WAANDAAJI wa Shindano la Miss Tanzania Kampuni ya ‘The Look’ kwa kushirikiana na wadhamini wa shindano hilo Startimes, Benki ya CRDB na kampuni za bima za Sanlam na Strategis, wamekabidhi zawadi kwa walimbwende walioingia katika tano bora katika kinyang’anyiro cha Miss Tanzania 2022 ambapo mlimbwende Halima Kopwe kutoka Mtwara aliibuka kidedea, Mashindano hayo yalifikia kilele mnamo Tarehe 20 Mwezi Mei 2022.
Akizungumza katika hafla ya kukabidhi zawadi iliyofanyika Makao Makuu ya Benki ya CRDB jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Kamati ya Miss Tanzania Azama Mashango, alisema zawadi, hizo ni sehemu ya ahadi ambazo zilitolewa kwa washiriki wa shindano hilo, huku akiwashukuru wadhamini wote waliojitokeza kufanikisha Miss Tanzania 2022.
“Leo hapa tunakabidhi zawadi kwa walimbwende walioingia katika tano bora kama ambavyo taratibu za mashindano zinavyojieleza. Zawadi zitakazokabidhiwa ni pamoja na bima ya maisha yenye jumla ya thamani ya Shilingi Milioni 50 kwa muda wa miaka mitano kutoka Kampuni ya Sanlam Life, bima ya gari kwa mshindi wa kwanza kwa ajili ya kukinga na majanga yatokananyo na ajali, kutoka sanlam general, bima ya safari kwa safari zote za mashindano ya nje kwa mwaka mzima kutoka kampuni ya strategis na zawadi za fedha taslimu,” alibainisha Azama.
Akikabidhi zawadi ya bima ya gari kwa mshindi wa kwanza wa Miss Tanzania 2022, Mkurugenzi wa Wateja Wadogo na Wakati wa Benki ya CRDB, Boma Labala alisema zawadi hiyo itamsaidia kumkinga mshindi huyo ambaye alipewa zawadi ya gari aina ya Benzi katika majanga yanayosababishwa na ajali.
“Thamani ya gari aliyopewa mrembo wetu Halima ni Shilingi Milioni 30, ni gari ya thamani kubwa, hivyo inapaswa kuwekewa ulinzi wa kibima ili aweze kufurahia matunda ya shindano hili. Benki yetu kupitia kitengo cha bima tumesema tutamsaidia kufanikisha hili kwa kumkatia bima ya mwaka mzima ili kumkinga na majanga,” alisema Boma.
Boma alisema kuwa kwa kutambua mchango wa mashindano hayo katika kuwainua vijana wakike na kulitangaza Taifa, Benki hiyo kwa kushirikiana na washirika wake wa kampuni za bima za Sanlam na Strategis pia wametoa bima ya maisha zenye jumla ya Shilingi Milioni 50, pamoja na bima ya safari ya mwaka kwa walimbwende ambao watashiriki mashindano ya kimataifa.
“Shindano la Miss Tanzania limekuwa daraja la mafanikio kwa vijana wengi wa kike wenye sifa za urembo. Lakini pia limesaidia kubadilisha mtazamo wa jamii juu ya kujishughulisha na maswala ya urembo. Sasa hivi wengi wetu tunatazama Sanaa ya Urembo kama ajira kwasababu ya mafanikio ambayo yanatokana na shindano hili dunia kote,” aliongezea.
Boma.Pamoja na zawadi hizo, Benki ya CRDB pia iliwafungulia washindi hao akaunti na kuwawezesha kupokea zawadi zao za fedha ambapo mshindi wa kwanza alikabidhiwa kiasi cha shilingi milioni 10, mshindi wa pili shilingi milioni 5, mshindi wa tatu shillingi milioni 3, mshindi wa nne shillingi milioni 1, na mshindi wa tano shilingi milioni 1. Benki hiyo pia iliahidi kutoa elimu ya fedha bure ilikuwasaidia kufikia malengo yao ya kifedha.
No comments:
Post a Comment