Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa pamoja na Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna
(kulia) wakimkabidhi Afisa Mtendaji Mkuu wa hospitali ya CCBRT, Brenda
Msangi mfano wa hundi yenye thamani ya Sh. Mil. 600 wakati wa mbio za
hisani za NMB Marathon 2022 ‘Mwendo wa Upendo’ kwa ajili ya kusaidia
matibabu ya akinamama wenye Fistula wanaotibiwa katika hospitali ya
CCBRT. Mbio ziliandaliwa na Benki ya NMB zilianzia na kuishia kwenye
viwanja vya Leaders Kinondoni jijini Dar es Salaam, mwishoni mwa wiki.
Kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya NMB, Dk. Edwin Mhede. (NA MPIGA PICHA
WETU).
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa (katikati)
akiongoza mbio hisani za NMB Marathon 2022 ‘Mwendo wa Upendo’ zilizoanzia na
kuishia kwenye viwanja vya Leaders Kinondoni jijini Dar es Salaam. Mbio hizo
zilizoandaliwa na Benki ya NMB, zililenga kukusanya kiasi cha Sh. Mil. 600 za
kusaidia matibabu ya akinamama wenye Fistula wanaotibiwa katika hospitali ya
CCBRT. Kulia ni Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna na wa pili kulia ni Mwenyekiti
wa Bodi ya NMB, Dk. Edwin Mhede.
Mwenyekiti wa Bodi ya NMB, Dk.
Edwin Mhede (kulia), akimvisha medali Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati wa
mbio za hisani za NMB Marathon 2022 ‘Mwendo wa Upendo’ zilizoanzia na kuishia
kwenye viwanja vya Leaders Kinondoni jijini Dar es Salaam, mwishoni mwa wiki. Mbio
hizo ziliandaliwa na Benki ya NMB kwa ajili ya kusaidia matibabu ya akinamama
wenye Fistula wanaotibiwa katika hospitali ya CCBRT. Katikati ni Afisa Mtendaji
Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna.
Na Mwandishi Wetu
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, ameiomba Bodi ya
Wakurugenzi ya Benki ya NMB chini ya Mwenyekiti wa Bodi, Dk. Edwin Mhede
na Menejimenti ya benki hiyo chini ya Afisa Mtendaji Mkuu Ruth Zaipuna,
kuendeleza Mbio za Hisani za NMB Marathon licha ya kuvuka lengo la
kukusanya Sh. Bil. 1 katika kipindi cha miaka miwili.
NMB
Marathon zilianzishwa mwaka jana 2021, lengo likiwa kukusanya Sh. Bil. 1
katika kipindi cha miaka minne (sawa na Sh. Mil. 250 kila mwaka),
lakini mwitikio chanya ukawezesha kukusanya Sh. Mil. 400 mwaka jana na
kisha Mil. 600 mwaka huu na kufikia lengo ndani ya miaka miwili.
Akizungumza
wakati wa kutoa shukrani kwa waandaaji, wadhamini na washiriki,
mwishoni mwa mbio hizo katika viwanja vya Leaders Club, Kinondoni jijini
Dar es Salaam Jumamosi Oktoba Mosi, Waziri Mkuu Majaliwa alisema baada
ya kuvuka lengo hilo, ni wakati sahihi sasa makusanyo yatokanayo na mbio
yakaelekezwa kwingine.
“Niipongeze
Bodi ya Wakurugenzi NMB chini ya Mwenyekiti, Dk. Edwin Mhede na
Menejimenti ya benki hii chini ya Afisa Mtendaji Mkuu, Ruth Zaipuna kwa
uratibu wa jambo hili zuri.
“Wito
wangu kwa NMB, malengo yalikuwa kukusanya fedha za fistula kiasi cha
Sh. Bil. 1 katika kipindi cha miaka minne, bahati nzuri tumefikia lengo
ndani ya miaka miwili, niwasihi endeleeni kutafuta maeneo mengine ya
kusaidia kama vile magonjwa ya saratani.
“Mwakani
mbio hizi ziwepo na miaka ijayo ziwepo pia, makusanyo yakasaidie
changamoto zingine. Pia kuwe na mbio endelevu, kwa ajili ya sio tu
kukusanya fedha za kusaidia matibabu, bali pia liwe jukwaa la mazoezi
ambayo ni mhimili wa afya ya kila Mtanzania katika ujezni wa taifa,”
alibainisha.
Waziri Mkuu
Majaliwa, alikiri kuvutiwa na ubunifu wa NMB uliozaa Mbio za Hisani za
NMB Marathon, huku akizipongeza Kampuni za Bima za Sanlam na UAP, kwa
udhamini mnono uliowezesha kuvuka lengo la makusanyo ya kusaidia
matibabu ya kinamama wenye Fistula nchini.
“Shukrani
pia kwa wadhamini walioamua kuiunga mkono NMB wakiongozwa na Kampuni ya
Sanlam na UAP, ambao wameota kiasi kikubwa zaidi, Sanlam Sh. Mil. 150
na UAP Sh. Mil. 100. Kwa kweli Sanlam, UAP na wadhamini wengineo
tunawashukuru, kama tunavyowashuku wakimbiaji wote.
“Niwasihi
wakimbiaji, wadhamini, waandaaji NMB na CCBRT, tuendeleze ‘Mwendo wa
Upendo,’ tusichoke kuchangia, kwani wahenga walisema kutoa ni moyo.
Pamoja na jitihada kubwa za Serikali katika kuboresha mazingira na
miundombinu ya afya, bado inahitaji uungwaji mkono na Watazania na
wote,” alisema.
Kwa
upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna, alisema ukubwa wa
tatizo la Fistula nchini, ambako kuna wagonjwa takribani 10,000, ambao
wanaongezeka kwa mwaka wagonjwa 3,000, huku wanaotibiwa wakiwa ni 1,300
pekee, uliwasukuma kujitoa kusiadia eneo hilo la jamii.
Alimshukuru
Waziri Mkuu Majaliwa kwa kukubali kuwa sehemu ya walioshiriki tukio
hilo, lililofanyika chini ya kaulimbiu ya Mwendo wa Upendo, uliolenga
kurejesha tabasamu usoni mwa kinamama wasio na uwezo wa kumudu gharama
za matibabu ya Fistula yanayofikia takribani Sh. Mil. 4.
“Kiasi
cha Sh. Bil. 1 tulichokusanya katika miaka miwili hii badala ya minne,
kinaenda kugharamia matibabu ya fistula kwa zaidi ya wanawake 250 kwenye
Hospitali ya CCBRT.
“Wanawake
10,000 wana Fistula kote nchini na kuna ongezeko la watu 3,000 kila
mwaka, wakati wanaotibiwa ni takribani kinamama 1,300 tu. Kwahiyo
tukaona umuhimu wa kuongeza nguvu ya makusanyo ili kusaisdia zaidi,
kwani Mil. 4, ni kiasi kikubwa mno kwa Mtanzania wa kawaida kumudu
kugharamia matibabu.
“Hii
ndio siri iliyotusukuma kuona umuhimu wa kuharakisha zaidi, kwani
wagonjwa wapo wengi na wana uhitaji, ambao haupaswi kusubiri miaka
minne. Leo tumekamilisha lengo kwa miaka miwili, tunawashukuru
Watanzania waliojitoa kusaidia kulikomboa kundi la kinamama wasiojiweza
pale CCBRT,” alisisitiza.
Kwa
nyakati tofauti, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Sanlam, Julius
Magabe na Mkurugenzi Mtendaji wa UAP, Donard Muthem aliyewakilishwa na
Aulerio Kimario, walifichua kwamba afya ya jamii ni miongoni mwa
vipaumbele vyao kama taasisi kongwe za Bima na kwamba ndio siri ya
udhamini wao mnono.
No comments:
Post a Comment