HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

April 22, 2022

Norway yaahidi kuendelea kushirikiana na Tanzania


Waziri wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, alisalimiana na Waziri wa Norway anayesimamia masuala ya Maendeleo ya Kimataifa, Bi. Anne Tvinnereim, walipokutana kando ya mikutano ya majira ya kipupwe ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), inayofanyika Jijini Washington DC, Marekani.

 

 

 Benny Mwaipaja, Washington DC

 

Serikali ya Norway imeahidi kuendelea kushirikiana na Tanzania katika hatua zake za kukuza uchumi na kuwaletea maendeleo wananchi wake kupitia miradi mbalimbali ambayo nchi hiyo inafadhili katika sekta za nishati, kusaidia kaya masikini na usimamizi wa fedha za umma.

 

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Norway anayesimamia masuala ya Maendeleo ya Kimataifa, Bi. Anne Tvinnereim, kando ya mikutano ya majira ya kipupwe ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), inayofanyika Jijini Washington DC, Marekani.

 

Alisema kuwa tangu mwaka 2010, Norway imewekeza nchini Tanzania zaidi ya shilingi bilioni 300 kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo iliyosaidia kuboresha maisha ya watu na kuchangia agenda ya mabadiliko iliyowekwa na Serikali katika kuinua Maisha ya watu wake.

 

“Serikali ya Norway imeahidi kwamba itaendelea kushirikiana na Tanzania kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika sekta ya nishati hususan usambazaji wa umeme vijijini, mabadiliko ya tabia nchi na kusaidia sekta ya fedha za umma” alisema Dkt. Nchemba

 

Kwa upande wake Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Norway Bi. Anne Tvinnereim, alisema kuwa nchi yake imeridhishwa na utekelezaji wa miradi inayofadhiliwa na nchi yake ikiwemo kuzisaidia kaya masikini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii-TASAF.

 

Aliahidi kuwa nchi yake itaendelea kusaidia mpango huo wa TASAF pamoja na kuangalia maeneo ya kuboresha hifadhi ya mazingira ambayo ni changamoto kubwa inayochangia mabadiliko ya tabia nchi.

 

Dkt. Nchemba anaongoza ujumbe wa Tanzania kwenye mikutano ya Majira ya Kipupwe ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa-IMF inayofanyika jijini Washington DC nchini Marekani.

 

No comments:

Post a Comment

Pages