HABARI MSETO (HEADER)


 


Breaking

October 25, 2022

PSSSF yawatahadharisha wastaafu

 

Meneja Uhusiano na Mawasiliano kwa Umma Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), James Mlowe, akitoa mada wakati wa Kikao Kazi baina ya mfuko huo na waandishi wa habari Mkoa wa Dar es Salaam. Kulia ni Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Dar es Salaam (DCPC), Sam Kamalamo na Mweka Hazina wa DCPC, Patricia Kimelemeta. (PICHA NA FRANCIS DANDE).



NA MWANDISHI WETU


MFUKO wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), kimewatahadharisha wastaafu wa mfuko huo kuwa makini na matapeli pindi wanapopata fedha zao.


Tahadhari hiyo imetolewa na Meneja wa Uhusiano na Elimu Kwa Umma wa PSSSF, James Mlowe, wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika kikao kazi baina ya mfuko huo na Chama Cha Waandishi wa Habari Dar es salaam (DCPC).


Akielezea sababu za wanachama wao kukumbwa na wimbi hilo la utapeli, alisema inatokana na sababu mbalimbali ikiwemo kutoa taarifa zao kwa wahusika wa wizi au matapeli kuwatumia maafisa waajili kutafuta taarifa zao kwa njia za udanganyifu.


Alisema, "Kuna wakati tuliwakamata matapeli watano, jijini Mwanza na tulipowahoji walisema huwatumia maofisa waajili kupata taarifa zote za wastaafu ikiwemo namba zao za simu. wanachofanya ni kudanganya kwamba  wanatoka Tamisemi au sehemu nyingine ya ajira na wanataka taarifa za wastaafu wote na maofisa waajili huwapatia."


Mlowe alitoa wito kwa waandishi wa habari kusaidia kutoa elimu kwa wastaafu kutomtumia mtu yeyote taarifa zake za kustaafu ikiwemo wafanyakazi wa PSSSF.


"Mstaafu anapopokea barua ya kustaafu anatakiwa kuanza hatua ya kufuatilia mafao yake, hivyo anatakiwa kwenda hatua inayofuata ya kufuata fomu ya PSSSF na kujaza ili kupeleka kwa mwajili wake na sio kufanya mawasiliano na mfanyakazi yeyote wa PSSSF." alisema Mlowe.


Akielezea kuhusu changamoto za kuchelewa kuwalipa wastaafu zilizokuwepo hapo nyuma alisema ilitokana na kurithi deni la Sh. trilioni moja ambalo lilitokana na madai ya kulipwa wanachama waliokuwa wametoka kwenye ajira katika mifuko minne iliyounganishwa na kuzaliwa PSSSF.


Pia alibaibisha kuwa wengine waliokuwa wakidai malipo ya mirathi  walichelewa kutokana na kutokamilisha taratibu za kutambua mrithi.


"Lakini pamoja na hayo yote tumepambana hadi mwaka jana  tumemaliza deni lote kwa mtindo wa kuwalipa wanachama wanaodai kwa awamu." alisema Mlowe.


Meneja huyo wa Uhusiano na Elimu kwa Umma wa PSSSF, aliongeza kuwa changamoto nyingine ilitokana na wanachama kutokamilishiwa michango na waajili wao, hivyo kusababisha kutumia muda kumfuatilia muajiri wake.

No comments:

Post a Comment

Pages