Kutokana na dhamira hiyo ya
Mheshimiwa Rais Dkt. Samia, Waziri Mkuu ameielekeza Wizara ya Mifugo na
Mamlaka za Serikali za Mitaa kufanya tathmini ya maeneo ya ufugaji
yaliyopo katika maeneo yao na kiasi cha mifugo kinachoweza kufugwa na
endapo mifugo itazidi uwezo wa eneo husika, wafugaji waelekezwe kuvuna
mifugo yao.
Mheshimiwa Majaliwa ametoa
maelekezo hayo leo Desemba 19, 2022 alipofungua mkutano wa
siku mbili wa wadau wa Sekta ya Mifugo unaofanyika katika ukumbi wa
PSSSF jijini Dodoma wenye dhima isemayo “Mwelekeo Mpya wa Sekta ya
Mifugo Nchini.
“Wafugaji wahamasishwe kuvuna
mifugo yao kwa wakati ili kuwawezesha kupata bei nzuri sokoni pamoja na
kupunguza changamoto za malisho hususan wakati wa ukame. Kwa ujumla kasi
ya uvunaji wa mifugo nchini bado ipo chini ya asilimia 10
ikilinganishwa na viwango bora vya uvunaji wa mifugo kitaifa ambavyo ni
kati ya asilimia 20 na 25.”
Waziri Mkuu
amezielekeza Wizara ya Ardhi na Mamlaka za Serikali za Mitaa zihakikishe
zinashirikiana na wadau wa sekta ya mifugo katika kuandaa Mipango ya
Matumizi ya Ardhi ya vijiji na kutenga maeneo ya malisho ya pamoja,
ranchi za vijiji na vitalu kwa ajili ya wafugaji binafsi.
Mheshimiwa
Majaliwa amesema kuwa kwa vijiji vyenye ardhi ya kutosha, vitenge
maeneo ya Ranchi za Vijiji zenye ukubwa wa kati ya hekta 200 na 500
ambazo zitatumika kwa utaratibu wa kuwapanga wafugaji kutoka ndani ya
kijiji husika.
“Wizara ya Mifugo na Uvuvi
ambayo inamiliki Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) ihakikishe maeneo
yote ya NARCO yaliyoko kwenye mikoa yetu, Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa
kwanza mtambue maeneo hayo yanamilikiwa na nani na mjue yapo katika
wilaya gani na yana ukubwa upi na je matumizi ni sahihi kama Serikali
inaotaka.
Kwa sababu tuna watu binafsi
wamechukua ardhi hiyo kazi yao ni kukodisha watu wengine, tumewaacha
wafugaji wenye ng'ombe na tunawajua huyu ana ng'ombe wake 200 huyu ana
ng'ombe wake 300 na tuna eneo la NARCO zuri tu badala ya kumpa hyu
mwenye ng'ombe tumempa mtu ambaye hana ng'ombe tumempa mtu ambaye hana
ng'ombe alafu anakuja kumpangisha mwenye ngombe. Hii Wakuu wa Mikoa
tuikatae wazi.”
Pia, ameiagiza Wizara ya Mifugo
na Uvuvi kwa kushirikiana na wadau na wafugaji kushiriki kikamilifu
katika kuhamasisha mabadiliko ya mfumo wa ufugaji ikiwemo ufugaji wa
kukaa katika eneo moja bila kuhamahama na wafugaji kulima malisho badala
ya kutegemea malisho ya asili peke yake.
“Viongozi
na watendaji wa Serikali, hakikisheni mnashirikiana kwa karibu na wadau
wakiwemo wafugaji katika kuwekeza na kuendeleza ujenzi wa miundombinu
ya mifugo ikiwemo majosho, malambo, visima vya maji na maeneo ya
malisho.”
Waziri Mkuu amesema kuwa uzalishaji
na usambazaji wa mbegu bora za mifugo uimarishwe ili kuongeza tija
katika sekta ya mifugo sambamba na kuwahamasisha wafugaji kutumia mifugo
bora iliyofanyiwa utafiti na kuonesha kuwa na tija zaidi.
Pia,
Mheshimiwa Majaliwa ameelekeza wizara husika kuimarisha huduma za ugani
kwenye sekta ya mifugo kwa kuweka vigezo vya kupima utendaji kazi na
kuwafuatilia Wagani wote nchini ikiwa ni pamoja na kuhimiza matumizi ya
TEHAMA, kuendelea kuwapatia vyombo vya usafiri na mafunzo rejea kuhusu
teknolojia mpya za ufugaji wenye tija na wa kibiashara.
Aidha,
Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Mifugo na Uvuvi ishirikiane na Wizara
ya Mambo ya Ndani ya Nchi katika kutatua migogoro baina ya wafugaji na
watumiaji wengine wa ardhi. Pia wafugaji waelimishwe na kuhamasishwa
kufuga kulingana na maeneo waliyonayo na kufuata sheria za nchi.
Awali,
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mashimba Ndaki alisema lengo la mkutano huo
ni pamoja na kuwaleta pamoja wadau wa sekta ya mifugo kujadili kwa kina
na uwazi kuhusu mwelekeo mpya wa sekta ya mifugo nchini na kuwajengea
uwezo wafugaji ili wafuge kwa tija na kibiashara kama wawekezaji kwenye
sekta ya mifugo.
Pia, Waziri Ndaki alisema Sekta ya Mifugo
inakabiliwa na changamoto mbalimbali, hivyo watatumia mkutano huo
kujadili namna ya ufugaji bora pamoja na kukabiliana na athari za
mabadiliko ya tabianchi. “Tumepanga namna ya kuwafikia wafugaji na
kuwaelimisha juu ya matokeo ya athari hizo kwani sehemu kubwa ya mifugo
imeathirika.”
No comments:
Post a Comment