Na Mwandishi Wetu
Kikosi cha wawakilishi bora wa Michuano ya Afrika, ukanda wa Afrika Mashariki na Kati Simba SC kimeondoka alfajiri ya leo kuwafuata De Agosto ya Angola tayari kwa mchezo wa mkondo wa kwanza wa hatua za awali Ligi ya Mabingwa Afrika CAFCL kuwania kufuzu hatua ya makundi.
Simba wameondoka na Ndege ya kukodi ambayo itawapeleka na kuwatudisha baada ya kucheza hapo kesho kurejea kujiandaa na mchezo wa mkondo wa pili.
Wana Robo Fainali hao wa Kombe la Shirikisho msimu uliopita wameondoka na kikosi cha wachezaji 24 huku wale walioko majeruhi wakisalia kuendelea na matibabu.
Simba wanatarajiwa kushuka dimbani kesho majira ya saa 12 jioni majira ya saa za Afrika Mashariki kuwakabili wenyeji wao De Agosto.
Akizungumza kabla ya kudondoka Kocha Mkuu Juma Mgunda amesema wamejiandaa vema na maandalizi yamekamilika kulingana na aina ya mpinzani wanaenda kucheza nae.
"Maandalizi yamekamilika na tuko tayari kwa ajili ya mapambano, tunatambua nakuheshimu ubora wa wapinzani wetu, tuko tayari kuukabili.
"Katika hatua hizi hakuna mchezo rahisi kama benchi la ufundi na wachezaji tunatambua kuwa jukumu lililoko mbele yetu ni kubwa lakini tunapaswa kufanya vizuri na tuko tayari kwa hilo.
"Kikosi kiko imara ukiachilia vijana wetu watatu, Peter Banda, Jimson Mwanuke ambao walipata kadhi hiyo tulipokuwa Zanzibar na kijana wangu Shomary Kapombe. Wengine wote wako timamu na imara tunaamini wataifanya kazi vyema ya kuiwakilisha Simba na Taifa kwa ujumla." Amesema Mgunda.
Kwa upande wa nahodha John Bocco amesema maandalizi yamekamilika kwa asilimia kubwa na wao kama wachezaji wanafahamu umuhimu wa mchezo ulioko mbele yao.
"Maandalizi yamekamilika kwa ajili ya mchezo ulioko mbele yetu, tunafahamu umuhimu na ugumu wa mechi hii na tumejiandaa kwa hilo.
"Ni hatua kubwa na ngumu lakini kama Simba tunatambua tunapaswa kufanya vizuri Ili kuweza kufuzu hatua ya makundi na kufikia malengo kama Klabu na kuiwakilisha nchi vizuri" amesema Bocco.
No comments:
Post a Comment