Serikali iko makini katika kupanga na kutekeleza mipango yake kwa kutilia maanani suala la ongezeko la idadi ya watu kwa kutatua changamoto ya upatikanaji na kujitosheleza kwa chakula nchini.
Hayo yamesemwa na Rais wa Zanzibar Mhe. Dkt. HUSSEIN ALI MWINYI katika hutuba aliyoisoma kwa niaba yake na Makamo wa pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. HEMED SULEIMAN ABDULLA katika ufunguzi wa Maonesho ya siku ya Chakula Duniani yaliyofanyika katika viwanja vya Chamanangwe mkoa wa kaskazini Pemba.
Amesema katika kutekeleza mipango hiyo serikali imeanzisha Taasisi za utafiti wa kilimo na mifugo pamoja na wakala wa Matrekta na zana nyengine za kilimo kwa lengo la kutatua changamoto zinazoikabili sekta hiyo na kubuni njia bora za uzalishaji kulingana na mazingira pamoja na kurahisisha shughuli za kilimo kwa kutumia zana mbali mbali.
Dkt. Mwinyi amewataka wananchi na wakulima kuchukua tahadhari katika uzalishaji wa mazao ya chakula kwani taarifa za hali ya hewa zinaonesha kuwepo kwa upungufu wa mvua za vuli ambazo zinatarajiwa kunyesha kwa mtawanyiko usioridhisha.
Rais wa Zanzibar amesema kuwa mara nyingi nchi hupatwa na hali kama hii hivyo amewataka wakulima kupanda mazao yanayoweza kuhimili hali ya hewa hiyo na kutumia mbegu za mazao yanayoweza kukomaa kama muhugo, viazi vitamu.mtama na jamii ya kunde.
Aidha Dkt. MWINYI amewaasa wafugaji kufuga mifugo ambayo wanaweza kuihudumia kwa malisho sambamba na kuhifadhi sehemu zote za malisho kwa maslahi ya wanyama hao.
Katika hatua nyengine Rais wa Zanzibar amewataka wananchi na wadau wengine kuacha kuvamia maeneo ya kilimo na misitu pamoja na ujenzi wa kiholela kwa visingizio vya uwekezaji na badala yake kufuata utaratibu wa ujenzi wa makaazi kwa maslahi ya nchi.
" maeneo yote ya kilimo na mifugo pamoja na misitu ni mali hivyo ni vyema kuyatunza na kuyatumia vyema kwa kuongeza tija na juhudi katika uzalishaji wa chakula ili kuweza kujikinga na balaa la njaa” amesema
Sambamba na hayo Rais Dkt. MWINYI amesema kuwa serikali kupitia wizara ya kilimo umwagiliaji maliasili na mifugo itahakikisha inasimamia vyema sekta ya kilimo ili kuongeza uzalishaji wa chakula pamoja na kuwa karibu na wakulima na wafugaji kwa kuwapa huduma, nyenzo na utaalamu ili kuhakikisha nchi inazalisha chakula kingi na chenye kutosheleza pamoja na kuiweka nchi katika hali ya kuwa na uhakika wa chakula.
Pia Dkt. Hussein amesisitiza umuhimu wa kuweka kipaombele katika ulaji wa chakula bora chenye lishe na kuwataka wananchi kujenga utamaduni wa kula vyakula bora, ikiwemo unywaji wa maziwa hususan watoto walio chini ya miaaka mitano (5) ili kupata watu wenye afya, akili na utaalamu unaohitajika.
Amesema serikali imekuwa ikichukua hatua mbali mbali za kuhakikisha upo ukakika wa upatikanaji chakula na lishe bora na kuunda mabaraza na kamati zenye kuhakikisha kuwa nchi inabakia salama na chakula cha kutosha.
Vile vile Rais Dkt. MWINYI amesema kwa sasa serikali inakamilisha ujenzi wa Maghala mawili (2) ya kuhifadhia chakula yenye uwezo wa kuhifadhi tani 2500 unguja na pemba.
Pia Rais MWINYI amesema kuwa serikali tayari imeshakabidhi mashine maalum za uchunguzi wa mazao na vyakula kwa taasisi ya utafiti wa kilimo (ZARI) na ZFDA ili kuhakikisha chakula kinahifadhiwa sehemu salama na wananchi wanakula chakula bora na chenye afya.
Nae waziri wa kilimo, umwagiliaji maliasili na mifugo mhe SHAMATA SHAAME KHAMIS amesema kuwa wizara imejipanga kuhakikisha inaongeza ufanisi mzuri katika upatikanaji wa chakula na lishe bora kwa wananchi wote.
Mhe SHAMATA amesema kuwa wizara kupitia maonesho haya itatoa elimu kwa wananchi wote kujifunza kulima kilimo cha kisasa na chenye tija kwa maslahi ya taifa.
Kwa upande wake katibu mkuu wa wizara ya kilimo,umwagiliaji maliasili na Mifugo Nd. SEIF SHAABAN MWINYI amesema maonesho haya yamefanikiwa kwa kiasi kikubwa kutokana na umoja na ushirikiano uliopo baina ya serikali na mashirika binafsi wa muda mrefu.
Nd.SEIF amesema kuwa maonesho haya ni tofafauti sana na maonesho yaliyopita kwani wizara imepanga kuweka siku maalum ya kuimarisha afya ya kijiji kwa kuwepo unywaji wa maziwa kwa wananchi wote.
Amesema kuwa jumla ya shilingi milioni 170.9 zinatarajiwa kutumika katika maonesho haya ambazo zitatumika kuboresha huduma muhimu maeneo haya na zaidi ya washiriki mia moja (100) wameeshiriki katika maonesho haya wakiwemo taasisi za serikali na taasisi binafsi.
No comments:
Post a Comment