HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 16, 2022

TAFITI ZA WATAALAMU WA NDANI KUTUMIKA KUTATUA CHANGAMOTO ZA JAMII

NA WyEST, MOROGORO


SERIKALI  imeanzisha mpango kabambe wa kutumia tafiti zilizofanyika na zinazoendelea kufanyika na wataalamu wa ndani ili kutatua changamoto zilizopo kwenye jamii.

Akizungumza katika Uzinduzi wa Kigoda cha Utafiti cha Oliver Tambo (Oliver Tambo Research Chair for Viral Epidemics) uliofanyika katika Chuo cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Morogoro, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Omari  Kipanga amesema katika kutekeleza mpango huo Serikali imetenga Shilingi bilioni 9 katika mwaka wa fedha 2022/2023 ili kuchochea maendeleo na matumizi ya tafiti katika nyanja ya Sayansi, Ubunifu na Teknolojia .

Naibu Waziri Kipanga amesema bajeti hiyo ya kufanya na kuendeleza tafiti nchini imeongezeka kutoka bilioni 3 mwaka wa fedha uliopita ikiwa ni hatua ya Serikali kuhakikisha matatizo yaliyopo kwenye jamii yanapatiwa ufumbuzi kwa njia za kitaalamu.

“Wakati tunapata uhuru ujinga ulikuwa ni moja ya maadui, hatuwezi kuondoa ujinga bila kufanya tafiti. Maendeleo yatapatikana kama tutaondoa ujinga kwanza,” amefafanua Mhe. Kipanga.

Naibu Waziri Kipanga amesema kwamba mpango huo utatekelezwa kupitia Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) ambayo itakuwa inaratibu tafiti zote ili kutoa kwenye maaandishi na kuziingiza kwenye matumizi.

"Kupitia tafiti hizi tunakwenda kutatua changamoto zilizopo, lengo kubwa sio tafiti hizi kubaki tu kwenye makaratasi, " amesema Kipanga.

Kipanga amezitaka taasisi zote zinazofanya tafiti nchini kushirikiana na COSTECH ili kuhakikisha tafiti zinazofanyika zinatoa majibu katika changamoto zinazoikabili jamii.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kigoda cha Utafiti cha Oliver R.Tambo  nchini, Prof. Gerald Misinzo kutoka Chuo cha Sokoine cha Kilimo (SUA) amebainisha kwamba lengo kuu la uanzishwaji wa kigoda hicho ni kupambana na magonjwa ya kuambukiza ili kuboresha afya ya binadamu na mifugo kupitia tafiti kutoka taasisi za elimu na wanazuoni wake.

No comments:

Post a Comment

Pages