Mratibu wa TenMet Taifa, Ochola Wayoga.
Na Mwandishi Wetu
MTANDAO wa Elimu nchini Tanzania (TenMet)
imelaani vikali mila potofu ambazo bado zinambagua mtoto wa kike katika
kupata elimu, kama ilivyo kwa mtoto wa kiume. Kwa mujibu wa taarifa
iliyotolewa na Mratibu wa TenMet Taifa, Bw. Ochola Wayoga ikiwa ni
sehemu ya kuadhimisha siku ya mtoto wa kike ulimwenguni inayofanyika
kila Oktoba 11.
Bw. Wayoga amesema ni jambo la kusikitisha kuona
hadi leo bado kuna jamii nchini Tanzania ambazo zinaendekeza mila potofu
zinazokandamiza haki ya mtoto wa kike kupata elimu, licha ya jitihada
zinazofanywa na Serikali na wadau wengine katika kumlinda mtoto wa kike.
"...
Tunatoa wito kwa jamii zote nchini Tanzania kuipa kipaumbele Elimu kwa
mtoto wa kike kama nyenzo muhimu ya maendeleo yao, ukuaji, ushiriki wa
kijamii kiuchumi na maendeleo. Tanzania imepiga hatua za kupongezwa
katika kutunga sera na sheria zinazolinda haki za mtoto ikiwa ni pamoja
na, Sheria ya Haki ya Mtoto ya mwaka 2009 na Mpango Kazi wa Kitaifa wa
Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto (NPAVAMWC 2017/18
-2021/22), ambayo inalenga kulinda na kudumisha ustawi wa mtoto na
kushughulikia ukatili dhidi ya wanawake na watoto," alisema katika
taarifa hiyo.
Hata hivyo, wameipongeza Serikali ya Tanzania kwa
kitendo cha kuridhia kurejea shuleni tena kwa wanafunzi wa kike
waliopata ujauzito ambao huenda waliacha shule kutokana na ujauzito.
Kurejeshwa tena kwa kundi hilo kumekuja hivi karibuni ikiwa ni jitihada
za kushughulikia usawa wa kijinsia katika elimu kama inavyotamkwa
kupitia (Waraka wa Elimu Na. 2, 2021).
Aliongeza kuwa licha ya
maendeleo hayo yanayoonekana bado kuna changamoto katika viwango vya
mpito vya wasichana kwenda kidato cha tano na sita sekondari hali
inayosababisha tofauti kubwa ya kijinsia katika elimu ya sekondari na
elimu ya juu nchini.
"...Takwimu zilizotolewa na Shirika la
UNICEF -2020 zinaonesha kuwa asilimia 31 ya wasichana nchini Tanzania
wanaolewa wakiwa na umri wa miaka 18, huku asilimia 5 kati yao wakiwa
kabla ya umri wa miaka 15. Kimsingi hizi ni takwimu za kutisha ambazo
zinathibitisha idadi kubwa ya wasichana ambao bado wameachwa nje ya
mfumo wa shule kwa sababu ya ndoa za utotoni na umaskini na pia inatoa
wito kwa hatua kali za kukabiliana na changamoto hizi miongoni mwa
nyinginezo," alisema katika taarifa hiyo.
Wakati Tanzania
inapoelekea kuadhimisha miaka 10 ya Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike,
tuhakikishe dhamira yetu ya kutokomeza mila potofu kwa watoto kwa kuweka
mazingira bora ya kupata elimu bora, usawa na kupatikana kwa urahisi.
TEN/MET inaitaka serikali kuchukua hatua madhubuti katika nyanja mbili
za kushughulikia changamoto nyingi zinazomkabili mtoto wa kike katika
kupata haki yake ya kupata elimu nchini.
Marekebisho ya Sheria ya
Elimu ya 1978 Kujumuisha kipengele cha sera ya kujiunga tena kwa
wanafunzi wote wanaokatisha masomo kutokana na sababu tofauti ikiwemo
mimba. Marekebisho haya yatazingatia ajenda ya kuingia tena nchini na
uendelevu wake.
Wakati Tanzania inaelekea kuadhimisha miaka 10 ya
Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike, TEN/MET inaiomba Serikali na wadau
wengine kushirikiana kuhakikisha inaweka mikakati thabiti ya kutokomeza
mila potofu kwa watoto kwa kuweka mazingira bora ya kupata elimu bora,
usawa na kupatikana kwa urahisi.
"Serikali ichukue hatua
madhubuti katika nyanja mbili za kushughulikia changamoto nyingi
zinazomkabili mtoto wa kike katika kupata haki yake ya kupata elimu
nchini. Pia tunapendekeza marekebisho ya Sheria ya Elimu ya 1978
Kujumuisha kipengele cha sera ya kujiunga tena kwa wanafunzi wote
wanaokatisha masomo kutokana na sababu tofauti ikiwemo mimba.
Aidha
alibainisha kuwa mazingira mazuri huwezesha mchakato mzuri wa
ufundishaji na ujifunzaji hivyo basi kuboresha matokeo ya ujifunzaji,
Hivyo ni wakati muafaka kwa serikali kuboresha mazingira ya kufundishia
na kujifunzia kwa kuwekeza katika miundombinu bora hasa katika ngazi ya
shule za msingi.
No comments:
Post a Comment