SERIKALI imepongezwa kwa hatua ya kufungua mlango wa majadiliano kuhusu mabadilio ya sheria zinazoongoza tasnia ya habari nchini.
Pongezi hizo zimetolewa na Theophil Makunga, Mwenyekiti Mstaafu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), wakati akizungumza na Kituo cha Televisheni cha Channel Ten kwenye Kipindi cha Baragumu Live leo tarehe 1 Agosti 2022.
Kwenye kipindi hicho, Makunga amesema serikali imeona umuhimu wa kufungua mjadala wa mazungumzo ya sheria hizo, kutokana na wadau wa habari kueleza kuwepo haja ya kuzipitia upya.
Tayari serikali kupitia Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, imeandaa mkutano wa wadau wa habari utakaofanyika kwa siku mbili (tarehe 11 – 12 Agosti 2022).
“Kuna vipengele vinatubana, tunaishukuru serikali kwa kukubali kufungua mjadala wa mazungumzo yanayolenga kuangalia namna gani ya kuondoa hivyo vipengele ili tuwe huru zaidi,” amesema Makunga.
Akizungumzia historia ya sheria ya vyombo vya habari nchini, Makunga amesema tangu awali, vyombo vya habari vilikuwa vikiendeshwa kwa sheria iliyoundwa mwaka 1979 – Sheria ya Magazeti.
“Sheria hii ilikuwa ikiongoza uandishi wa habari, utangazaji na namna gani ya kufanya, ilikuwa inasema ukiwa na kosa kwenye gazeti, anaweza kushtakiwa mwandishi, mhariri, mmiliki, mchapaji wa gazeti,” amesema.
Hata hivyo anasema, kutokana na mabadiliko ya teknolojia, sheria sasa inapaswa kuendanani na wakati uliopo.
Akizungumzia umuhimu wa kuwa na Baraza Huru la Vyombo vya Habari amesema, kuna kila sababu ya wanataaluma wanahabari wakasimamia chombo kinachowaongoza wao wenyewe.
Ameeleza kuwa, Baraza Huru la Vyombo vya Habari Huru linapaswa kuwa kama mabaraza ya taaluma zingine akitoa mfanbo wa namna Baraza la Madaktari pia Baraza la Wanasheria yanavyoendeshwa.
“Kinapaswa kuwa chombo cha wanataaluma wahusika kinachoendeshwa na waandishi wa habari. Kwa hiyo, matatizo yote yatakayokuwa yanahusu taaluma ya waandishi wa habari, yapitie kule kwenye lile baraza ambalo litakuwa likiendeshwa na waandishi wa habari wenyewe.
“Hatua ya serikali ama Mkurugenzin wa Idara ya Habari Maelezo kupewa jukumu la kuangalia maudhui na kazi za vyombo vya habari, sisi tunaliona sio sasasawa.
“Maombi yetu ni kwamba, lile jukumu badala ya kupewa Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo, lipewe Baraza Huru la Vyombo vya Habari kusimamia mambo yote yanayohusu taaluma ya Habari,” amesema Makunga.
No comments:
Post a Comment