Na Mwandishi Wetu
RAIS wa Klabu Yanga, Hersi Said amewahakikishia mashabiki, wanachama na wapenzi wa timu hiyo, itatinga hatua ya makundi Kombe la Shirikisho Afrika (CAF CC) kwa kuitoa Club Africain ya Tunisia baada ya kukwama Ligi ya Mabingwa.
Yanga itaanzia nyumbani Novemba 2 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam ikiwakaribisha Club Africain mchezo wa mkondo wa kwanza wa mtoano kusaka tiketi ya kutinga hatua ya makundi.
Akizungumza mara baada ya kumalizika mchezo dhidi ya Geta Gold FC jijini Mwanza ambapo Yanga iliibuka na ushindi wa bao (1-0).
Amesema mashabiki wanapaswa kuwa nyuma ya timu wakati wote bila kuwa sehemu ya wanaoibomoa na kuikana pale inapofungwa, huku akisisitiza ushindi kwenye mechi yao ya ligi utawapa hali ya kujiamini kuelekea mchezo huo.
“Nataka niwahakikishie tutasonga mbele kwenda hatua ya makundi, siyo jambo baya kuumia kwa kitu unachokipenda, lakini usiipende Yanga kisa inashinda ikifungwa siyo yako. umeipenda nembo ya Yanga, rangi na klabu, hujaipenda sababu ya matokeo, sisi tunapaswa kuwa na mapenzi na klabu hii na siyo mapenzi na matokeo, kama ni hivyo katafute kitu kingine cha kupenda.”
“Hili tatizo la kuipenda timu ikishinda tuachane nalo na watu kama hao siyo wana Yanga. Mfano Barcelona na Manchester United mara ya mwisho wamechukua ubingwa lini licha ya uwekezaji unaofanywa? Lakini kila siku wako nyuma ya timu yao,” amesema Hersi.
No comments:
Post a Comment