Na John Richard Marwa
'Kila Ndege huruka na mbawa zake' ndio, kama Popo na mbawa zake huruka kivyake, Mwewe na mbawa zake hunyakua mwenyewe, ni kama kasi ya binadamu Iko miguuni mwake.
Leo ni siku adhimu kwenu wanasimba, siku inayowakumbusha mapito yenu yaliyojenga jina lenu na limekaa kwenye mioyo ya Waafrika na wapenda soka.
Ni kipindi cha kwanza cha dakika 90 za ugenini dhidi ya De Agosto fanyeni kama mlivyowafanya Mbabane Swallows, Nkana Red Devils na Red Arrows hapo jana.
Njia ni ileile ya kusini mwa Afrika, kwenda kuwatesa kaskazini mwa Afrika mliyoifanya kuwa mbuga yenu. Sio Serengeti wala Ngorongoro bali mapori yote ya Afrika mnayatawala.
Kumbukeni 'Maji ukiyavulia nguo huna budi kiyakoga' kawaonyeshe hao wa Angola namna ya kukoga na kunawa, namna ya kutafuna kisha njooni nao muwafunze kumeza.
Vipi Ndugu yenu kawaangusha?? ama mlimuachia mzinga asijue cha kufanya? Nyuki wamemwachia nundu, sumu Iko kwenye utamu wake. Si mnajua mzinga wenu na nyuki wake, basi 'Mfuata nyuki hakosi asali', asali' yenu ni De Agosto, mumunyeni ama lambeni lunyasi.
Mnatambua kuna ugumu, lakini msisahau.. 'Mchumia juani hulia kivulini' kubalini kuteseka leo, kivuli cha makundi mtashibia hapo si mnajua zigo limetuna?!
Kama kuna ugumu utajitokeza kumbukeni Mkoba wenu... 'Mbinu hufuata mwendo' ishini humo maana mwendo wenu mnaujua, basi rejesheni mbinu zenu kwenye uwanja wa vita.
Vipi nafsi zenu zimepooza baada ya mtani kushindwa kutamba ama Azam kulishwa 'ice cream zake mwenyewe'?! Kumbukeni kuwa 'Mchimba kisima huingia mwenyewe' ndio hiki ni kisima chenu wenyewe mlichokichimba ingieni kunyweni maji yenu kwa utulivu, ndugu zenu wataendelea kujifunza wawe kama nyinyi.
Kila la heri Simba SC, kumbukeni mna Chama, Okrah, Phiri, Sakho, Bocce, Zimbwejr, Kanoute, Mkude, Mzamiru, Inonga, Onyango, Manula na vijana wenu, Afrika inawaamini ndo fahari ya hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika CAFCL.
No comments:
Post a Comment