HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

October 31, 2022

Ugumba; Teknolojia inavyoutafsiri na kuleta matumani kwa mwanamke-2

  Mwonekano tofauti wa mjamzito na mama aliyetoka kujifungua akifurahi na mwanae. PICHA NA MTANDAO

 

NA CHRISTINA MWAKANGALE


KUKUA kwa teknolojia kumerahisisha huduma za kijamii ambazo awali majibu yake hayakupatikana wakati mwingine wala haikuwezekana nyakati za miaka ya nyuma, hususan kwa nchi zilizopo Kusini mwa Jangwa la Sahara (SSA), hasa kwenye sekta ya afya.


Kwenye toleo lililopita lilizungumzia ugumba tatizo linalotokana na sababu mbalimbali na kusababisha, wenza ama waliopo kwenye mahusiano kushindwa kupata mtoto kwa njia ya kibaolojia, teknolojia-tiba ya IVF imeleta matumaini kwa kundi hili.


IVF ni moja ya teknolojia hiyo ambayo inatumika kwa ajili kupandikiza mimba, imeshika kasi barani Afrika na hapa nchini, licha kugundulika zaidi ya miaka 40 iliyopita huko nchini Uingereza. Inaelezwa hadi mwaka jana, idadi ya watoto waliozaliwa kwa njia ya teknolojia hiyo duniani ni milioni nane.


Kwa sasa suala la umri umri kwa aliyechelewa kushika ujauzito, sio tatizo kwa sababu kwa sababu mbinu hiyo ya IVF, imekwishatoa majibu baada ya mwanamke mwenye umri wa zaidi ya miaka 50 kubeba mimba, nchini.


Bingwa na Mtaalamu wa kutengeneza Watoto kwa njia ya teknolojia (Embriologist) kutoka Hospitali ya Kairuki Green IVF, George Tryphone, akizungumza na blog hii, jijini Dar es Salaam, anasema: Watu wana zaidi ya miaka 20 na 30 wameshindwa kupata ujauzito, lakini utakuta mama wa miaka zaidi ya miaka 50 kapata ujauzito.”


“IVF kitaalamu ni huduma inayowasaidia wale waliopata changamoto ya kupata watoto kwa njia ya kawaida na kwa wakati muafaka. Walengwa ni familia ambazo katika makundi mawili, walio katika umri wa kuzaa iwe kwa wanawake au wanaume kundi la pili ni wanaohitaji kutafuta mtoto waliopo kwenye mahusiano ama ndoa,” anasema bingwa huyo.


Anasema mchakato wa matibabu ya aina hiyo, muda wake unategemea iwapo walengwa wanataka kufuata taratibu za upandikizaji za (IVF) kwa kuwa, huchunguzwa ili kutambua tatizo na kuwapa tiba ya  awali.


Anafafanua kwamba, maandalizi hutegemea kama itakuwa njia ndefu au ni muda wa mwezi mmoja na wiki kadhaa na njia fupi itakuwa ni mwezi mmoja tu au isiyozidi miezi miwili.


“Kwa hapa nchini, Julai, mwaka huu tumeweza kuwafanyia huduma akinamama 10 na kati ya hao, saba walifanikiwa, lakini wengine watatu hawakufanikiwa kutokana na changamoto mbalimbali kwa sababu kila mtu na tatizo lake na hilo haliwezi kuendana na la mtu mwingine, tunajipanga, kuwarudia tena.”


MWANZO WA HUDUMA


Tryphone anasema msukumo wa kuanzisha programu hiyo ya IVF, ilianzishwa muda mrefu na marehemu Hubert Kairuki mwaka 1982  alipokuwa nchini Canada. 


Pia, baadae Dk. Clementina Kairuki ambaye ni Daktari Bingwa wa magonjwa ya akinamama kwa sasa aliyebobea katika masuala ya changamoto ya uzazi aliendelea kufanya  utafiti  kwa wakinamama wengi wenye matatizo ya kupata watoto.


“Tatizo linapofika kwa wataalamu na mnakuta hamuwezi kulitatua, inabidi mtu atoke aende nje  na gharama yake huwa ni kati ya Sh milioni 30 na zaidi hata akienda huko inakuwa haina uhakika.


“Unakuta anaenda hajapata na anatamani anarudi tena akajaribu na unakuta wengine ni watumishi wa umma, kachukua mkopo wake sasa inakuwa ni gharama juu ya gharama.” 


“Kutokana na tatizo hilo, mwaka 2016 hospitali, ikaamua kuleta huduma hiyo nchini na kuanza ujenzi wa kituo hicho maalum kwa IVF, huduma ikaanza rasmi mwaka huu, Februari, kuandaa hao 10 na Julai, wakatoa toleo la kwanza, Oktoba mwaka huu tutatoa batch nyingine,” anasema.


“Kwenye huduma hiyo iliyohusisha akinamama 10 kati yao saba wakafanikiwa kupata ujauzito na mmoja mwenye umri wa miaka zaidi ya 50 amepata huduma na ni mjamzito, ni Mtanzania. Tunapokea wanaohitaji huduma kutoka hata nje ya nchi mfano, Comoro, DRC (Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo)  na hao wote hawajawahi kupata watoto kwa vipindi tofauti, mwingine miaka 10 na zaidi.


Anasema wataalamu wa huduma hiyo ni kutoka ndani ya nchi baada ya kupata mafunzo India, Scotland, Uhispania, wengine chuo cha Oxford kwa  muda wa miaka mitatu maalum kwa ajili ya kutoa huduma ya IVF.


WANAOHITAJI HUDUMA


Bingwa huyo anasema mahitaji yanaongezeka na kwa siku wanaofika kwa ajili ya huduma hiyo hospitalini hapo, ni 10 na kwamba huduma hiyo inahitaji muda wa siku mbili za mazungumzo baina ya wenza na bingwa, mwanasaikolojia ili kupata maelezo na utayari wao.


Anasema wapo wanawake ambao hufika hospitalini hapo bila wenza na wanaohitaji mtoto, akisema mbegu zipo ambazo hutolewa na wanaume wachangiaji wanaojitolea bure kama vile wanaochangia damu.


IDADI MAYAI MWANAMKE


Tryphone anasema kinachotokea kwenye mwili wa mwanamke tangu akiwa tumboni mwa mama yake, akiba ya mayai hupindukia 6,000,000 haadi anapokuja kuzaliwa hupungua hadi kufukia 1,000,000.


“Hadi mtoto wa kike anafikia hatua ya kubalehe mayai yanakuwa yamepungua na kufika laki sita au nne, na kila mwezi anavyooenda siku zake mayai yanazidi kupungua. Na watu hudhani mwanamke hupoteza yai kila mwezi hapana, mwanamke huweza kupoteza mayai mengi mwezi mmoja yanakuwa hadi 10 au 15 hata 20,” anasema Tryphone.


Anasema kadri umri wa mwanamke unavyozidi kusonga idadi ya mayai hupungua, na kwamba kibaolojia mwanamke hatengezi mayai bali hupunguzwa kila mwezi ambayo alizaliwa nayo.


“Mwanamke, uolewe, usiolewe, uzae au usizae vyovyote vile kumbuka unayapoteza mayai kila mwezi kupitia siku zako, kibaolojia. Unapofika 'levels' ya miaka 49 au 50 na kuendelea ‘reserve’ (akiba) inakuwa imepungua sana,” anasema.


Anasema tofauti na mwanaume ambaye hutengeneza mbegu kila baada ya siku 90 maisha yake yote, ambazo zina ubora kulingana na mlo na kuwa na uwezo wa kumpa mwanamke ujamzito.


Bingwa huyo anasema kwa mwanamke ambae umri umefika miaka 50 na kuendelea akiba ya mayai ikiwa imeisha na siku zake kukoma si kwamba hawezi kupata ujauzito, hapo suala ni atatungishwa kwa yai gani, ndipo linapokuja suala la kupatiwa yai kutoka kwa mwingine.


“Kwa hiyo akiba ya mayai ikiisha sio suala muhimu, mfuko wa kizazi si bado upo, hapo ndipo huyu mwanamke anachohitaji ni yai la ziada kutoka kwa ‘donor' na kisha linachanganywa na mbegu ya mwanaume, mimba tayari,” anasema bingwa huyo.


WANAWAKE WAGUSWA


Gladness Mathias (47) mkazi wa Kinondoni, anasema tangu alipoona na kusikia taarifa mbalimbali ikiwamo kwenye mitandao ya kijamii, kuhusu kuwapo kwa huduma ya upandikizaji mimba ‘IVF’ nchini, alivutiwa na kutaka kujua gharama na huduma yenyewe.


“Nilibahatika kupata mtoto mmoja miaka kama 10 imepita ingawa kila ninapotaka kutafuta mwingine na mume wangu imepita muda tuseme imeshindikana. Niliwahi kwenda kwenye moja ya hospitali binafsi ipo jijini hapa hapa, gharama zake kubwa mno,” anasema Gladness.


Anasema gharama ya huduma hiyo kwenye hospitali hiyo ni Sh milioni 15 hadi 18, hivyo inamuwia vigumu kwake kulingana na kipato anachokipata


“Hapo watakaomudu gharama ni wenye fedha au matajiri, hayo mamilioni kwa mkuouo mmoja natoa wapi, ingekuwa milioni mbili au tatu, ningesema nitadunduliza kwenye shughuli zangu na mume wangu au hata tukope, watoto ni faraja,” anasema mama huyo.


Theonista Brighton (45), anasema hajawahi kubahatika kuwa na mtoto hadi umri huo, akisema anatamani kuwa mama lakini imebainika anatatizo la kushika mimba kibaolojia na kwamba njia pekee ambayo ingemfaa kwa ushauri wa kitabibu ni IVF.


“Awali nilidhani ni kati ya huduma zilimo kwenye orodha zinazotolewa na bima ya afya (Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya). Mimi Mtanzania wa kawaida Sh milioni 15 naitoa wapi? Nasubiri majaliwa ya Mungu pekee,” anasema Theonista.


MWANASAIKOLOJIA

Joseph Kayinga, Mtaalamu wa Ustawi wa Jamii na Mshauri wa Mahusiano ya Familia, Malezi na Watoto kutoka Asasi ya HERO, anasema binadamu yeyote hujiandaa kuwa mama au baba na kuitunza familia tangu utotoni, hasa kupitia michezo ya utotoni.


“Kupitia malezi katika jamii tunapokuwa kwenye familia, watu tangu wakiwa  watoto hujifunza kwa kuishi na kuona, hata bila ya kuambiwa na mtu yeyote hujifunza namna ya kuwa mwanaume ama mwanamke tangu anapokuwa mtoto mdogo. 


“Nina hakika unaifahamu michezo ya kibaba baba na kimama mama, ambapo watoto hujifunza nakuigiza namna ya kuwa baba na ama mama. Na huwa wanajipanga jinsi wanavyotaka hata kuwa na watoto na familia,” anasema.


No comments:

Post a Comment

Pages