HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

October 09, 2022

NMB yaongeza kiwango cha mkupuo mmoja wa mkopo hadi 250bn/-

 

Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Ng’wilabuzu Ludigija (wa pili kushoto) akipeana mkono na Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Benki ya NMB, Benedicto Baragomwa katika hafla ya kukutana na wateja wakubwa wa Benki ya NMB katika hoteli ya Johari Rotana jijini Dar es salaam. Kushoto ni Mstahiki Meya wa jiji la Ilala, Omar Kumbilamoto na kulia ni Meneja wa NMB Kanda ya Dar es Salaam, Donatus Richard.

 

Na Mwandishi Wetu

 

Ufanisi mkubwa wa kiutendaji ambao Benki ya NMB imeupata miaka ya hivi karibuni umeiwezesha taasisi hiyo kinara wa huduma za kifedha nchini kuimarika kiufadhili.

 

Viongozi wake waandamizi wamebainaisha mwishoni mwa juma lililopita kuwa miongoni mwa matokeo ya kufanikiwa huko kifedha ni kuiwezesha benki hiyo kuongeza kiasi cha mkupuo mmoja wa mkopo kwenye miaka ya hivi karibuni.

 

Akizungumza Ijumaa jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya Mtandao wa Wateja Wakubwa na Wanaochipukia (BEN) wa NMB Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa benki hiyo, Bw Benedicto Baragomwa, alisema kiwango kikubwa cha mkupuo mmoja wa mkopo sasa kimefikia TZS bilioni 250.

 

Kiasi hicho ni kikomo cha kikanuni ambacho benki hiyo inaweza kumkopesha mteja mmoja kwa mkupuo.

 

Hilo limewavutia sana wateja wa NMB na viongozi wa jiji na mkoa wa Dar es Salaam walioudhuria mkutano huo walioipongeza kwa hatua hiyo kubwa kiufadhili na kusema ni matokea ya uwezo wake kiubunifu na uwekezaji wa kizalendo inaoufanya nchini.

 

“Sisi ndio mkopeshaji mkubwa mwenye viwango vya faida ambavyo havina mpizani sokoni na haina tofauti tofauti za huduma za mikopo kama ile ya dharura inayopatikana papo kwa papo kidijitali kwa kutumia simu za mkononi,” Bw Baragomwa aliwaambia washiriki 100 wa mkutano wa BEN wa Mkoa wa Dar es Salaam.

 

Akizungumza katika hafla ya namna hii iliyofanyika pia katuika jiji la Mbeya, mkuu wa idara ya mikopo wa benki ya NMB, Demetus Kamguna alisema sasa hivi NMB inajivunia kuwa na mizania mipana yenye rasilimali zenye thamani ya takribani TZS trilioni 9 pamoja na amana zipatazo TZS trilioni 6.6.

 

Aidha, alisema kukua kwa mali zake zote kumesaidia kupanua kiasi cha mtaji wake hadi zaidi ya TZS trilioni 1 na kupelekea kuzidisha ukomo wa mkupuo mmoja kwa kila mkopaji mwenye sifa.

 

“Pia NMB tunatoa mikopo kadri ya uwezo wa mfanyabiashara, tukiwa na uwezo wa kutoa hado TZS bilioni 250 kwa mkopaji mmoja,” kiongozi huyo mwandamizi alisema kwenye mchapalo huo wa kujadili masuala muhimu na wateja wake wakubwa wa Mkoani Mbeya uliofunguliwa rasmi ya Mkuu wa Mkoa ya Mbeya, Bw Juma Homera.

 

Akielezea kiwango kipya cha mkupuo wa juu wa mkopo kwa kila mteja, Mkuu wa Idara ya Biashara wa NMB, Bw Alex Mgeni, alimwambia mwandishi wa habari hii kuwa maendeleo ya ukopeshaji yaliyopatikana pia ni matokea chanya ya faida kubwa ambazo NMB imekuwa ikipata miaka ya hivi karibuni.

 

Pamoja na mambo mengine mengi, faida za NMB zimekuwa pia zikitumika kuimarisha utendaji na uendeshaji wa benki hiyo na pia kudhatiti mtaji wake. Matokeo ya uwekezaji huo, Bw Mgeni alifafanua, ni pamoja na kuongeza kiwango cha NMB kuwakopesha wateja wake.

 

“Kimsingi, mtaji wetu sasa ni TZS trilioni 1.2 ambazo zinapelekea mkupuo mmoja wa mikopo yetu kufikia hadi TZS bilioni 300 kwa kuzingatia kanuni ya Benki Kuu ya benki kukopesha asilimia 25 ya mtaji wake,” Bw Mgeni alisema.

 

Katika hotuba yake ya ufunguzi, Mkjuu wa mkoa wa Mbeya aliwasihi Benki ya NMB kuendelea kuwaunga mmono wakulima kwani ni sekta inayokuwa kwa kasi sasna kwa hivi Karibuni huku akisisiktiza juu ya kuendelea kuwek nguvu kubwa katika ufadhili wa kilimo cha maparachichi, mchele na pareto.

 

Aidha, katika hafla ya jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Bw Ludigija, aliimwagia sifa NMB kwa kuja na wazo la BEN akisema si muhimu tu kwa ajili ya kupata mrejesho kutoka kwa wateja lakini pia kusaidia kuchangia mawazo ya sera za kitaifa.

 

NMB ilianzisha mtandao wa BEN mwaka 2014 ikilenga kuitumia mikutano yake kama jukwaa la kukutana na wateja wake wenye mzunguko wa fedha kuanzia TZS bilioni 5 kwa mwaka kwa ajili ya kubadirishana wazo na uzoefu wa kibiashara.

 

Mpango huo ulilenga mikoa mikubwa na inayoongoza kiuzalishaji na mpaka sasa, mtandao huu upo kwenye mikoa saba tu ambako ina washirika zaidi ya 1,000. Mikoa hiyo ni Dar es Salaam, Dodoma, Morogoro, Kilimanjaro, Mwanza, Arusha na Mbeya.

 

Kwa upande wake, Meya wa Ilala, Bw Omary Kumbilamoto, alisema NMB sasa ni mshirika wa kimkati wa maendeleo ya kibiashara wa kitaifa ambaye anaisaidia Serikali ya Awamu ya Sita kuboresha upatikanaji wa huduma za kijamii.

No comments:

Post a Comment

Pages