Muonekano wa Kivuko cha MV. Kazi ambacho ukarabati wake unaendelea jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa akisisitiza jambo kwa Meneja wa Ujenzi wa Vivuko wa Wakala wa Ufundi na Umeme nchini (TEMESA), Eng. Lukombe Kingo'mbe alipokagua ukarabati wa Kivuko cha MV. Kazi jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa akijadiliana jambo na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Songoro Marine Bw Meja Songoro alipokagua ukarabati wa Kivuko cha MV. Kazi jijini Dar es Salaam (kushoto) ni Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni Bi, Fatma Almas Nyangasa na Bw. Ramsey Kanyanga (kulia) kutoka Wizara ya Ujenzi wakifuatilia.
Na Selemani Msuya
WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa ameiagiza Kampuni ya Songoro Marine Transport inayotengeneza Kivuko cha MV. Kazi kuhakikisha inakamilisha kazi hiyo chini ya miezi minne.
Aidha, Mbarawa ameitaka Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), kuwasilisha mpango wao wa matengenezo ya vivuko ili kuepusha matengenezo makubwa ambayo yanagharimu fedha nyingi.
Waziri Mbarawa ametoa maagizo hayo jana wakati alipofanya ziarakwenye kitui cha matengenezo cha kampuni hiyo kilichopo wilayani Kigambano jijini Dar es Salaam.
Amesema muda wa miezi minne ya matengenezo makubwa ya kivuko hicho ni mwingi hasa ikizingatiwa kuwa wananchi wa Kigamboni wanahitaji huduma ya chombo hicho.
“Wizara ipo tayari kutoa fedha, naomba mchakato wa kuanza kusaini ufanyike ifikapo Ijumaa ya wiki hii, ili manunuzi ya vifaa husika yafanyike na ikiwezekana matengenezo hayo yakamilike ndani ya miezi mitatu na sio minne kama ambavyo mnasema,” alisema.
Waziri Mbarawa amesema Kigamboni ni eneo ambao lina mchango mkubwa kwenye kukuza uchumi, hivyo huduma zinapokuwa duni Serikali inapata hasara.
Mbarawa amewataka wakandarasi hao kuhakikisha wanatumia mitambo ambayo inaendana na ulimwengu wa sasa ili kurahisisha matengenezo kwa haraka.
Aidha, Prof. Mbarawa amesema ili kuhakikisha matengenezo ya vivuko hayachukui muda mrefu TEMESA wanawajibu wa kutoa taarifa mapema ili fedha zitolewe kwa haraka.
“Napenda kuchukua nafasi hii kuwataka TEMESA kuandaa mpango kazi ambao utaonesha ni lini vivuko vinafanyiwa matengenmezo kwa nchi nzima,” amesema.
Katika hatua nyingine Waziri Mbarawa amesema Serikali inatarajia kutenga fedha kupitia Bajeti ya 2022/2023 kwa ajili ya ujenzi wa kivuko kipya ambacho kitaweza kubeba abiria 3,000 na magari 80 kwa wakati mmoja.
Amesema matarajio ya Serikali ni vivuko vyote kufanya kazi kwa pamoja na kuweza kuvusha watu 7,000 kwa wakati mmoja, hivyo kumaliza adha ya kuvuka katika eneo hilo.
Akizungumza katika ziara hiyo, Meneja wa Ujenzi na Matengenezo TEMSA, Mhandisi Lukombe King’ombe amesema matengenezo ya Kivuko cha MV Kazi yatagharimu Sh.bilioni 4.5.
“Kivuko hiki kinafanyiwa matenmgenezo makubwa ambayo yatagharimu zaidi ya Sh.bilioni 4.5 baada ya kutumika miaka mitano, hivyo injini itabadilishwa na mitambo mingine,” amesema.
Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni Fatma Nyangasa, amesema mateso ambayo wanapitia wakazi wa Kigamboni ni makubwa hivyo kumtaka mkandarasi kuharakisha ukarabati wa kivuko hicho.
Nyangasa aliiomba Serikali kuondoa tozo kwa magari ya abiria yanayotumia Daraja la Nyerere ili kuwezesha wananchi wengi kupita njia hiyo.
Diwani wa kata ya Kigamboni Dotto Msawa amesema matengenezo ya kivuko hicho yataweza kuwapunguzia adha wananchi wa wilaya hiyo ambao kwa sasa wanakaribia milioni 1.5.
Amesema kwa siku zaidi ya watu laki mbili wanavuka kutumia vivuko hivyo hali ambayo inaongeza msongamano mkubwa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Songoro, Major Songoro amesema wao wamejipanga kumaliza ukarabati huo kwa wakati pindi fedha zikiingia.
Amesema changamoto ambayo inaweza kutokea ni kuwasili kwa vifaa hasa vinavyotoka nje, ila wanaahidi kukamilisha kazi kwa wakati ulipangwa.
“Kazi kubwa ni kubadilisha mabati, injini, jenereta na kupiga rangi kivuko chote, naamini tutamaliza ndani ya muda,” alisema.
No comments:
Post a Comment