Na Hussein Ndubikile, Dar es Salaam
Serikali imewahakikishia Wahitimu wa kozi mbalimbali za Usafirishaji kuwa itaendelea kuwekeza kwenye miundombinu ya usafiri na usafirishaji sambamba na kuzingatia ongezeko la wataalam ili kuhakikisha miundombinu inasimamiwa kwa kuzingatia weledi.
Hayo yamesemwa jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri wa Uchukuzi Atupele Mwakibete katika Mahafali ya 38 ya Chuo cha Taifa cha Usafirishaji Nchini (NIT) ambapo amesema soko la ajira katika sekta ya usafirishaji limeongezeka sanaa kutokana na maboresho mbalimbali yanayofanywa na Serikali kwenye bandari, ujenzi wa meli, viwanja vya ndege, na ununuzi wa ndege.
“Sekta ya usafiri na usafirishaji inakuwa kila siku na uwekezaji unaendelea kufanywa kwenye miundombinu, nyinyi kama wahitimu mtaweza kupata ajira kwenye maeneo ya reli, bandari na viwanja vya ndege kupitia uwekezaji huu”, amesema Naibu Waziri Mwakibete.
Naibu Waziri Mwakibete ametumia fursa hiyo kuwaasa wahitimu kuzingatia misingi ya uadilifu waliyofundishwa kwani usimamizi wa miundombinu unahitaji nidhamu na uadilifu ili kuifanya iweze kudumu kwa muda mrefu.
Aidha Naibu Waziri Mwakibete ameipongeza NIT kwa kuhakikisha inaongeza kozi katika njia tano za usafirishaji na kupunguza gharama kubwa inayotumia Serikali kwa kuwasomesha wataalam wa fani hizo nje ya nchi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha NIT, Profesa Zacharia Mganilwa amesema kwa sasa chuo kimeongeza udahili na kufikisha wanafunzi zaidi ya elfu kumi na mbili kwa mwaka 2022 ikilinganishwa na wanafunzi elfu sita kwa mwaka 2020.
Profesa Mganilwa ameishukuru Serikali kwa kutoa fedha za kununua ndege mbili zenye injini moja kwa ajili ya shule ya usafiri wa anga zitakazosaidia wanafunzi wa urubani na uhandisi wa ndege.
Nae, Mbunge wa Jimbo la Manonga Mkoani, Tabora Seif Gulamali ambaye ni mwanafunzi aliyewahi kusoma chuoni hapo ameiomba Serikali kuharakisha mchakato wa kuanzisha Bodi ya Usafirishaji ili kuendeleza tasnia hiyo kwa kuzingatia weledi.
Katika Mahafali ya 38 wanafunzi zaidi
ya elfu mbili mia saba wametunukiwa shahada za uzamili, shahada,
stashahada za juu, shahada na astashahada katika maeneo mbalimbali ya
Usafirishaji.
No comments:
Post a Comment