Balozi wa India nchini, Binaya Pradhan akiwasilisha hotuba yake wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Kimataifa wa Ushirikiano baina ya Tanzania na India Jijini Dar es Salaam.
Akifungua Mkutano wa Kimataifa wa Ushirikiano baina ya Tanzania na India leo Jijini Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula, amesema ushirikiano wa Tanzania na India ni wa kihistoria na umekuwa imara nyakati zote, na kwa sasa mataifa hayo yamekusudia kuongeza maeneo ya ushirikiano hususan katika sekta ya filamu.
Balozi Mulamula ameongeza kuwa, maeneno mengine ambayo Tanzania na India zimekusudia kuongeza ushirikiano ni katika sekta ya filamu hasa katika kuwaendeleza wasanii wa Tanzania katika kujifunza zaidi masuala ya uzalishaji wa filamu bora kama wanavyofanya wenzetu wa India.
“Tumekubaliana na Balozi kuwa tufufue ushirikiano katika eneo hili muhimu ili kuwawezesha wasanii wetu hapa nchini kuwa na uwezo wa kutengeneza filamu zenye viwango kama wenzetu wa India,” amesema Balozi Mulamula
Awali Balozi Mulamula amesema ushirikiano wa Tanzania na India umekuwa imara wakati wote kutokana na misingi ya kihistoria iliyowekwa na waasisi wa mataifa hayo mawili, Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julias Nyerere wa Tanzania na Baba wa Taifa la India, Mahatma Gandhi.
Waziri Mulamula amesisitiza kuwa misingi hiyo imesaidia kukuza ushirikiano wa Tanzania na India katika sekta za elimu, afya, maji, ulinzi, utalii, tehama, kilimo, mabadiliko ya tabia nchi, nishati na uchumi wa buluu pamoja na biashara na uwekezaji. Alama ya ushirikiano katika nyanja hizo iliachwa na waasisi wa mataifa haya mawili (Mwl. Nyerere na Mahatma Gandhi) imekuwa chachu ya kuimarisha uhusiano wa Tanzania na India nyakati zote kwa maslahi ya pande zote mbili.
Amefafanua kuwa ushirikiano baina ya nchi hizo mbili umesaidia watanzania 4,500 kufaidika na fursa ya ufadhili wa masomo ya elimu ya juu inayotolewa na Serikali ya India.
Kwa upande wake, Balozi wa India nchini, Binaya Srikanta Pradhan ameongeza kuwa India imekuwa na uhusiano mzuri na Tanzania, ambapo uhusiano huo umesaidia kuimarisha maendeleo baina ya mataifa hayo katika nyanja za elimu, afya, biashara na uwekezaji, kilimo na utamaduni.
“Ushirikiano uliopo baina ya India na Tanzania umekuwa chachu ya maendeleo kwa mataifa yetu na tumeshuhudia mabadiliko makubwa katika sekta za biashara na uwekezaji ambayo yamekuwa chachu ya maendeleo ya uchumi wetu,” amesema Balozi Pradhan.
Nae, Mkurugenzi wa Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni, Achiles Bufure amesema mkutano huo utasaidia kuamsha ari ya vijana kujua ushirikiano kati ya Tanzania na India ulipotoka na unapokwenda.
Mwezi Agosti, 2022, Tanzania na India ziliahidi kuendelea kuimarisha ushirikiano ikiwemo kuhakikisha sekta za afya na nyingine zinaimarika ikiwemo kilimo.
Aidha, India kupitia Hospitali ya Apollo zilisaini mkataba wa makubaliano (MoU) na Kampuni ya Eclipse Group Afrika ya Jijini Dar es Salaam wa kujenga Kituo cha Kisasa cha Kutoa Huduma za Uchunguzi za Magonjwa ya Saratani kinachotarajiwa kuanza kujengwa nchini kuanzia mwezi Novemba 2022.
No comments:
Post a Comment