Meneja Mkazi wa M-Bet, Fernando Perez (wa pili kushoto), akikabidhi mfano wa hundi ya Sh. Bilioni 26.1 kwa viongozi wa Simba SC wakati wa hafla ya kutangaza udhamini wa miaka 5 walioingia na klabu ya Simba. Kutoka kulia ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez, Mkurugenzi wa Masoko wa M Bet, Allen Mushi, Menyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba SC, Salim Abdallah ‘Try again’ na Mwenyekiti Simba, Murtaza Mangungu.
Na Mwandishi Wetu
MIAMBA ya soka Tanzania bara, Simba SC imeingia mkataba wa shilingi Bilioni 26 na kampuni ya kubashiri ya M-Bet kwa miaka mitano.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Masoko wa M Bet, Allen Mushi, Umma utambue kwamba wameingia mkataba na Simba, kwa sababu hata rangi zao zinaendana.
Mushi alisema Simba ni timu kubwa Tanzania, hakuna mjadala kuhusu hilo.
Alichanganua kwamba mwaka wa kwanza – Sh. Bil 4.670 huku mwaka wa pili-Bil 4.925 wakati mwaka wa tatu- Bil 5.205, mwaka wa nne Bil 5.514 na wa tano – Bil 5.853. jumla ikiwa ni Bilioni 26, milioni 168 na 5000.
"Tunaamini kama M-Bet tukishirikiana na Simba tutajitangaza ndani na nje ya Tanzania," alisema Allen Mushi na kuongeza.
"M-Bet ni kampuni namba moja ya michezo ya kubashiri, sasa tunashirikiana na klabu namba moja Tanzania." Alisema Mushi.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi wa Simba SC, Salim Abdallah ‘Try again’ alisema hajawahi kuona Simba day kama hii, imeandaliwa ikaandalika, naona kama siku haifiki. Tuje kwa wingi siku hiyo.
"M-Bet mlichotaka mtakipata. Pesa ni nyingi hizi, tumieni hii nafasi kutanua biashara yenu kupitia mashabiki wetu." Alisema Try Again na kuongeza.
"Tunakaribisha makampuni mengine kufanya nayo kazi sababu hii ni klabu ya watu, wasiogope tuko tayari kufanya nao kazi," alisema Try Again.
Try again alisema Simba ni waungwana, wanawashukuru wadhamini waliopita, sasa wako na mdhamini mpya na wanaamini watafanyakazi kwa karibu.
Meneja wa kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally alisema pesa hiyo iliyotajwa haijahusisha marupurupu mengine ambayo Simba itayapata kutoka M-Bet.
Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez alisema hiyo ni mara ya kwanza mdhamini mkubwa anakuwa na senior team pekee, huko nyuma mdhamini mkuu alikuwa kwa timu zote lakini sasa timu zingine wanaweza kuzifuatia udhamini wake.
"Kwa ukubwa wa Simba ni lazima kujihusisha na kampuni ambayo inaongoza kwenye biashara ambayo wanafanya. Mkiangalia takwimu M-Bet wanaongoza kwa ukubwa Tanzania," alisema Gonzalez na kuongeza.
"Leo ni siku kubwa kwa Simba na M-Bet. Swali kubwa ni kwanini M-Bet. Sababu kubwa ni wameweza kukidhi mahitaji yetu," alisema Gonzalez.
No comments:
Post a Comment