HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 04, 2022

STAMICO lajipanga kuzindua Mkaa Mbadala


Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Dk. Venance Mwasse wakati akitoa taarifa kwa wanahabari kuhusu matukio yatakayofanyika kuelekea kilele cha Maadhimisho ya kutimiza Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Shirika hilo.
 
 
Na Hussein Ndubikile, Dar es Salaam

Katika kuelekea Kilele cha Maadhimisho ya kutimiza Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Shirika hilo limesema litafanya matukio mbalimbali ikiwemo kupanda miti, utoaji wa vifaa kwa wachimbaji wadogo wa madini wenye changamoto ya usikivu,kutembelea viongozi waliotangulia, kutembelea wagonjwa wa Saratani pamoja na kuzindua mkaa mpya (mbadala).

Hayo yamesemwa jijini Dar es Salaam na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Dkt. Venance Mwasse wakati akitoa taarifa kwa wanahabari kuhusu matukio yatakayofanyika kuelekea kilele cha maadhimisho hayo.

Amebainisha kuwa STAMICO itashiriki kupanda miti 10,000 katika eneo la Ipagala mjini Dodoma ambalo wamekabidhiwa na Serikali na kwamba miti hiyo itapandwa Agosti 10 mwaka huu huku mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Selemani Jafo.

" Tumeamua kupanda miti hii ili kuhakikisha tunaunga mkono juhudi za Serikali ya kupambana na changamoto ya mabadiliko ya tabia ya nchi, amsesma Dkt. Venance.

Amesisitiza kuwa upandaji miti umebeba kauli mbiu isemayo panda miti tumia mkaa mbadala okoa mazingira na kwamba wana mkakati wa kuitunza mpaka itakapokua.

Ameongeza kuwa wamepanga kutoa vifaa vya uchimbaji kwa wachimbaji wadogo hao waliopo mkoani Geita kwani kwa kufanya hivyo watatoa fursa kwao kushiriki kuvuna maliasili zilizopo.

Amefafanua kuwa watayatumia maadhimisho hayo kutembelea viongozi kuwaeleza hali ya STAMICO na mafanikio yaliyopatikana pamoja na kutembelea wagonjwa wa Saratani waliopo Taasisi ya Saratani ya Ocean Road.

Katika hatua nyingine, amesema Agosti 12 mwaka siku ya kilele itakayofanyika Dodoma watazindua mkaa mbadala ambao umebuniwa na STAMICO.

Dkt. Venance amesema katika ubunifu wa mkaa wameshirikisha Tume ya Sayansi na Teknolojia Tanzania (COSTECH) huku tayari wakiwa wamepatiwa kibali na Shirika la Viwango Nchini (TBS).

Pia amesema kuwa STAMICO tangu kuanzishwa mwaka 1972 hadi limepata mfanikio mbalimbali ikiwemo uzinduzi wa kiwanda cha kwanza cha kusafisha dhahabu mkoani Mwanza, kuingia kwenye biashara kwa kushindana na mashirika mengine na kupata ushindi wa jumla kwenye Maonesho ya SabaSaba.

Mafaniko mengine ni kuwapa mafunzo na vifaa wachimbaji wadogo, ununuzi wa mitambo miwili iliyopo Kibaha na Kiwira yenye uwezo wa kuzalisha tani 2 kwa saa za mkaa huo huku  mbili zikiwa zimeshaagizwa moja itapelekwa Dodoma na nyingine Kanda ya Ziwa.



No comments:

Post a Comment

Pages