HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 01, 2022

MHAGAMA AWATAKA MAAFISA TEHAMA KUWEZESHA MIFUMO YA SERIKALI KUBADILISHANA TAARIFA KUPITIA MFUMO WA GovESB


Na Jasmine Shamwepu, Dodoma


Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na UtawalaBora Jenista Mhagama amewataka Wakuu wa Idara za Tehama Serikalini. kuhakikisha mifumo yote ya TEHAMA inayotumika katika Taasisi zeo iboreshwa ili kuweza kubadilishana taarifa ifikapo tarehe 30 Septemba, 2022. kupitia Mfumo wa Serikali wa Ubadilishanaji Taarifa (GovESB).

Mhagama  ameyasema hayo  leo Jijini hapa katika kikao kazi cha wakuu wa Idara za Tehama kujadili uzingatiaji wa sheria Kanuni taratibu viwango na miongozo ya Serikali Mtandao katika Taasisi za umma


Amesema Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025, Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2021/22 - 2025/26) na Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2020 kwa pamoja zinatambua nafasi ya TEHAMA katika kufikia malengo ya Taifa na hivyo kusisitiza haja ya ongezeko la matumizi yake katika utendaji wa shughuli za Serikali na utoaji huduma kwa Umma.


Amesema yameonekana  manufaa ya kusanifu, kutengeneza, kusimika na kuendesha mifumo mhimili na tumizi ya kimkakati na kisekta kwa kutumia wataalamu wa ndani kutoka katika taasisi zenu na wataalamu kutoka Mamlaka ya Serikali Mtandao.


"Katika kuhakikisha TEHAMA inatoa mchango chanya katika uendeshaji na usimamizi wa majukumu ya Serikali, jitihada mbalimbali zimefanyika na mafanikio yamepatikana katika maeneo ya Sera, Sheria, Kanuni, Viwango na Miongozo; Usimamizi; Miundombinu; Mifumo tumizi na Shirikishi; na Huduma za Serikali Mtandao.

Aidha  amesema  pamoja na mafanikio yaliyopatikana , lakini eneo hilo bado linakabiliwa na changamoto kadhaa za kiutekelezaji, zikiwemo: Kutoshabihiana kati ya taratibu za utendaji kazi Serikalini  na teknolojia inayotumika kutopatikana thamani halisi ya fedha zinazotumika kwenye miradi.

Aidha amesema Serikali imeweka msukumo mpya katika kutekeleza Serikali Mtandao kwa kusisitiza ushirikiano na matumizi ya pamoja ya rasilimali za TEHAMA miongoni mwa Taasisi za Umma, ikiwa ni pamoja na kuboresha taratibu za utendaji kazi kwa kila taasisi.

“Naelekeza matumizi ya Mifumo Shirikishi pale taratibu za utendaji kazi za Taasisi za Umma zinapokuwa zinafanana badala ya kila Taasisi kuwa na Mfumo unaojitegemea.

“Naelekeza kuwa, Mifumo tumizi yote ya Serikali ihifadhiwe katika Vituo vya kuhifadhia Mifumo vilivyoidhinishwa na Mamlaka ya Serikali Mtandao.

Hata hivyo amesema kuwa  kila taasisi ihakikishe kuwa inahifadhi Mifumo yake katika vituo mbadala (Disaster Recovery Site) vinavyofanya kazi ili kuwa na uhakika wa kuendelea kutoa huduma pale inapotokea hitilafu kwenye kituo kikuu (Primary Site).


Mhagama amesema ili kuhakikisha TEHAMA inatoa mchango chanya katika uendeshaji na usimamizi wa majukumu ya Serikali, jitihada mbalimbali zimefanyika na mafanikio yamepatikana katika maeneo ya Sera, Sheria, Kanuni, Viwango.

Kwa upande wake Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais,Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Hassan Kitenge,amesema kuwa maboresho ya Utumishi wa Umma yamefanyika katika eneo la sera na mifumo ili kuongoza utekelezaji wa jitihada za serikali mtandao.
‘Utekelezaji wa jitihada za Serikali Mtandao ni moja ya maeneo muhimu ya maboresho yaliyofanyika katika Utumishi wa Umma, ambao umesaidia kuboresha utendaji kazi na utoaji huduma kwa Umma.”amesema Bw.Kitenge

Awali Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), Mhandisi Benedict Ndomba,amesema kuwa e-GA, ni Taasisi ya Umma iliyoanzishwa kwa Sheria ya Serikali Mtandao Na. 10 ya Mwaka 2019 ikiwa na jukumu la kuratibu, kusimamia, kukuza jitihada za Serikali Mtandao na kuhimiza uzingatiaji wa Sera, Sheria, Kanuni, Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao ili kuhakikisha Taasisi za Umma zinatumia TEHAMA kwa usahihi na Usalama.

Hivyo Mhandisi Ndomba amesema kuwa ni wajibu wa Wakuu wa Idara/Vitengo vya TEHAMA Serikalini kusimamia utekelezaji wa jitihada za Serikali Mtandao katika Taasisi zao kwa weledi na kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao iliyopo.


Hata hivyo amewataka washiriki  wa kikao kazi hicho kuwa wasikivu lakini pia kuwa tayari kutoa maoni yao pale itakapohitajika ili waweze kufikia lengo la uzingatiaji wa Sheria, Kanuni, Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao wakati wa utekelezaji wa Jitihada za Serikali Mtandao kwenye Taasisi zao.

No comments:

Post a Comment

Pages