HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

November 16, 2022

Serikali yaipongeza Benki ya CRDB


Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia, Nape Nnauye na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela (kushoto) wakiangalia huduma zinazopatikana CRDB Wakala baada ya uzinduzi wa mfumo mpya wa utoaji huduma kupitia CRDB Wakala.



 
Na Mwandishi Wetu

 

SERIKALI imeipongeza Benki ya CRDB kwa ubunifu wa kuboresha huduma kwa wateja na kuongeza ufanisi kwa Mawakala wake.

 

Kuanzishwa kwa huduma za kifedha kwa njia ya simu, pamoja na huduma za benki kwa wakala, kumeongeza upatikanaji wa huduma za kifedha nchini hususan maeneo ya vijijini, na kupunguza gharama za miamala ya kifedha.


Hayo yamesemwa jijini Dar es Salaam na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia, Nape Nnauye wakati wa uzinduzi wa mfumo mpya wa utoaji huduma  kupitia CRDB Wakala ulioshuhudiwa na mawakala wa benki hiyo kutoka Tanzania Bara na Visiwani.


"Benki ya CRDB imeweza kuunganisha mifumo yao ya malipo inayosaidia wananchi kufanya malipo kwa urahisi, lakini pia kuisaidia serikali kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato." amesema Waziri Nape.

 

Alisema katika utekelezaji wa Mifumo na Mipango ya Maendeleo ya Sekta ya Fedha nchini, Serikali imeweka msisitizo mkubwa juu ya umuhimu wa matumizi ya teknolojia za kidijitali katika kukuza ujumuishi wa kifedha na kuleta maendeleo ya kiuchumi.

 

Hii inathibitishwa na matokeo ya tafiti za Finscope zilizofanyika mwaka 2013 na 2017, ambapo uwiano wa watu waliojumuishwa kifedha kwa huduma rasmi za kifedha uliongezeka kufikia asilimia 57 na kisha asilimia 65.

 

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela amesema huduma za CRDB Wakala zilianzishwa mwaka 2012 na zimekuwa zikiboresha siku hadi siku ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia.

 

 "Tunafahamu teknolojia inabadilika kila wakati na inaenda kasi sana lazima tuwe katika sehemu ya kwenda kasi ninafarijika kusema Benki yetu ya CRDB inalitambua sana, tumewekeza kiasi cha kutosha katika  mifumo yetu kuhakikisha huduma zetu zinakuwa za kidijitali, zinapatikana kwa usahihi na zinakuwa salama zaidi" alisema.

No comments:

Post a Comment

Pages