Na John Richard Marwa
Mabingwa mara 22 wa Ligi Kuu Soka Tanzania Bara NBC PL, Simba SC wamezipigia simu nzito klabu wenza wa Ligi hiyo kwa kwatandika kono la Nyani 0-5) Geita Gold FC mtanange uliolindima Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Ulikuwa mchezo wa haja kwa pande zote mbili ukifungua mzunguko wa pili wa msimu huu ikiwa ni raundi ya 16, Mnyama alianza kuufanya unyama kupitia kwa John Bocco akiunganisha kross safi ya Shomary Kapombe.
Simba waliamua kucheza kikubwa kama vile walisikia king'ora cha Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF CL) kumbe yalikuwa mawimbi ya Ziwa Victoria.
Clatous Chota Chama Mwamba wa Lusaka akaweka kamba ya pili kikatili sana mbele ya Mkongwe Kelvin Yondani.
Show za Chama ziliendelea katika nyasi za Kirumba na miamba ikaitika kwa kupiga mdundo wa hakuna huruma, Chama tena akaweka assist kwa Pape Sakho akifunga bao la kikatili kweli kweli dakika za mwanzo za kipindi cha pili.
Geita walijaribu kila mbinu kufurukuta lakini wakajikuta maumivu yanazidi kwa Sakho tena kuwasulubu kwa bao la nne la umbali mrefu haswa.
Simba ni kama walinogewa na namna walivyokuwa wanaziyeyusha Dhahabu za Geita Chama akaweka tena assist yake ya tisa msimu huu kwa Kibu Denis na kuhitimisha msumali wa mwisho kwa vijana wa Kocha Felix Minziro.
Licha ya kipigo hicho walijaribu kila mbinu za kutaka kuweka mambo sawa lakini Simba waliamua kuwakabidhi nyaraka nzito za msimu huu kwa kuwapa maswali nane bila majibu.
Mzunguko wa kwanza raundi ya kwanza Simba walichalaza Geita mabao (3-0) Uwanja wa Benjamin Mkapa na sasa msimu huu Geita wamepoteza michezo yote miwili kwa jumla ya mabao (8-0).
No comments:
Post a Comment