Waziri wa Ulinzi Dk. Stergomena Tax ( aliyevaa barakoa) akikagua miradi ya SUMAJKT katika maonesho ya 46 ya kimataifa ya biashara yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Nyerere maarufu kama Sabasaba.
Aidha amesema shirika hilo lipo tayari kushirikiana na wafanyabiashara wengine nchini kwa lengo la kutengeneza bidhaa bora na zenye viwango ikiwemo za vyakula ili ziweze kupenya katika masoko ya nje ya nchi.
Tax amesema hayo leo wakati alipotembelea banda la SUMAJKT lililopo kwenye maonesho ya 46 ya Kimataifa ya biashara yanayofanyika katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere maarufu kama Sabasaba Dar es Salaam, shirika hilo linaadhimisha miaka 41 tangu kuanzishwa kwake.
Amesema SUMAJKT ipo tayari kushirikiana na mfanyabiashara biashara yoyote aliyetayari katika kutengeneza bidhaa zenye ubora na viwango.
Amesisitiza kuwa ubora wa bidhaa ni muhimu kwa walaji na kama bidhaa zinazozalishwa hazina ubora, hawawezi kuzipeleka katika masoko ya nje.
“Serikali imefanya jitihada kubwa kama ambavyo Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akitembea maeneo mbalimbali duniani kwa lengo la kututafutia fursa za kibiashara hivyo, ni jukumu letu kuzalisha bidhaa zitakazokubalika kwenye masoko ya nje,” amesema Tax.
Amesema zipo fursa huru za biashara Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo Kusini kwa Afrika na Umoja wa Afrika ambazo zinahitaji ubora, wingi wa bidhaa na kuzifikisha kwa wakati hivyo watimize matakwa hayo kufanya biashara nchi mbalimbali.
“Nitoe wito kwa SUMAJKT nafahamu wamefanya kazi kubwa katika miaka hii 41 lakini wanapaswa waangalie eneo moja kubwa ambalo watajipanua na kufika maeneo mengi, miradi mikubwa ya kitaifa ndio jukumu tulilonalo kuanzisha ili kuchangia zaidi katika uchumi wa nchi na masuala mengine ya kijamii,” alifafanua.
Alisisitiza kubwa SUMAJKT wana viwanda vya kuzalisha bidhaa mbalimbali ikiwemo vya kuzalisha malighafi kwa ajili ya sekta ya kilimo, uchakataji wa bidhaa za ujenzi, samani na huduma mbalimbali za ulinzi bandarini na kuimarisha huduma katika sekta afya, matumizi ya teknolojia katika ulinzi.
“SUMAJKT ni mahali sahihi pa biashara na uwekezaji, zipo shughuli mbalimbali zinazofanyika kwa ajili ya kuchangia uchumi wa nchi yetu. Jukumu la jeshi letu ni kulinda mipaka na uchumi ili kuwa huru jambo ambalo linachagizwa na kujitegemea kiuchumi na kijamii na kubaki imara kama taifa na kutekeleza majukumu mengine,” amesema Tax
Hata hivyo amesema kuwa bajeti ya mwaka huu kwenye SUMAJKT kuna ongezeko la asilimia zaidi ya 200 kwenye miradi ya maendeleo na kwamba haitagusa miradi yote badala yake itahusika katika kuboresha miundombinu ya kimkakati ikiwemo kilimo.
Anesema katika bajeti kuu ya serikali msisitizo mkubwa umewekwa katika uzalishaji kupunguza changamoto ya mfumo wa bei kwenye mafuta ya kupikia hivyo, watashirikiana na Wizara ya Kilimo kuona namna watakavyoshiriki katika uzalishaji huo.
Pia amesema jeshi hilo litaendelea kulinda mipaka ya nchi kwa lengo la kuwa huru na kujitegemea kiuchumi na kijamii ili kubaki imara kama taifa na kutekeleza majukumu mengine.
“Aliongeza kuwa wanao vijana wanaopitia JKT ambako wanapata stadi mbalimbali hivyo, aliwataka vijana hao wanaojitolea kutumia stadi hizo kujiendeleza kiuchumi na kufundisha wengine.
No comments:
Post a Comment