Kikosi cha Yanga.
Na John Marwa
Klabu za Yanga SC na Azam FC zimeangua vicheko kuelekea michezo yao ya hatua za awali Ligi ya Mabingwa Afrika CAFCL na Kombe la Shirikisho CAFCC.
Yanga wamecheka kwa kuwabugiza mabao (2-1) dhidi ya Ruvu Shooting mtanange uliopigwa Dimba la Benjamin Mkapa.
Licha ya ubora wa kikosi cha Charles Boniface Mkwasa 'Master' na upinzani walioutoa kwa Wananchi bado haukufua dafu na kukubali kichapo hicho kutoka kwa vichwa vya Feisal Salum na Bakari Mwamnyeto huku bao la kufutia machozi la Ruvu Shooting likiwekwa kimiani na Lorand Msonjo.
Ushindi huo umeifanya Yanga kupanda hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa NBC Primier League nyuma ya watani wao kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa wakiwa wamelingana pointi 13 kwa kila timu baada ya kucheza michezo mitano kila mmoja.
Ushidi huo wa Yanga unawapa kujiamini kuelekea mchezo wa mkondo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika CAFCL dhidi ya Al Hilal ya Sudan jumamosi ya wiki hii.
Wakati Yanga wakitakata Azam nao wamezikamua alzeti za Singida Big Stars kwa bao (1-0).
Bao la Azam limewekwa kimiani na Sospeter Bajana akifunga bao kali na kuwapatia wanalambalamba ushindi na point tatu muhimu.
Kimekuwa kipigo cha kwanza kwa Singida Big Stars msimu huu tangu wapande Ligi Kuu wakiwa wamecheza michezo mitano, wameshinda miwili sare miwili na kupoteza mmoja.
No comments:
Post a Comment