Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Omary Mgumba akizungumza na wananchi waliofurika kusikiliza namna ya utatuzi wa mgogoro huo.
Na Mwandishi Wetu, Tanga
MKUU wa Mkoa wa Tanga, Omar Mgumba ametumia muda wa dakika 30 kutatua mgogoro wa mpaka uliodumu kwa miaka zaidi ya 30 kati ya Wilaya za Tanga Jiji na Mkinga na kutoa maagizo sita.
Mgogoro huo ulihusisha Mtaa wa Mlemi uliopo Halmashauri ya Jiji la Tanga na Gombero iliyopo Mkinga.
Akizungumza na viongozi na wananchi wa maeneo hayo, RC Mgumba alisema hatua alizochukua ni kuunda timu iliyokuwa na viongozi wa maeneo husika na wataalamu kutoka Wizara ya Ardhi mkoani Tanga ambao walibaini mambo manane ambayo aliyapatia ufumbuzi wakati huo huo.
Aidha, RC Mgumba alibainisha kuwa viongozi waliopita walijitahidi kutatua mgogoro ambao ni mchakato lakini imeangukia mgogoro huo utatuliwe na yeye.
“Mgogoro huu umetokana na mambo mbalimbali ikiwamo uelewa wa viongozi wa wananchi katika kutambua mipaka.
“Ukiangalia Mkinga imezaliwa mwaka 2005 walipopata eneo lao la utawala la Wilaya ya Mkinga katika kutambua mipaka yao wakaenda kuweka mipaka sehemu tofauti na mpaka halisi ulipo na watu wa Tanga wakasema kama Mkinga wamesema mpaka wao uko pale sisi tutabaki Tanga kwa hiyo wa Tanga hawana makosa yoyote sisi wenyewe Mkinga tunasema eneo letu linaishia hapa.
“Lakini baada ya timu hii kupita tumebaini kuwa kimsingi matangazo yote matatu ya magazeti ya serikali ambapo tangazo la kwanza Namba 89 la kuanzisha Halmashauri ya Tanga la mwaka 1983, Tangazo la pili Namba 237 la mwaka 2005 la kuanzisha Jiji la Tanga na tangazo la tatu la gazeti la serikali namba 337 la mwaka 2005 la kuanzisha Wilaya mpya ya Mkinga matangazo yote matatu yanashabihiana mipaka iliyotamkwa. Kwa hiyo hatuna mgogoro kwenye matangazo ya serikali yote matatu yanakubaliana mpaka ndiyo hapo ulipopita,” alisema RC Mgumba.
Hata hivyo, RC Mgumba alibainisha kuwa tangazo lingine la kuanzisha Kata ya Mzizima nalo linashabihiana na matangazo hayo manne kwa hiyo hauna mgogoro kwenye matangazo hayo ya serikali.
“Sasa baada ya timu yetu kupitia kuna mambo ambayo yamebainika. Jambo la kwanza sehemu ya wakazi wanaoitikia katika Mtaa wa Mlemi Halmashauri ya Jiji la Tanga, wapo ndani ya Wilaya ya Mkinga kwa mujibu wa tafsiri ya matangazo hayo ya serikali.
“Tumebaini kuna nyumba 54 zilizopo kwenye eneo la mgogoro ambapo awali zilikuwa zinatambulika kwamba zipo Wilaya ya Tanga sasa zitatambulika ziko Wilaya ya Mkinga.
“Jambo la pili ni uelewa wa wananchi wenye eneo lenye mgogoro hususani la mipaka ya Mtaa wa Mlemi unatokana na kilichokuwa Kijiji cha Mlemi ambacho mipaka yake inashabihiana na mipaka ya upimaji ya Kijiji cha Gombero.
“Jambo la tatu ni mpaka wa upimaji wa vijiji vya Gombero Wilaya ya Mkinga kilichokuwa Kjiji cha Mlemi Halmashauri ya Jiji la Tanga inashabihiana na jambo la nne ni mpaka wa mapipa uliowekwa na Wilaya ya Mkinga hauko sahihi kwa mujibu wa tafsiri za mipaka iliyotokana na matangazo ya serikali Namba 237 la mwaka 2005 na Namba 337 la mwaka 2005 na hivyo kuacha sehemu ya eneo la Wilaya ya Mkinga ndani ya Halmashauri ya Jiji la Tanga,” alisema.
RC Mgumba alibainisha jambo la tano ni kuwa mipaka ya upimaji wa vijiji vya Gombero Wilaya ya Mkinga na kilichokuwa Kijiji cha Mlemi Halmashauri ya Jiji la Tanga haishabihiani na mipaka kwa mujibu wa tafsiri ya matangazo ya serikali.
Alisema jambo la sita timu hiyo ilibaini kuwa Shule ya Msingi ya Rubawa iliyosajiliwa tangu Julai Mosi mwaka 1992 na kuhudumiwa na Halmashauri ya Jiji la Tanga, iko ndani ya Wilaya ya Mkinga kwa mujibu wa tafsiri ya matangazo ya serikali.
“Jambo la saba tulibaini kuwa tangazo la serikali lililokwenda kata za Halmashauri za Jiji la Tanga hususani Kata ya Mzizima ambapo Mtaa wa Mlemi upo haitoi tafsiri sahihi juu ya mpaka wa wilaya.
“Mwisho ni kwamba kuwepo kwa tangazo la serikali namba 176 la Agosti 9, mwaka 1996 ambalo limetangaza maeneo ya mpango kikiwemo Kijiji cha Gombero ambapo itasimamiwa na sheria ya mipango miji namba 8 ya mwaka 2007,” alisema.
Pamoja na mambo mengine, Mgumba alisema yapo mambo mengine ambayo yamebainishwa na timu yake, kwamba baadhi ya wenyeviti wa mitaa wa Kata ya Mzizima katika Halmashauri ya Jiji la Tanga walikuwa wanauza ardhi kwa wananchi wa Tanga na nje ya Tanga na wanajua tangu mwaka 2005 Halmashauri ya Tanga ilishageuka kuwa Jiji la Tanga.
“Kwa mujibu wa sheria hiyo Namba 8 ya Mipango Miji ya Mwaka 2007, mamlaka za miji na jiji ardhi yake upatikanaji wake hauko kwenye mamlaka ama ya Mwenyekiti wa Kijiji au wananchi wa mtaa huo, ndiyo maana kule jiji kunaitwa mitaa huku Gombero vijijini tunaitwa vijiji,” alisema.
Baada ya kuzungumzia kiini hicho Mgogoro kama ilivyobainishwa na timu yake, RC Mgumba alitoa maelekezo sita ambayo yalimaliza mgogoro huo.
Katika hatua hiyo, aliwaagiza wataalamu, viongozi wa pande zote mbili, wenyeviti na wananchi wote kushiriki kwa kupita kwenye mipaka yao ili wajue mipaka ya Tanga na Mkinga inaishia wapi.
“Sasa basi, natoa amelekezo kwamba mapipa yote yaliyopandwa kwenye mipaka isiyo sahihi yang’olewe kuanzia leo. Mapipa hayo na alama nyingine zote za kudumu ziwekwe kwenye mipaka sahihi unaotambulika kwa mujibu wa sheria ili hata wenye hizo nyumba 54 wajijue wako eneo gani kwamba zamani walikuwa Tanga Jiji sasa wanakuwa Mkinga.
“Na wananchi msipate hofu kuwa zamani ulikuwa kule sasa umehamia huku ardhi itabaki ya kwako, nyumba ya kwako kilichobadilika tu ni utawala. Kwamba awali ulikuwa unaitikia Tanga sasa utaitikia Mkinga kila kitu ni cha kwako hakuna mtu atakuja kukusogeza kama ardhi yako ulipata kwa mujibu wa shria, lakini kama ulipata kwa Mwenyekiti wa Kijiji alikuuzia basi njoo huku wakurasimishe viongozi wa huku.
“Mipaka iliyowekwa kwa mujibu wa sheria iheshimiwe na ifuatwe. Upimaji wa kijiji cha Gombero na kilichokuwa Kijiji cha Mlemi ufanyiwe mabadiliko ili kuendana na tafsiri ya mpaka uliopo kwa mujibu wa matangazo ya serikali tangazo la mwaka 1996 lilipotosha ule mpaka sasa uwekwe vizuri,” alisema.
Aidha, Mgumba aliwaagiza Wakuu wa Wilaya ya Tanga na Mkinga kuwepo siku ya kukabidhiana maeneo na rasilimali za umma watu watambue maeneo yao kama zilikuwa zinasomeka Tanga Jiji sasa zisomeke Mkinga na mapipa yaliyowekwa yaondolewe.
Alisema tangazo la serikali iliyoanzisha halmashauri ya Tanga Namba 294 la mwaka 1994 lifanyiwe marekebisho hususani kwenye mipaka ya Mzizima ambayo ni kata ya mpakani inapopakana na Mlemi ili iendane na mpaka kwa mujibu wa sheria na tangazo la serikali Namba 237 la mwaka 2005.
“La sita na la mwisho; Kijiji cha Gombero kimetangazwa kuwa ni eneo la mpango mwaka 1996 hivyoi ni vema maeneo yake yakaandaliwa mipango ya kina kwa kuzuia ujenzi holela na kuwa na uendelezaji unaofuata sheria kwa mujibu wa Sheria ya Mipango Miji Namba 8 ya mwaka 2007,” alisema RC Mgumba.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga, Pili Mnyema alisema kunapokuwa na changamoto ya kutoelewana hali inakuwa si nzuri lakini wananchi hao licha ya kuwepo kwa mgogoro huo wameendelea kuwa wamoja, wasikivu na wavumilivu na hatimaye changamoto yao imepata ufumbuzi.
No comments:
Post a Comment