HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

March 02, 2022

Zao la mtama lilivyobadilisha maisha ya wakulima Dodoma

 

 

Mkuu wa Ofisi ya Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), Neema Sitta akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za shirika hilo mkoani Dodoma kuhusu Mradi wa Kilimo Himilivu cha Mtama (CSA), unaotekelezwa katika wilaya sita mkoani hapa.

 

 

Mkulima Patrick Mbeho, akielezea namna mashine ya kupembulia mtama inavyofanya kazi, kulia kwake ni mke wake, Happy Philemon akionesha mtama uliotayari kwa kuuzwa.

 

 Meneja Mradi wa Kilimo Himilivu cha Mtama (CSA) kutoka  Shirika la FarmAfrika, Grace Changanyika akielezea namna wanavyotekeleza mradi huo.


Na Selemani Msuya, Dodoma

 

WAKULIMA 22,000  waliopo kwenye Mradi wa Kilimo Himilivu cha Mtama (CSA), kutoka wilaya sita za mkoa wa Dodoma, wamefanikiwa kuingiza Sh.bilioni 13.5 kwa msimu wa mwaka 2020 hadi 2021.

Aidha, Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) kwa kushirikiana na FarmAfrika wamewahakikishia wakulima wa mtama masoko ndani na nje ya nchi.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Ofisi Ndogo ya WFP, Neema Sitta wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye ofisi zao zilizopo jijini Dodoma.

Alisema mradi huo wa CSA unatekelezwa katika vijiji zaidi ya 200 vilivyopo kwenye wilaya sita za Bahi, Chamwino, Mpwapwa, Kongwa, Chemba na Kondoa ambapo kwa msimu wa mwaka 2020 hadi 2021 wamefanikiwa kuuza zaidi ya tani 28,000 za mtama, zenye thamani ya Sh. bilioni 13.5.

Sitta alisema mradi huo unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo ya Ireland (IrishAid) na kusimamiwa na WFP unatekelezwa na FarmAfrika kwa Sh.bilioni 1.7.

“Mradi wa CSA ambao umefikia wakulima 22,000 na kunufaisha zaidi ya watu 100,000 umeweza kuwaingizia wakulima zaidi ya Sh.bilioni 13.5 baada ya kuzalisha zaidi ya tani 28,000. Matarajio yetu ni kuona wakulima wa mtama wanaongeza uzalishaji kwa msimu mpya, ili kujipatia kipato cha uhakika,” alisema.

Mkuu huyo wa ofisi ndogo alisema sababu ya wao kujikita katika kilimo cha mtama ni kutokana na zao hilo kukubali ardhi na mazingira ya Dodoma, pamoja na uhakika wa soko.

“Zao la mtama lina vitamin nyingi ambazo zinafaida kwa mwili wa binadamu, hivyo mkakati wetu wa siku zijazo ni kuongeza uzalishaji,” alisema.

Alisema soko la zao la mtama mweupe lipo nchini Sudani Kusini ambao ni wateja wakubwa, Kiwanda cha Bia Tanzania (TBL) na kampuni nyingine za ndani.

Sitta alisema ufanisi wa mradi huo ambao unatekelezwa na FarmAfrika umetokana na mafunzo ambayo wakulima wamepatiwa pamoja na kuwaunganisha na masoko ya ndani na nje.

Alisema wakati mradi huo unaanza walikuta wakulima wanavuna gunia tatu kwa hekari ila kwa sasa wanavuna gunia 10 kwa hekari moja hiyo hiyo.

Alisema WFP na FarmAfrika wameweza kuunganisha wakulima na soko moja kwa moja na kuondoa madalali waliokuwa wanachangia kushusha bei ya zao.

Alifafanu kwa sasa bei ya zao la mtama kilo moja inaunzwa hadi Sh 550 kutoka Sh 250 ya awali hivyo kuongeza kipato kwa wakulima na kuhamasisha kilimo hicho.

Sitta alisema kilimo cha mtama ambacho kinalimwa mkoa wa Dodoma kinazingatia mfumo wa kilimo hai jambo ambalo linachangia kuwepo na uhakika wa soko kote duniani.

Alisema ushiriki wao kwenye kilimo ni kuhakikisha mkulima ananufaika na kilimo lakini ardhi inakuwa endelevu kwa vizazi vijavyo.

Kwa upande wake Meneja Mradi wa CSA, kutoka FarmAfrika Tanzania, Grace Changanyika alisema mradi huo umekuwa na mafanikio makubwa kwa wakulima jambo ambalo linawarahisishia kufikisha ujumbe wao kama watekelezaji wa mradi.

Changanyika alisema mafanikio waliyoyapata wakulima 22,000 kupata zaidi ya Sh.bilioni 13.5 yamevutia wakulima wengi kutaka kuingia kwenye mradi.

“Kilimo hiki kimebadilisha maisha ya wakulima kiuchumi, kijamii na maendeleo, ukilinganisha na kipindi cha nyuma kabla ya mradi,” alisema.

Naye Mkulima Patrick Mbeho wa kijiji cha Mkola wilayani Bahi, alisema mradi huo umefanya mapinduzi makubwa kwenye maisha yake kwa kipindi cha muda mfupi.

Mbeho ambaye ana zaidi ya hekari 20 za mtama, alisema ameweza kupata mavuno mara tatu ya yale ambayo akiyapata katika miaka ya nyuma kwenye eneo lenye ukuba uleule, pia uhakika wa soko.

“Kwangu haya ni mapinduzi ya kiuchumi, kijamii na maendeleo kwani nilikuwa napata Sh. milioni mbili kwa shamba la hekari 20 ila kwa sasa  napata hadi Sh. milioni sita, nimefanikiwa kujenga nyumba ya biashara, mashine ya kupembulia mtama na mengine mengi,” alisema.

No comments:

Post a Comment

Pages