Mgeni rasmi Katibu Tawala (DAS), Karatu,, Faraja Msigwa, akimkabidhi zawadi mshindi wa mbio za Km. 10 Wanaume, Emmanuel Giniki.Rais wa Chama cha Baiskeli Tanzania (CHABATA), Jax Mhagama, akimkabidhi mshindi wa mbio za baiskeli wanawake, Regina Doto (kulia), kutoka Shinyanga.
NA TULLO CHAMBO, KARATU
TAMASHA la 21 la Michezo la Karatu 'Karatu Sports Festival 2022' limefikia tamati kwenye viwanja vya Mazingira Bora mjini Karatu, Manyara huku ule usemi wa Mtoto wa Nyoka ni Nyoka, au 'Ukipanda mahindi lazima uvune mahindi na si Maharage' ukijidhihirisha.
Usemi huo wa Wahenga, umejidhihirisha baada ya kushuhudiwa katika mbio za Baiskeli Kilometa 30 Wanawake, mshindi kuibuka Mama na Mwanaye.
Ikoje hii! Katika mbio hizo za baiskeli ambazo leo zilikabiliwa na hali ngumu kwa washiriki kutokana na mvua iliyonyesha, ilishuhudiwa Regina Doto, akiibuka mshindi huku akifuatiwa na nguli Makirikiri Joseph nafasi ya pili na wa tatu akiwa Regina...
Lakini katika jambo ambalo wengi walikuwa hawalijui, Makirikiri mshindi wa pili, ambaye amekuwa akitawala mbio za baiskeli kwa wanawake kwa muda mrefu hapa nchini akitokea Shinyanga, ndiye mama mzazi wa mshindi Regina Doto.
Makirikiri, ambaye mbali ya kupiga pedeli kwa kasi, pia ni mahiri kukimbia na baiskeli huku akiwa na ndoo ya maji kichwani bila kudondoka.
Akizungumzia matokeo hayo, Makirikiri, alisema anajivunia kuwarithisha mafanikio yake vijana wake, na kwamba siri ya mafanikio ni mazoezi na nidhamu.
Kwa upande wa wanaume, Mkali Masunga Duba wa Simiyu, alikumbana na ushindani mkali kutoka kwa chipukizi Richard Charles wa Shinyanga, aliyeibuka mshindi katika kilomita 60.
Fainali za leo, zilipambwa pia Riadha Kilomita 10 Wanaume na Kilomita 5 Wanawake, huku Emmanuel Giniki kutoka Katesh aking'ara huku Jackline Sakilu wa JWTZ akitesa kwa upande wa wanawake. HABARI ZAIDI...
Wapanda baiskeli wa Shinyanga wenye kutumia baiskeli za kawaida leo wametia fora katika Tamasha la 21 la Michezo na Utamaduni la Karatu baada ya kushika nafasi nne za kwanza katika kilometa 60 za mchezo huo.
Wapanda baiskeli hao pamoja na kutumia baiskeli za kawaida ambazo wengi wanafikiria kuwa hazina kasi,waliwashinda wenzao wa Arusha waliokuwa wakitumia baiskeli za kisasa, ambazo maalumu kwa ajili ya mashindano.
Katika mchezo huo, Richard Charles, Mashanga Dura, Paulo Mihambo na Lameck Shiwelu wote wa Shinyanga walishika nafasi nne za kwanza kwa kutumia saa 1:48.09.22, 1:48.13.66, 1:48.16.35 na 1:50.49.10, huku nafasi ya tano ikienda Arusha kwa Mussa Hussein aliyetumia saa .1:50.50.10.
Katika riadha, Emmanuel Giniki wa Talent ya Arusha na Jackline Sakillu wa JWTZ nao waling’ara katika mbio za kilometa 10 na tano kwa wanaume na wanawake wakimaliza wa kwanza.
Giniki alimaliza wa kwanza katika mbio za kilometa 10 kwa wanaume akitumia dakika 30:01.82 akifuatiwa na Inyasi Sulle naye wa Talent aliyetumia dakika 30:30.01 huku Josephat Bitemo wa Polisi akimaliza watatu kwa kutumia dakika 31:11.54.
Sakillu alimaliza wa kwanza katika mbio za kilome tano kwa wanawake kwa dakika 15:20.91 wakati mwanariadha chipukizi kutoka Serengeti, Neema Nyaisawa alimaliza wa pili kwa kutumia dakika 15:41.19 na Agnes Protas wa JWTZ alimaliza watatu kwa dakika 15:52.19.
Mbali na riadha na baiskeli pia tamasha hilo lilihusisha mpira wa wavu, soka, ngoma, sarakasi na kwaya kutoka vikundi mbalimbali vya sanaa kutoka maeneo mbalimbali ya wilaya ya Karatu.
No comments:
Post a Comment