kilimo Himilivu cha Mtama (CSA), kutoka Shirika la Farm Afrika, Timoth Gwandu akielezea umuhimu wa wakulima wa zao la mtama kuwa na mashamba darasa kwa ajili ya kuzalisha mbegu bora, pembeni ni Mkulima Joyce Ng’ambi.

   

Mkulima Joyce Ng’ambi akielezea waandishi wa habari ambao wametembelea shamba lake la kuzalisha mbegu za mtama, kwanini aliamua kuanzisha shamba hilo.

  Na Selemani Msuya, Dodoma

WAKULIMA zaidi ya 22,000 wa zao la mtama, kupitia Mradi wa Kilimo Himilivu cha Mtama (CSA), wamepatiwa mafunzo ya kilimo cha kisasa na kuzalisha mbegu bora za zao hilo.

Mradi huo utatekelezwa katika wilaya za Bahi, Chemba, Mpwapwa, Kongwa, Chamwino na Kondoa na kuwezesha wakulima kuongeza kipato, mavuno na lishe bora.

Hayo yamebainishwa na Ofisa Mradi kutoka Shirika la Farm Afrika Timoth Gwandu, wakati akionesha waandishi wa habari shamba darasa linalomilikiwa na Mkulima Joyce Ng’ambi wa kijiji cha Miganga kata ya Idifu, wilayani Chamwino.

Gwandu, alisema moja ya changamoto ambayo wamekutana nayo katika kutekeleza kilimo hicho ni mbegu bora, hivyo Farm Afrika na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), wameweza kutoa mafunzo ya kilimo bora na uzalishaji wa mbegu kwa wakulima.

Alisema kiwango cha mbegu ya mtama kinachozalishwa na wazalishaji mbalimbali hakikidhi mahitaji ya wakulima na soko, hivyo ili kuziba pengo hilo wamekuwa wakihamasisha wakulima kuanzisha mashamba darasa.

Gwandu alisema katika kijiji cha Miganga mkulima Ng’ambi amejitolea kutekeleza kilimo kwa kulima mwenyewe na kuzalisha mbegu bora ambazo anauzia wakulima wenzake.

“Mradi huu ambao unafadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Ireland (IrishAid), kusimamiwa na WFP na kutekelezwa na sisi Farm Afrika tumelazimika kutoa elimu ya shamba darasa na hapa Miganga tunaye Nga’mbi ambaye anaziba pengo ambalo lilo,” alisema.

Ofisa huyo alisema kupitia shamba darasa hilo wameweza kusaidia wakulima wengi kupata mbegu bora na kuongeza uzalishaji.

Naye mzalishaji mbegu Ng’ambi alisema amefikia uamuzi huo baada ya kuona kuwani fursa iliyopo katika eneo hilo hasa kwa wakulima wenzake wa kijijini.

Ng’ambi alisema amekuwa akiwauzia wakulima wenzake mbegu ya mtama kwa shilingi 3,000 bei ambayo wakulima wengi wanaweza kununua.

Mwanamama huyo ambaye ni mjane alisema kupitia kilimo cha mtama ameweza kusomesha watoto wake, kujenga nyumba na kuhudumia familia.

“Mimi ni mkulima mjane, ambaye nimepata cheti cha kuzalisha mbegu kutoka kwa Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA), nawauzia wakulima wenzangu na matokeo yake yamekuwa makubwa tangu mradi huu wa kilimo himilivu kuanza,” alisema.

Ng’ambi alisema uhitaji wa mbegu ni mkubwa katika kijiji chao na vijiji vingine, hivyo kuwataka wakulima wenzake kuanzisha mashamba darasa.

Alisema WFP na Farm Afrika wamefanya mapinduzi ya kiuchumi, kijamii na maendeleo katika maisha yake na wananchi wengine ambao wanajihusisha na kilimo.

Kwa upande wake Ofisa Ugani wa kata ya Idifu, alisema mradi wa CSA umekuwa msaada kwake katika kutoa elimu kuhusu kilimo bora na chenye tija.

Alisema anachofanya Ng’ambi kimesaidia wakulima wengi ambao wanajihusisha na uzalishaji wa zao hilo ambalo limeongezewa thamani kwa sasa.

No comments:

Post a Comment

Pages