HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

September 18, 2022

Nipe Fagio: Siku ya Usafi Duniani jukwaa madhubuti la kupambana na janga la plastiki duniani


Afisa Uhamasishaji Jamii Taasisi ya Nipe Fagio, Nasra Juma, akizungumza mara baada ya kufanya usafi katika eneo la Daraja la waenda kwa miguu katika Stendi ya Maguli ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Usafi Duniani.
Afisa Usafi Manispaa ya Ubungo, Boniface Katikiro, akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Usafi Duniani ambapo watumishi wa manispaa pamoja na wadau mbalimbali walijitokeza katika eneo la Daraja la waende kwa miguu katika Stendi ya Magufuli Mbezi Louis jijini Dar es Salaam.
Taka zilizokusanywa katika eneo la Daraja la waenda kwa miguu katika stendi ya Magufuli.
Wafanyakazi wa taasisi ya Nipe Fagio wakipima taka walizokusanya katika eneo la Daraja la waenda kwa miguu katika Stendi ya Maguufuli Baada ya zoezi la kufanya usafi. Kutoka kulia ni Abdi Hudefo, Marium Shadrack, Ibrahim Mlenga na Regina Obedi.
Siku ya Usafi Duniani ni siku muhimu katika ukuzaji uelewa juu uchafuzi wa mazingira kwa ujumla. Ni fursa ya kuwaleta watu pamoja ili kujifunza kuhusu hali ya taka nchini na kusukuma sera thabiti zinazohusiana na mzunguko wa maisha ya plastiki.

 

Akizungumza wakati wa kuadhimisha Siku ya Usafi Duniani jana katika eneo la fukwe za  Salenda jijini Dar es Salaam, Ana Le Rocha, Mkurugenzi Mtendaji wa Nipe Fagio alisema shirika lake linajivunia kuwa kiongozi wa Siku ya Usafi Duniani nchini Tanzania.

 

“Tunajivunia sana kuongoza Siku ya Usafi Duniani nchini kwa mwaka wa tano mfululizo, tangu mwaka 2018. Mwaka huu tulikuwa na usafi katika maeneo nane jijini Dar es Salaam na maeneo ishirini katika mikoa mingine nchini.

 

"Pamoja na uchafu kuwa suala la msingi nchini Tanzania, matukio kama Siku ya Usafi Duniani ni njia sahihi ya sisi kushirikisha watu na kukusanya takwimu kupitia ukaguzi wa taka na chapa, ambayo hutusaidia kubaini wachafuzi wakuu na vyanzo vya uchafuzi wa mazingira nchini. Tunatumai kuwa juhudi hizi zitaleta mabadiliko ya kimfumo katika sekta ya mazingira na usimamizi wa taka ngumu nchini Tanzania” Ana alisema.

 

Bi. Rocha alieleza kuwa ripoti ya ukaguzi wa taka na chapa iliyotokana na Siku ya Usafi Duniani ni muhimu katika kuwapa watoa maamuzi zana za kushughulikia suala la taka na uchafuzi wa plastiki kwa kuimarisha maamuzi yanayotokana na takwimu ili kuleta mabadiliko chanya nchini Tanzania.

 

"Moja ya malengo ya kuandaa Siku ya Usafi Duniani ni kuwafanya watu kuelewa vyema uchafuzi unaopatikana katika mazingira yetu na kukusanya takwimu ili kupaza sauti kwa ajili ya tatuzi, kama vile uwajibikaji kwa wazalishaji wa vifungashio vya plastiki, unaowezesha mabadiliko ya kimfumo" Ana alibainisha.

 

Kama kiongozi wa Siku ya Usafi Duniani Tanzania, Nipe Fagio inapenda kuwashukuru washirika wetu kote nchini kwa msaada wao na kupongeza vikundi vyote vya kijamii, watu wa kujitolea, mashirika yasiyo ya kiserikali, serikali za mitaa, shule na wahusika wengine wakuu katika sekta ya mazingira kwa kufanya Siku ya Usafi Duniani mwaka huu kuwa yenye mafanikio.

 

"Tunahitaji kufanya kazi kwa pamoja ili tuweze kushinda uchafuzi wa plastiki na kuifanya Tanzania kuwa nchi isiyo na taka kupitia uhamasishaji, ukusanyaji wa takwimu na kupaza sauti zaidi ili kuleta mabadiliko," Ana aliongeza.

 

Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari Kibamba walioshiriki kufanya usafi wakiwa katika eneo la Daraja la waenda kwa miguu katika Stendi ya Magufuli.


No comments:

Post a Comment

Pages