*Utoaji huduma,
ukusanyaji wa michango, matumizi ya TEHAMA, ukwasi wa Mfuko yapewa kipaumbele
*Yajayo ni neema
tupu NSSF kuvutia wanachama wapya kutoka makundi mbalimbali ya sekta isiyo
rasmi
Na MWANDISHI
WETU
Mwenyekiti wa
Bodi ya Wadhamini ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Balozi Ali Idi
Siwa, amesema Mfuko utaendelea kusimamia maono ya Serikali ya Awamu ya Sita ya
kuhakikisha Watanzania waliopo kwenye sekta binafsi na sekta isiyo rasmi
wanasajiliwa na NSSF pamoja na waajiri kuwasilisha michango stahiki ya
wafanyakazi wao.
Balozi Siwa
alisema hayo jana jijini Mwanza wakati wa ufunguzi wa mkutano wa 49 wa Baraza
Kuu la Wafanyakazi wa NSSF, ambapo aliwataka watumishi wa Mfuko kuendelea kutoa
huduma bora, kujielekeza katika matumizi ya TEHAMA, kushirikiana sehemu za kazi
na kuifika sekta isiyo rasmi kwani imebeba sehemu kubwa ya Watanzania ambapo
kupitia kundi hilo Mfuko utapata wanachama wengi wapya.
Alisema mpango
wa mwaka na bajeti pendekezwa ya Mfuko kwa mwaka wa fedha 2022/23, Mfuko
umeweka malengo mbalimbali ikiwemo kusajili wanachama wapya 313,478, kukusanya
michango ya shilingi trilioni 1.61 pamoja na kukusanya shilingi bilioni 383.5
ambazo ni mapato yatokanayo na uwekezaji.
Aliwataka
wajumbe wa baraza hilo wakawe kioo kwa wenzao ili Mfuko uweze kuwa na matokeo
chanya kwa wanachama na Mfuko kwa ujumla.
Naye, Ibrahim
Maftah ambaye ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, alisema Mfuko umefanya vizuri
katika kutekeleza majukumu yake ambayo ni kuandikisha wanachama, ukusanyaji wa
michango, kuwekeza na kulipa mafao.
Alisema Mfuko
umefanya mapitio ya Mpango wa Uchangiaji wa Hiari ili kuvutia wanachama wapya
kutoka katika makundi mbalimbali ya sekta isiyo rasmi ikijumuisha wakulima,
wavuvi, wamachinga, mama lishe, waendesha boda boda na bajaji.
"Lengo la
mapitio hayo ni kuongeza wigo wa wanachama na kuwa na mafao yanayokidhi
mahitaji ya makundi hayo," alisema Maftah.
Maftah alisema
katika mwaka wa fedha wa 2022/23, Mfuko unategemea ongezeko la wastaafu 30,084
kutoka wastaafu 20,894 mwishoni mwa mwaka 2021/2022
Awali, Kaimu
Mkurugenzi wa Rasilimaliwatu na Utawala, Ekwabi Mujungu, alisema watumishi wako
tayari kuendelea kutoa huduma kwa mujibu wa taratibu zilizopo.
Kwa upande wake, Willy Kibona ambaye ni Mkuu wa Sekta ya Fedha TUICO Taifa alisema kazi kubwa ya baraza hilo ni kuishauri Menejimenti kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo kupitia mpango wa mwaka na bajeti ya Mfuko kwa mwaka wa fedha 2022/23 pamoja na makadirio ya mapato na matumizi.
"Tunashukuru
kwa somo tosha kutoka kwa mgeni rasmi ambalo litaweza kusaidia kujadili
kushauri na hatimaye yale yatakayokuwa tumependekeza tutakapokuja kwako kwenye
Bodi yapate baraka," alisema Kibona.
No comments:
Post a Comment