SERIKALI
ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) inaendelea kujikita katika kutekeleza
mipango ya uhakika ya upatikanaji wa nishati mbadala kwa kwaajili ya
maendeleo endelevu Zanzibar kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa nje
na ndani ya nchi.
Akiwasilisha
mada ya nishati mbadala katika jukwaa la uwekezaji upatikanaji wa
nishati mbadala Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na
Nishati, Madini, Dkt Mngereza Mzee Miraji, amesema mipango inayoendelea
Tanzania katika kusambaza umeme vijijini inalenga kuimarisha maisha na
kukuza maendeleo ya kijamii na kiuchumi kupitia upatikanaji wa nishati
ya umeme wa uhakika.
Dkt
Mngereza alisema, Dira ya Maendeleo ya Zanzibar ya 2050 inaeleza
mahitaji ya mfumo wa nishati ya uhakika kupitia vyanzo mbalimbali vya
nishati, hasa nishati mbadala.
Aidha
alisema Benki ya Dunia inaisaidia Zanzibar kutekeleza mradi wa
Kuifanyia Mabadiliko Sekta ya Nishati - ZESTA ili kutatua changamoto za
upatikanaji umeme kisiwani humo.
Alifahamisha
kwamba kukamilika kwa mradi wa ZESTA kutapanua upatikanaji wa huduma za
umeme wa uhakika na wenye ufanisi ili kuongeza uzalishaji wa nishati
mbadala ikiwemo kuzalisha 18MW za umeme wa jua.
Alisema,
mradi huo ni mradi wa miaka mitano unaotekelezwa kwa gharama ya dola
Milioni 142 kutoka Benki ya Dunia na utakapokamilika utanufaisha watu
300,800 katika kisiwa cha Zanzibar.
Aidha
amefafanua kuwa, ukuaji wa sekta ya nishati unatarajiwa kuchangia na
kukuza ukuaji wa uchumi, huduma za jamii pamoja na kuvutia wawekezaji.
“Juhudi
kubwa zimechukuliwa na Serikali kuhakikisha Zanzibar inakuwa na vyanzo
vyake vya ndani vya kuzalisha umeme ambapo matumizi ya nishati ya jua
yameongezeka kwa asilimia 6.1 mwaka 2019-2020 ambapo lengo ni kufikia
asilimia 20 ifikapo mwaka 2030,” alisema Dkt Mgereza.
Dkt
Mgereza aliongeza kuwa Visiwa vya Kokota na Njau, kisiwani Pemba
vimeunganishwa na umeme wa jua wa KW 130 ambayo unanufaisha zaidi ya
Kaya 140, mradi huo umesaidia kuondoa changamoto ya nishati ya umeme
katika visiwa hivyo, umetekelezwa kwa ushirikiano ya SMZ na Serikali ya
Norway kwa gharama ya dola za Marekani 458,000.
Naye
Meneja Mwakilishi kutoka katika mradi wa nishati katika nchi za Umoja
wa Ulaya, Massimiliano Pedretti, ameihakikishia serikali ya Tanzania
kuwa nchi hizo zitaendelea kushirikiana na Tanzania ili kuleta maendeleo
endelevu katika sekta ya uchumi na jamii.
Jukwaa
hilo la siku tatu lililoshirikisha wadau kutoka nchi mbali mbali ikiwa
ni pamoja na Congo DRC, Uganda na Msumbuji, lilifunguliwa na Waziri wa
Nishati, January Makamba, ambapo wadau walijadili mafanikio na
changamoto zinazoikabili sekta ya nishati katika nchi zao.
No comments:
Post a Comment