HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

September 18, 2022

NMB mabingwa wa soka NMB-Bunge Bonanza

 Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB ,Ruth Zaipuna (katikati) akinyanyua kombe juu kushangilia pamoja na wachezaji wa mpira wa miguu wa benki hiyo walipoishinda timu ya Bunge Sports Club kwenye bonanza la kivumbi na jasho liliofanyika Jijini mwisho wa wiki ,NMB iliandaa bananza hili lilishirikisha michezo mbalimbali kati ya Wabunge na Wafanyakazi wa NMB, mechi hiyo ilichezwa uwanja wa Kilimani na michezo mingene ilifanyika viwanja vya Chinangali Park.
 

Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson akikabidhi kikombe kwa timu ya mpira wa miguu  ya NMB baada ya kuifunga timu  ya Bunge Sports Club 2- -0 wakati wa mchezo uliochezwa kwenye viwanja vya Kilimani jijini Dodoma kwenye Bonanza la NMB Kivumbi na Jasho. Kushoto ni Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna.

 

NA MWANDISHI WETU, DODOMA

KIKOSI cha timu ya soka ya NMB, kimeibuka wababe wa Tamasha la NMB-Bunge Bonanza 2022 ‘Kivumbi na Jasho,’ baada ya kuwachapa wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ‘Bunge FC’ kwa mabao 2-0 katika fainali ya bonanza hilo, Jumamosi jioni, kwenye Uwanja wa Kilimani, jijini Dodoma.

NMB-Bunge Bonanza ni tamasha la siku moja la michezo baina ya timu za Benki ya NMB na Bunge, lililoanza kwa matembezi yaliyoongozwa na Spika Dk. Tulia Ackson na Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB (iliyoandaa bonanza hilo), Ruth Zaipuna, kabla ya timu za kila upande kuchuana katika michezo mbalimbali.

Baada ya Bunge SC kufanya vema katika michezo ya Kuvuta Kamba, Kukimbiza Kuku, Mpira wa Wavu, Netiboli na Kikapu kwenye viwanja vya Chinangali Park, NMB ilikuja juu na kupindua meza ya matokeo hayo kwa kushinda fainali ya soka kwa mabao ya Alex Joseph na Laurent Kilumanga.

Ukiondoa ushindi huo, NMB-Bunge Bonanza limefanyika kwa mafanikio makubwa, huku kila upande miongoni mwa timu shiriki, ukilitumia tamasha hilo kufanya mazoezi ya ushiriki wa matukio tofauti ya kimichezo, yanayohusisha timu za NMB na Bunge SC.

Wakati Bunge SC, ikilitumia bonanza hilo kunoa makucha kuelekea Mashindano ya tisa ya Mabunge ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA 2022), timu za NMB wamelitumia kupasha misuli moto, kujiandaa na Mbio za Hisani za NMB Marathon 2022 ‘Mwendo wa Upendo.’

Akizungumza wakati wa bonanza hilo, Spika Dk. Tulia alisema ya kwamba, wanaamini NMB-Bunge Bonanza 2022 yatakuwa na mchango chanya kwa timu zao, kuelekea EALA 2022 na kwamba walipanga kulipa uzito mkubwa ili kuhakikisha linanufaisha timu zao, kama ilivyokuwa mwaka jana.

“Mwaka jana tulishiriki Mashindano ya Mabunge na tuliongoza kwa ujumla, mafanikio hayo yalitokana na ubora na uimara wa timu zetu, ambao ulianzia katika NMB-Bunge Bonanza, na tunaamini limetupa mazoezi ya kutosha mwaka huu, kutuwezesha kufanya makubwa zaidi ya msimu uliopita,” alisema Spika Tulia.   

Kwa upande wake, Zaipuna alisema timu zake zimeshiriki bonanza hilo kama sehemu ya uenyeji wao wa Mbio za NMB Marathon, zitakazofanyika hivi karibuni, Mgeni Rasmi akitarajiwa kuwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, likilenga kukusanya Sh. Mil. 600 za kusaidia matibabu ya kinamama wenye Fistula.

“Siku chache zijazo tutakuwa wenyeji wa NMB Marathon, ndio maana tunalitumia bonanza hili kufanya mazoezi, huku tukiwaomba Mheshimiwa Spika na Wabunge wote, mjitokeze kujisajili ili kushiriki mbio hizo, zenye lengo la kukusanya pesa za kutibia kinana mama wenye fistula katika Hospitali ya CCBRT,” alisema.


Licha ya NMB kuibuka na ushindi huo katika soka, pia ilishinda mchezo wa kufukuza Kuku wanaume, huku timu za Bunge zikitawala Michezo Mingine yote.

Katika Kikapu wanaume, Bunge iliibuka na ushindi wa pointi 44-40, huku upande wa wanawake Bunge nao wakishinda bada ya NMB kutoingiza timu uwanjani.
 
Michezo Mingine ambayo Bunge iliishinda NMB ni Kuvuta Kamba (wanawake na wanaume), netiboli 29-4, wavu wanawake na kufukuza Kuku wanawake.

No comments:

Post a Comment

Pages