Askofu kiongozi wa Kanisa la Calvary Assemblies of God, Imelda Maboya
akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uvamizi kanisani hapo.
Na Mwandishi Wetu
UONGOZI wa
Kanisa la Calvary Assemblies of God umeiomba Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan iwasaidie
kuwadhibiti baadhi ya wahuni wachache wenye nia ovu ya kutaka kuondolewa
kwa kanisa hilo lililoko Ubungo Maziwa jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika ibada ya Jumapili kanisani hapo, Mchungaji kiongozi wa
kanisa hilo, Imelda Maboya alisema wako katika eneo hilo kwa zaidi ya
miaka 22, ameshangazwa na wavamizi kuwavamia Kanisani hapo mara mbili
wakati malengo yao ni kuiombea jamii ya watanzania.
Maboya alisema ibada yao kila miezi miwili huiombea amani nchi, kuombea viongozi na wananchi.
Alisema
eneo waliloko ni la Tanzania Steal Pipe (TSP) ambao ndio wamiliki
halali wa eneo hilo lakini wako hapo kwa ofa maalum iliyotolewa kipindi
cha ubinafsishaji wa mashirika ya umma (PCRC) ambako walielezwa kwamba
ikitokea patauzwa, watapewa kipaumbele.
"Mahali
hapa lilipo kanisa kulikuwa ni kichaka cha wavuta bangi, walevi na
wahuni wengine, kanisa limesaidia kuiondosha hali hiyo," alisema.
Aliiomba serikali kuanzia wilaya, mkoa na Taifa kuwasaidia ili kuliweka sawa suala hilo.
Sylvia
Rweyemamu ambaye ni muumini wa kanisa hilo alisema mama Samia asikie
kilio chao kwani mbali ya ibada pia wanajipanga kutoa elimu kwa vijana
kuhusu sakata la Panya road ambalo ni janga kwa nchi yetu.
Anna
Nderumaki alisema alishangazwa na uvamizi wa watu zaidi ya 100
waliovamia Kanisani hapo kwa sababu katika maisha yake hajawahi kuona
uvamizi kwenye nyumba ya ibada.
Naye Ezron Matowo
alimshukuru Rais Samia ni msikivu na mwenye huruma, hivyo suala kama
hilo ni dogo zaidi kwake kwa sababu anayoyatekeleza yanaonekana.
Muumini
Placid Malaki alitumia fursa hiyo kuiomba serikali kuwaongezea eneo
hilo kwa ajili ya kufanya ibada kwani wanachotekeleza kwa ajili ya nchi
ni kikubwa zaidi.
No comments:
Post a Comment