NA MWANDISHI WETU, MATUKIO DAIMA APP
ALIYEKUWA MGOMBEA Ubunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Ado Shaibu Ado amewatakia heri wabunge tisa walioshinda kwenye kinyang'anyiro hicho.
Taarifa kwa umma aliyoitoa leo Septemba 23,2022 Ado amesema anawatakia uwakilishi mwema washindi tisa wanaokwenda kuliwakilisha Taifa kwenye Bunge la EALA.
Mbali na hilo, Ado ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo amewashukuru wabunge waliompigia kura jana akisema hatowasahau.
"Mimi nilikuwa mgombea kwenye kundi la Walio wachache bungeni. Mshindani wangu, Mashaka Ngole wa CUF alichaguliwa.
"Licha ya kutoshinda, napenda kueleza yafuatayo;
"Ninakishukuru chama changu cha ACT Wazalendo kwa kuniamini na kunichagua kukiwakilisha kwenye Uchaguzi huu. Wajibu wetu ulikuwa ni kulionesha Taifa kuwa ACT Wazalendo kinaweza kutoa uwakilishi bora kuliwakilisha Taifa kwenye Bunge la EALA. Ni imani yangu kuwa tumetekeleza wajibu wetu ipasavyo." amesema Ado na kuongeza kuwa:
"Yaliyotokea yalikuwa nje ya uwezo wetu,
ninawashukuru wabunge wote 78 walionipigia kura. chama chetu kina wabunge wanne pekee ndani ya Bunge. Hata hivyo wabunge 74 wa nje ya chama changu, kutoka Kambi ya wachache na Chama Cha Mapinduzi (CCM) walioonesha imani na mimi, asanteni sana"ilisema taarifa hiyo ya Ado kwa umma.
Aidha licha ya kushindwa mgombea huyo wa ACT-Wazalendo ameshukuru pia wabunge ambao hawakumpigia kura ambapo amesema wamempa changamoto kwamba kila jambo kwenye safari ya siasa ni darasa.
Katika taarifa hiyo, pia amewashukuru wabunge wa Kambi ya walio wachache bungeni kwa kazi kubwa ya kumshika mkono, kumuongoza kwenye siasa za bungeni.
No comments:
Post a Comment