HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

April 06, 2022

Serikali yawekeza zaidi kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum

 Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, akizungumza wakati uzindizi wa usambazaji wa bajaji kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum.

Dk. Aneth Komba Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) akizungumza wakati wa uzinduzi huo leo.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia akikata utepe kuashiria uzindizi wa usambazaji wa bajaji kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum.
 
Na Irene Mark

KIASI cha Sh. 707,000,000 zimetumika kuchapisha vitabu vya braille kwa wanafunzi wasioona, vyenye maandishi yaliyokuzwa, kununua vifaa saidizi kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum na bajaji kwaajili ya wanafunzi wa kidato cha tano, sita na vyuo vikuu hapa nchini.

Hii ni mara ya kwanza katika historia ya elimu hapa nchini ambapo nakala 9,100 ya vitabu vya Braille vyenye jumla ya juzuu 32,140 na vitabu vya michoro mguso vyenye juzuu 20,400 vimechapishwa.

Sambamba na vitabu hivyo vitabu vya kiada vya maandishi yalikuzwa nakala 60,283 kwa ajili ya wanafunzi wenye uoni hafifu ambavyo vimechapwa kwa uwiano wa vitabu vitatu kwa mwanafunzi mmoja.

Akizindua usambazaji wa vitabu, vifaa saidizi na bajaji 35 leo Aprili 5,2022 Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda alisema fedha hizo ni  sehemu ya Sh. bilioni 64 iliyopokelewa wizarani kwa ajili ya mradi wa  maendeleo kwa ustawi na mapambano dhidi ya UVIKO 19 kati ya zaidi yabSh. trilioni tatu ambazo serikali ilizipokea na kuelekeza kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo elimu.

Waziri Mkenda amesema vitabu hivyo vitawezesha wanafunzi wenye mahitaji maalumu ya uoni kujifunza kama ilivyo kwa wanafunzi wengine na kupata stadi na mahiri zitakazowawezesha kumudu changamoto wakati wa kujifunza.

“Ndio maana tunamshukuru sana Rais wetu mama Samia Suluhu Hassa kwa kuiendeleza kwa vitendo sekta ya elimu... haijapata kutokea na wahakikishia vyuo vyote vikuu 11 vyenye wanafunzi wenye mahita maalum watapata vifaa hivi.

“...Kuna Tablets (vishkwambi) 175 kwa ajili ya kupakia kamusi ya Lugha ya Alama ya Tanzania kwa wanafunzi viziwi na Audiometer 39 kwa za kupima kiwango cha usikivu kwa wanafunzi viziwi kwakuwa kila baada ya miezi mitatu lazima mwanafunzi apimwe uwezo wake wa kusikia.

“Vitabu hivyo vinakusudiwa kusambazwa kwa wanafunzi 3,677 katika shule 764 za wanafunzi wasioona na wenye uoni hafifu Tanzania Bara na Zanzibar wakati vifaa maalum na saidizi vitagawiwa kwa wanafunzi 364 wenye ulemavu wa viungo, wasioona na viziwi wanaosoma katika vyuo vikuu 11,” amesisitiza Profesa Mkenda.

Awali waziri huyo alisema  serikali ina uhusiano mzuri na wadau mbalimbali wa maendeleo na kupitia hayo  imepata msaada wa kuandaa na kuchapa vitabu kutoka shirika la Siloam Center for the Blind lenye maskani yake Korea Kusini na ofisi ndogo mkoani Kilimanjaro.

“Shirika hili limetusaidia kuchapa vitabu vya kiada vya Braille kwa sekondari kidato cha kwanza hadi cha sita nakala 4,000 za masomo ya English, History, Geography, Fasihi, Lugha na Sarufi kwa uwiano wa vitabu vitatu kwa mwanafunzi mmoja,” amesema Profesa Mkenda.

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Dk. Aneth Komba amesema vitabu hivyo vitasambazwa katika halmashauri zote Tanzania bara na visiwani kwenye shule zote zenye wanafunzi wenye mahitaji maalumu kwa uwiano uliopangwa.

Kwa mujibu wa Dk. Komba kazi ya uandaaji wa vitabu hivyo ilianza Oktoba 2021 na vyote vimechapwa hapa nchi kwenye kiwanda cha serikali kiitwacho PressB ambacho ni pekee hapa nchini kinachochapa vitabu vya breill.

Amesema vitabu walivyopokea kutoka shirika la Siloam ni vitabu vya kiada ambavyo viliandikwa na TET na ubadilishwaji wa vitabu hivyo umefanywa na wataalamu wa taasisi na wengine kutoka Korea Kusini na uchapishwaji umefanyika nchini Korea.

Mbunge wa Viti Maalum na Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Huduma za Jamii, Rose Tweve amesema serikali inahakikisha watoto wote wanapata elimu bila kujali hali zao hivyo niwajibu wa wanafunzi kufanya bidii ili kupata wabunge, mawaziri na rais ajae.

No comments:

Post a Comment

Pages