HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 05, 2022

Serikali yapandisha hadhi maonesho ya dhahabu Geita


NA TATU MOHAMED 

SERIKALI imeyapandisha hadhi maonesho ya dhahabu yanayofanyika mwezi Septemba ya kila mwaka mkoani Geita na kuwa ya kitaifa.

Kufuatia kupanda hadhi kwa maonesho hayo Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade) wameingia makubaliano na mkoa wa Geita ya kuhakikisha maonesho hayo ya dhahabu yanakuwa na hadhi hiyo ya kitaifa.

Akizungumza wakati wa utiaji saini wa makubaliano hayo uliyofanyika  katika maonesho ya 46 ya biashara ya kimataifa, Mkuu wa Mkoa wa Geita Rosemary Senyamule amesema makubaliano hayo yatakwenda kuyafanya maonesho hayo ya dhahabu kuwa makubwa kuliko yote yanayofanyika hapa nchini.

Amesema maonesho hayo ya dhahabu kuwa ya kitaifa yatasaidia kukua na kuwavutia wawekezaji wengi ndani na nje ya nchi kushiriki katika kuonesha bidhaa zao.

"Tunafahamu kuwa muda uliobakia ni mchache kwani Septemba ndiyo yatafanyika maonesho ya dhahabu mkoani Geita, tumeshawaambia wadau kuwa hatutayapeleka mbele hivyo kwa kushirikiana na Tantrade tutakaa pamoja na kukubaliana namna bora ya kuyaboresha ili yaonekane ya hadhi na kisasa," amesema 

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Geita, Zahra Michuzi amesema makubaliano hayo yatasaidia kuleta mapinduzi na kufanya mabadiliko kwenye teknolojia ya dhahabu.ndani ya mkoa wa Geita.

Amesema wanataka kufanya mageuzi makubwa katika sekta ya madini ya dhahabu hivyo kupanda hadhi kwa maonesho hayo kutachagiza mabadiliko hayo.

"Tumepokea kwa furaha nia njema ya kuingia makubaliano na Tantrade kwani kutafanga maonesho hayo kutambulika nchini na kupanua wigo mpana wa ufanyaji biashara," amesema 

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Tantrade,  Latifa Khamis amesema kusainiwa kwa makubaliano hayo kutakwenda kuimarisha na kuufanya uwanja wa Geita kuwa wa kisasa kwa ajili ya maonesho ya dhahabu.


No comments:

Post a Comment

Pages