Na Dotto Mwaibale, Singida
SERIKALI katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2023/2024 inatarajia kutenga Sh.Bilioni 4.6 kwa ajili ya kununua zana za kilimo Mkoa wa Singida.
Waziri wa Kilimo Hussein Bashe ameyasema hayo kwenye kikao cha kupanga mkakati wa kuongeza uzalishaji wa zao la alizeti kilicho washirikisha mkuu wa mkoa, wakuu wa wilaya, wenyeviti na wakurugenzi wa halmashauri pamoja na maafisa kilimo ambacho kiliketi leo Oktoba 5, 2022 katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
Alisema Serikali baada ya kununua zana hizo halmashauri zitatakiwa zitenge maeneo maalumu ambapo zana hizo zitawekwa na kutakuwepo mtu maalum wa kuzisimamia na wakulima watakuwa wakienda kukodisha.
Alisema fedha zitakazopatikana baada ya wakulima kukodi zana hizo zitarudishwa Serikalini na kwenda kununua zana hizo katika mikoa mingine.
Awali akitoa mchanganua wa bajeti ya ununuzi wa zana hizo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya mkakati ya kuongeza uzalishaji wa zao hilo Justice Kijazi alisema Halmashauri za Wilaya za Ikungi,Mkalama, Iramba na Itigi kila moja zitahitaji zana zenye thamani ya Sh.706 Milioni.
Alisema Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni itahitaji Sh.791Milioni huku Singida DC ikiwa ni Sh.309 Milioni.
Akizungumzia kuhusu mpango mkakati wa zana hizo Kijazi alisema ni kuimarisha upatikanaji wa zana bora za kilimo, mkoa unaboresha mazingira ya uwekezaji ili kuvutia wawekezaji wa zana za kilimo, kuanzisha vituo vya umahiri wa zana (Agricultural mechanization hub) kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo.
Alitaja mkakati mwingine kuwa ni kuwaelimisha wakulima kuhusu mikopo ya kibenki yenye lengo la upatikanaji wa zana bora za kilimo kwa masharti nafuu na Mfuko wa Pembejeo (AGITF) uwezeshe wakulima upatikanaji wa mikopo nafuu ya zana za kilimo mkoani hapa.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba alisema mkoa umejipanga kusimamia kilimo ili kiwe sababu ya kuondoa umasikini kwa wananchi.
“Mheshimiwa Waziri napenda kukuhakikishia kuwa hapa Singida kazi kubwa ni kilimo tutakifanya usiku na mchana ili tuweze kuwasaidia wananchi wetu na maelekezo yako yote tutayafanyia kazi” alisema Serukamba.
Serukamba alisema awali watu walidhani kuwa kilimo ni jambo la kawaida na la mtu binafsi lakini sasa ni biashara na mkombozi kwa wananchi na kuwa wanazipongeza jitihada zote zinazofanywa na Serikali za kuinua kilimo na wao kama mkoa wanaziunga mkono na kutekeleza maagizo yote waliyopewa.
No comments:
Post a Comment