MKUU WA WILAYA APONGEZA KASI YA DKT. BITEKO KWENYE USIMAMIZI SEKTA YA MADINI
Tume ya Madini kupitia Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Morogoro imezindua Kituo cha Ukaguzi na Biashara ya Madini katika Wilaya ya Gairo.
Uzinduzi huo uliofanywa na Mkuu wa Wilaya ya Gairo Mhe Jabir Makame umehudhuriwa na viongozi mbalimbali ikiwa ni pamoja na Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Emmanuel Shija, Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Gairo.
Wageni wengine walikuwa ni pamoja na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya ya Gairo, Katibu wa Mbunge wa Gairo, Madiwani wote wa Halmashauri ya Wilaya ya Gairo, Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji wa Madini wa Mkoa wa Morogoro (MOREMA),Dkt Mzeru Nibuka,
watumishi wa Halmashauri pamoja na wachimbaji wa Wilaya ya Gairo.
Akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa kituo hicho, Mkuu wa Wilaya ya Gairo, Jabir Makame amepongeza juhudi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita kupitia Wizara ya Madini kwa kuwasaidia wachimbaji wadogo wa madini.
Katika hatua nyingine ameipongeza Wizara ya Madini kwa uanzishwaji wa masoko ya madini nchini ambayo yamekuwa na manufaa makubwa hasa kwa wachimbaji wadogo wa madini kwa kuwa kwa sasa wanafanya biashara zao katika masoko ya uhakika huku wakiuza madini yao kulingana na bei elekezi zinazotolewa na Tume ya Madini kulingana na Soko la Dunia.
Pia amempongeza Waziri wa Madini, Dkt. Doto Biteko kwa kutimiza mapema ahadi aliyoiweka alipokua katika ziara yake Wilaya ya Gairo mapema Januari 06 mwaka huu ya kufungua Ofisi na kuleta wataalam wa Madini katika Wilaya ya Gairo.
" Nampongeza Mheshimiwa Dkt. Biteko kwa kutimiza ahadi yake ya kufungua kituo hiki pamoja na usimamizi makini kwenye Sekta ya Madini kwa kuwa mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa umeendelea kuongezeka, wachimbaji wananufaika na ninaamini kupitia kituo hiki Serikali itapata mapato zaidi ambayo yatasaidia kukuza Sekta nyingine," alihitimisha Makame
No comments:
Post a Comment