Rais wa CAJ Christopher Isiguzo.
Na Mwandishi Wetu, Nairobi
BARAZA
la Waandishi wa Habari Afrika, (CAJ), limefanikiwa kupata Rais wake
Christopher Isiguzo kutoka nchini Nigeria, huku likitangazwa rasmi kuwa
jiji la Nairobi nchini Kenya ndio yatakuwa makao makuu yake.
Maamuzi
hayo yamefikiwa na bodi ya uongozi ya CAJ ilokutana juzi jumatano
(Sept.21) kujadili maendeleo ya taasisi hiyo na kutoa mamlaka ya
kisheria kuanzishwa kwa Sekretarieti ya CAJ Jijini Nairobi, nchini
Kenya.
CAJ iliyozinduliwa
Juni 23 mwaka 2020, tayari imesajiliwa rasmi chini ya sheria za Kenya
ambapo katika kikao chake, bodi hiyo pia imetangaza maendeleo mapya
yaliyofikiwa kisheria yanayotoa msukumo kukabiliana na changamoto za
waandishi wa habari barani Afrika.
Baraza
la CAJ linalenga kuleta mtazamo wa Kiafrika kwa masuala ya
kushughulikia changamoto za uhuru wa vyombo vya habari, usalama wa
wanahabari na upatikanaji wa habari, unaoathiri wanahabari wanapokuwa
wakifanya kazi zao kulingana na Ajenda ya Umoja wa Afrika 2063 na mwamko
wa Kiafrika kukabiliana na masuala hayo.
Rais
wa CAJ Isiguzo kutoka nchini Nigeria ambaye pia ni Rais wa Muungano wa
Wanahabari wa Nigeria (NUJ) anabainisha kuwa Baraza hilo linaendelea
kuchukua jukumu la kulinda na kutetea uhuru wa kujieleza na habari kama
ilivyoainishwa katika Azimio la Kanuni za Uhuru wa Kujieleza na Kupata
Habari Barani Afrika.
Isiguzo
alichaguliwa kuwa Rais mpya wa CAJ kwenye mkutano wa Baraza la Uongozi,
akichukua nafasi ya Rais mwanzilishi Alexandre Niyungeko, Rais wa
Muungano wa wanahabari wa Burundi UBJ ambaye amejiuzulu kutokana na
majukumu mengine
Katibu
wa CAJ anaendelea kuwa William Oloo kutoka chama cha Wanahabari wa
Kenya(KCA) na mweka hazina, Bi. Monique Kacou kutoka nchini Ivory cost
(Cote d'Iviore).
Wajumbe
wengine wa Baraza la Uongozi ni Ibrahima Ndiaye kutoka nchini Senegal,
Bi. Idda Francis Mushi kutoka Tanzania, Bi. Indira Correia Balde kutoka
Guinea - Bissau, Syabonga Dlamini wa Swaziland, Abdalle Ahmed Mumin wa
Somalia Bi. Patsy Athanase wa visiwa vye Shelisheli (Seychelles) na
Emmanuel Chibwana kuroka nchini Malawi.
Mjumbe
mwingine mpya anatarajiwa kutangazwa wakati wowote toka sasa kuziba
nafasi ya Foster Dongozi kutoka Zimbabwe aliyefariki dunia Desemba mwaka
Jana.
"Sote
tunafurahia usajili wa CAJ kwa sababu hii itaiwezesha kutekeleza jukumu
lake katika kuchangia utatuzi wa changamoto zinazowakabili waandishi wa
habari barani Afrika,'' Alisema Alexander Niyungeko, Rais wa CAJ
aliyemaliza muda wake.
Alisisitiza
wadau mbalimbali kushirikiana na Baraza hilo kuleta maendeleo
yanayokusudiwa katika tasnia ya habari kwani yatatoa nafasi ya kusonga
mbele na kutoa nafasi ya kuthibitisha mamlaka hiyo kusonga mbele kwa
kasi kubwa katika kutekeleza wajibu wa kushughulikia matatizo
yanayowakabili wanahabari barani Afrika.
Rais
Isiguzo pia alisisitiza dhamira kubwa ya CAJ kukabiliana na
changamoto zinazowakabili wanahabari barani ambapo tayari wameidhinisha
vikao vya mashauriano vya kikanda kuhusu Mpango wa Utekelezaji wa Umoja
wa Mataifa kuhusu Usalama wa Waandishi wa Habari (UNPA) unaoongozwa na
UNESCO.
"Matokeo haya
yatachangia kuboreshwa kwa juhudi katika kushughulikia suala hili la
usalama wa wanahabari barani Afrika" Alisema Rais huyo mpya wa CAJ.
Hivi
karibuni CAJ wataweka wazi mpango wa shughuli mbalimbali watakazofanya
zikilenga kushughulikia dhamira za wanahabari barani Afrika ambapo Rais
Isiguzo amewaalika washirika mbalimbali wa maendeleo na masuala ya
wanahabari kufanya nao kazi nasi kufanikisha malengo hayo.
No comments:
Post a Comment