Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Anayesimamia Sekta ya Uvuvi, Dkt. Rashid Tamatamah (kushoto) akipeana mkono na na Meneja Mkuu, Kampuni ya ujenzi ya CHEC, Cheng Yongjian (kulia) ikiwa ni ishara ya makubaliano baada ya kusaini nyaraka za makubaliano ya ujenzi wa bandari ya uvuvi ya Kilwa katika hafla fupi ya utiaji saini iliyofanyika jijini Dodoma Juni 7, 2022.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki akitoa hotuba katika hafla fupi ya utiaji saini wa nyaraka za makubaliano ya ujenzi wa Bandari ya Uvuvi ya Kilwa baina ya Serikali na Kampuni ya Ujenzi ya China Habour Engineering Company (CHEC) iliyofanyika jijini Dodoma Juni 7, 2022. Kulia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, Mhe. Dkt. Christina Ishengoma na kushoto ni Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, anayesimamia sekta ya Uvuvi, Dkt. Rashid Tamatamah.
Mbunge wa Kilwa, Mhe. Ally Kasinge akitoa neno la shukrani wakati wa hafla fupi ya utiaji saini wa nyaraka za makubaliano ya ujenzi wa bandari ya uvuvi ya Kilwa baina ya serikali na Kampuni ya ujenzi ya China Habour Engineering Company (CHEC) iliyofanyika jijini Dodoma Juni 7, 2022.
Na Mbaraka Kambona, Dodoma.
WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki amesema mradi wa ujenzi wa
bandari ya uvuvi utakaoanza hivi karibuni wilayani Kilwa, mkoani Lindi
utachochea ukuaji wa uchumi wa bluu na kupelekea kuongezeka kwa pato la taifa.
Ndaki aliyasema hayo wakati wa hafla fupi ya utiaji saini wa nyaraka za
makubaliano ya ujenzi wa bandari hiyo baina ya Serikali na Kampuni ya ujenzi ya
China Habour Engineering Company (CHEC) iliyofanyika jijini Dodoma Juni 7,
2022.
Alisema kuwa anamshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kukubali kwake
kujenga bandari hiyo kwa fedha za ndani huku akiongeza kuwa kukamilika kwa
bandari hiyo kutakuwa na faida nyingi za kiuchumi kwa wavuvi, wananchi na taifa
kwa ujumla.
“Namshukuru Mhe. Rais kwa kukubali kufanya jambo hili ambalo lilikuwa ndoto
sasa kuwa kweli, amekubali kutoa jumla ya shilingi za Kitanzania bilioni 266.79
kwa ajili ya ujenzi wa bandari hii pamoja na miundombinu mingine ikiwemo soko
la kisasa la samaki”, alisema.
Aliongeza kwa kusema kuwa bandari hiyo ikikamilika itakuwa na uwezo wa
kuhifadhi tani Elfu 60 kwa mwaka za mazao ya uvuvi kutoka katika ukanda wa bahari ya hindi huku
akisisitiza kuwa bandari hiyo itakuwa kubwa kuliko zote zilizopo katika pwani
ya Afrika Mashariki.
Waziri Ndaki alifafanua kwamba uwepo wa bandari hiyo ambayo imesubiriwa
tangu nchi ipate uhuru itasaidia kuinua
uzalishaji wa mazao ya uvuvi kwa wingi kutoka katika ukanda huo wa bahari
tofauti na ilivyo sasa ambapo mazao mengi yanayotumika yanatoka katika ukanda wa
ziwa ikiwemo ziwa Viktoria na ziwa Tanganyika.
“Uwepo wa bandari hii pia kutasaidia kuvutia wawekezaji wengine katika
nyanja mbalimbali ikiwemo viwanda vya kuchakata mazao ya samaki na hivyo
itasaidia kutoa ajira kwa wananchi na kukuza uchumi wa nchi”, aliongeza.
Aidha, Waziri Ndaki aliutaka uongozi wa Kampuni ya CHEC ambao ndio wamepewa
Kandarasi ya kujenga bandari hiyo kuhakikisha ujenzi huo unakamilika ndani ya
muda uliopangwa kwa sababu pesa kwa ajili ya kufanya kazi hiyo zipo hivyo
hawatavumilia udhuru wowote utakaopelekea kuchelewesha mradi huo.
Naye, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji,
Mhe. Dkt. Christina Ishengoma aliihimiza wizara kuhakikisha wanamsimamia vyema
mkandarasi aliyekabidhiwa kujenga bandari hiyo huku akiongeza kuwa wao kama
kamati watakuwa wanafuatilia kwa karibu kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa
wakati ili watanzania waone matunda ya pesa yao.
Kwa upande wake, Meneja Mkuu, Kampuni ya ujenzi ya CHEC, Cheng Yongjian
alisema kuwa mradi huo ni muhimu kwa serikali ya Tanzania hivyo kwa kutumia
uzoefu walionao wanaimani kwamba watakamilisha ujenzi wa bandari hiyo ndani ya
muda uliopangwa.
Awali akitoa taarifa fupi kuhusu mchakato wa ujenzi wa bandari hiyo, Katibu
Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, anayesimamia
sekta ya Uvuvi, Dkt. Rashid Tamatamah alisema kuwa kutokuwapo kwa
bandari ya uvuvi kumepelekea nchi kupoteza mapato mengi yatokanayo na sekta ya
uvuvi kwa sababu Meli kubwa zinazofanya uvuvi katika ukanda maalum wa bahari
hapa nchini zimekuwa zikishusha shehena ya samaki katika nchi jirani na hivyo
kupelekea nchi hizo kunufaika zaidi kuliko Tanzania.
No comments:
Post a Comment