HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

November 01, 2022

Nchi Wanachama Ukanda wa Maziwa Makuu zakumbushwa kuendesha uchaguzi huru na wahaki

 


 

Na Hussein Ndubikile, Dar es Salaam

 

Nchi Wanachama za Jumuiya ya Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu zimekumbushwa kuzingatia kuendesha uchaguzi huru na wahaki unaozingatia usawa kwa wote pamoja na kuheshimu haki za binadamu.

Hayo yamesemwa leo jijjini Dar es Salaam na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu( Sera, Bunge na Uratibu)  George Simbachawene wakati akifungua Mafunzo ya Siku nne ya kuzijengea uwezo Tume za Uchaguzi na wadau wa uchaguzi wa jumuiya ya nchi za ukanda huo (ICGLR.) ambapo mafunzo hayo ni sehemu ya itifaki ya Umoja wa Mataifa(UN) inayohusiana na masuala ya Demokrasia na Utawala Bora.

Amesema kuwa Tume za Uchaguzi za Nchi Nchi Wanachama wa  Jumuiya ya Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu ( ICGLR) zitajadili namna ya kuboresha uadilifu na uchaguzi unaoshirikisha makundi yote katika jamii wakiwemo  wanawake , wazee,Vijana,na Watu Wenye Ulemavu.

Amebainisha kuwa  matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika uchaguzi pia yatajadiliwa,pamoja na fursa zilizopo katika kuboresha ushiriki wa vijana katika uchaguzi ama kama wagombea au wapiga kura ,ambapo pia wajumbe wa mkutano huo unatarajia kujadili  changamoto na fursa zilizopo katika kuboresha ushiriki wa watu wenye ulemavu na wanaoishi kwenye mazingira magumu katika chaguzi mbalimbali.

Amesisitiza kuwa tume za  uchaguzi na Wadau wa uchaguzi wa Jumuiya ya ukanda huo ( ICGLR) zitahakikisha zinaondoa changamoto ambazo zimekua zikisababisha kuwepo kwa siasa chafu na Demokrasi isiyotoa haki sawa kwa makundi yote ikiwemo vijana na watu wenye ulemavu katika kugombea nafasi mbalimbali za uchaguzi.

Ameongeza kuwa  hali ya kuwepo kwa Demokrasia safi husaidia nchi wanachama kuwa na amani na utulivu kwenye mataifa yao,hali ambayo pia inasaidia kuondoa vifo visivyo vya lazima vitokanavyo na masuala ya uchaguzi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Tanzania (NEC), Dkt Charles Mahera amesema kuwa mafunzo hayo yatawasaidia kuwajengea uwezo wajumbe na watendaji wa Tume za Uchaguzi za Jumuiya ya Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu.

Pia amesema kuwa lengo lingine ni kuhakikisha chaguzi zinakuwa huru,za haki na zenye kuaminika ili kusaidia kukuza demokrasia itakayochochea amani , usalama na ustawi wa wananchi.

 Amezitaja nchi  wanachama wa jumuiya ya ukanda huo ni Tanzania,Angola,Burundi, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jamhuri ya Kongo,Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Kenya, Uganda, Rwanda,Sudani Kusini,Sudani na Zambia,

No comments:

Post a Comment

Pages